Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa msimamo na nguvu ya Serikali katika vita dhidi ya Rushwa na ufisadi nchini na kuwatahadharisha wanaodhani kuwa ni nguvu ya soda.

Akiongea juzi na watanzania waishio jijini Lusaka nchini Zambia, Majaliwa alisema kuwa Serikali itaendelea kuwasaka na kuwachukulia hatua mafisadi na wala rushwa bila kukoma.

“Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kupambana na wala rushwa na mafisadi. Wala hatutanii. Hawa tutacheza nao na wala wasidhani vita hii ni nguvu ya soda. Tutaendelea kuwasaka hadi tufike mwisho,” alisema Waziri Mkuu.

Aidha, Waziri Mkuu alisema kuwa Serikali imedhamiria kurudisha heshima katika utumishi wa umma kwa kuhakikisha wananchi wanaofika katika ofisi za umma wanasikilizwa na kuhudumia bila kuombwa rushwa.

“Hatutaki tabia iliyokuwepo ya mwananchi anakuja ofisini kutaka huduma lakini hasikilizwi hadi atoe chochote, sisi hiyo tabia hatutaki kuisikia kabisa. Tumedhamiria kurudisha heshima kwenye utumishi wa umma na nimeanza kupata faraja kwani sasa hivi (nimeambiwa) katika baadhi ya taasisi unasikia mtu akiulizwa una shida gani, nenda pale, jambo ambalo zamani halikuwepo,” alieleza.

Alisema Serikali haitawavumilia watumishi wazembe, wanaokwenda kinyume na taratibu za utumishi na kushindwa kuwatumikia Watanzania lakini haitamuonea mtumishi yeyote.

“Hapa tunasisitiza usawa na hatutaki kutengeneza gap kati ya mwananchi mtumishi na wa mwananchi wa kawaida, tunataka kila mwananchi aione Tanzania ni nchi yake na kila kinachozalishwa ni sehemu yake. Tukifika hapo, tunaamini kila mmoja ataweza kuisemea nchi yake.”

Pia, aliwataka watumishi hao kuhakikisha wanasimamia kwa uadilifu miradi ya maendeleo ili kukamilisha nia ya Serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo baada ya kuongeza bajeti ya maendeleo kutoka asilimia 27 hadi asilimia 40.

“Ole wake atakayepokea fedha hizi halafu zisifanye kazi yake, ukiipoteza wewe utafute njia ya kwenda,” Waziri Mkuu alionya.

Alisema Serikali imechukua uamuzi huo ili kuhakikisha inawatoa wananchi katika uchumi wa chini hadi kufikia uchumi wa kati na kwamba hilo litawezekana kwa kuwekeza katika uzalishaji wa viwanda vya ndani.

Antonio Conte Amuweka Njia Panda Alexandre Pato
Victor Wanyama Autikisa Uongozi Wa Southampton