Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kuhakikisha kwamba programu zote zinazotolewa na taasisi za elimu ya juu zinawawezesha wahitimu kujiajiri na kuwa na sifa za ushindani katika soko la ajira kimataifa.

Majaliwa ametoa agizo hilo wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 12 ya Elimu ya Juu, jijini Dar es Salaam, ambapo amesema kuwa wakati umefika sasa kwa wasomi katika vyuo vyetu vikuu tujiridhisha kuwa mitaala inayotolewa kama inawaandaa wahitimu kupata taaluma na stadi za kuweza kujiajiri na kupambana na changamoto za kimaisha.

Amesema taasisi za elimu ya juu nchini ziangalie mitaala yake na kuimarisha mfumo wa ithibati na udhibiti wa ubora wa elimu na mafunzo ili kwenda sambamba na dunia ya kazi inayoendana na agenda ya maendeleo ya Taifa.

Pia ameeleza kuwa maonesho hayo ni jukwaa la kipekee ambalo litaibua mjadala sahihi kuhusu uhalali wa kozi zinazotolewa na vyuo husika vya elimu ya juu. “Hivyo mnayo nafasi ya kuonesha kwa vitendo uwezo wenu katika utafiti, ubunifu na matumizi ya sayansi na teknolojia zinazotumika katika maendeleo ya viwanda.”

Amesema taasisi za elimu ya juu ziweke mikakati ya kuinua na kuboresha taaluma  wanayoitoa ili ilete tija kwa maendeleo ya Taifa na Dunia. Pia kuanzisha program za mafunzo zenye kukidhi mahitaji na kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kuzingatia mahitaji ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Aidha, Majaliwa amezitaka taasisi hizo kuendelea kuimarisha mfumo wa udahili na kujipanga kutumia fursa za elimu na mafunzo ndani na nje ya nchi kwa makundi yote ya jamii kwa usawa katika ngazi zote hususan ufundi, hisabati, sayansi na teknolojia.

Amesema ni wakati muafaka kwa taasisi za elimu ya juu nchini kuandaa mikakati ya kuongeza udahili kwa kuzingatia mahitaji ya rasilimali watu na ujuzi unaohitajika katika sketa zinazokua haraka mfano mafuta, gesi na madini.

Video: Makonda atoa siku ishirini kubomolewa Baa, Gesti Dar es salaam
Video: Makonda kuboresha shule zilizochakaa Dar