Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewahakikishia wakazi wanaohama kwa hiari yao kutoka katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro kuelekea kijiji cha Msomera, Handeni Mkoani Tanga, kuendelea na shughuli zao za ufugaji katika mazingira yaliyo bora.

Majaliwa ameyasema hayo hii leo Juni 23, 2022 wakati akiwaaga wakazi wa Ngorongoro wanaohama kwa hiari yao kupisha shughuli za uhifadhi katika eneo hilo, katika viwanja vya Ofisi Kuu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCCA), Ngorongoro Mkoani Arusha.

“Ninawaomba msafiri kwa amani kabisa na mioyo yenu ikunjuke isikilizeni Serikali yenu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan sasa hivi mko huru, nendeni mkakae kwenye nchi yenu kwa uhuru,” amesisitiza.

Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro, Dkt. Christopher Timbuka amesema awamu ya pili ya zoezi la kuwahamisha wakazi wa eneo la Ngorongoro kwa hiari lilianza Juni 20, 2022, ikihusisha jumla ya kaya 27 zenye watu 127 na mifugo 488.

Amesema hadi sasa kaya zilizohama kwa hiari katika eneo la Ngorongoro katika awamu ya kwanza na ya pili ni 48 zenye jumla ya watu 233 na mifugo 899 na kwamba utaratibu wa kuwahamisha umefanyika kwa kufuata hatua mbalimbali ikiwemo kuhakiki idadi ya watu.

“Hatua nyingine ni kusainisha vitabu vya fidia vya wakazi wanaohama kwa hiari awamu ya pili, kuhakiki idadi ya mifugo na kuiweka alama ili iweze kusafirishwa pamoja na kuhakiki na kutambua aina za nyumba za wakazi hao kwa ajili ya taratibu za ubomoaji,” amefafanua Dkt. Timbuka.

Hata hivyo, amesema mbali na kupewa nyumba, fidia na shamba, kaya zote zitapewa magunia mawili ya mahindi kwa kwa kipindi cha miezi mitatu ili waweze kujikimu kwa kipindi cha mpito wakati wakijiandaa na msimu wa kilimo.

Mmoja wa wakazi wanaohama kwa hiari kutoka Ngorongoro kwenda Msomera, Emmanuel Saitoti wa Kijiji cha Nainokanona, ameishukuru Serikali kwa upendeleo ilioutoa kwao kwa kuwa mbali ya kupewa nyumba pia Msomera wanakwenda kupata fursa zitakazowakuza kiuchumi.

Amesema, “Serikali tunaishukuru imetupendelea sana, tumepata hati za nyumba na mashamba pamoja fidia ya fedha, naishauri iendelee kuwahamasisha na wakazi wengine nao wahame kule hakuna maendeleo. Msomera tunakwenda kufanya shughuli nyingi za maendeleo.”

Tanzania yazidi kupaa Kimataifa
Kisa Morrison, Bumbuli aisemea mbovu Simba SC