Katika kuhakikisha kuwa Serikali inatetea maslahi ya wakulima na kuimarisha shughuli za kilimo nchini, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kusimamia biashara ya mazao mbalimbali katika maeneo yao ili wakulima waweze kunufaika.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ilasilo kilichopo mpakani wa Mkoa wa Mbeya na Songwe alipokuwa njiani kuelekea Wilayani Songwe kwa ajili ya ziara ya kikazi.

Majaliwa amesema kuwa kwa sasa bodi ya mazao mchanganyiko inazunguka nchi nzima kutafuta taarifa za bei za mazao ili kubaini bei zinazotumiwa na wanunuzi wa mazao hayo kama zinastahili baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wakulima wa eneo hilo.

“Wakulima msikubali kuuza mazao ovyo, wekeni na akiba ya chakula. Pia  Bodi ya Mazao Mchanganyiko itakuja hapa kwa kuwa sasa inapita sehemu mbalimbali kupata taarifa za bei za mazao pamoja na kuwatafutia masoko yenye tija.”amesema Majaliwa.

Aidha, Majaliwa amewaagiza wale wote wanaohusika na suala la usambazaji wa pembejeo kuhakikisha wanazifikisha kwa wakulima katika kipindi kisichopungua muda wa miezi miwili kabla ya kuanza kwa msimu ili kuwaondolea changamoto ya uchelewashwaji wa huduma hiyo

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Gallawa amesema kuwa changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya kilimo ni kutokuwepo kwa soko la uhakika la mazao pamoja na uingizwaji wa pembejeo zisizofaa katika mkoa

 

Hata hivyo, Gallawa ametaja mikakati waliyojiwekea katika kukabiliana na changamoto hiyo kuwa ni kufanya ukaguzi kwenye maduka yote yanayouza pembejea pamoja na kutoa elimu ya kutambua pembejeo zisizofaa ili watoe taarifa mapema na wahusika wachukuliwe hatua

Video: Fanyeni kazi usiku na mchana kukamilisha barabara ya Kibondo-Nyakanazi-JPM
Mawakili wa Trump watofautiana na msemaji wao, aamua kujiuzuru