Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewaagiza waalimu wanaoishi mbali na shule zao wakati zina majengo wahame mara moja na warudi kuishi kwenye nyumba za shule.

Amesema haiwezekani  walimu waishi mbali na maeneo ya shule kwani hali hiyo inachangia uchelewaji kazini na inapunguza muda wa kuwasimamia wanafunzi au kuwasaidia jioni pale wanapohitajika kufanya hivyo.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Chingumbwa, kata ya Mbekenyera, wilayani Ruangwa kwenye mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi kijijini hapo.

“Nimeambiwa kuwa walimu wako wachache kwa sababu hapa shuleni hakuna nyumba za kuishi walimu. Mbona wanakaa Mbekenyera? Watawezaje kuwahi kazini asubuhi wakati hawana magari? Mvua ikinyesha watafikaje shuleni? Kuanzia leo, walimu wote warudi mara moja na waje kupanga hapa kijijini kwa sababu nyumba zipo,” amesema Majaliwa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa,  Andrea Chezue asimamie zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha anapunguza walimu walioko Ruangwa mjini na kuwahamishia shule za vijijini ambako kuna upungufu wa walimu.

Sumaye, Lowasa wamfariji Lema Mahabusu
TRA yanasa wakwepa kodi jijini Dar es salaam