Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewanusuru viongozi 19 wa vyama vikuu vya ushirika vya mikoa ya Shinyanga (SHIRECU) na Mwanza (NCU) wasiende selo na huku akiwataka kuandaa taarifa ya mali za vyama hivyo ndani ya siku 23.

Viongozi hao wanatuhumiwa kuhusika na upotevu wa mali zilizokuwa zikimilikiwa na vyama hivyo vya ushirika. Waziri mkuu amefikia uamuzi huo kwenye kikao cha wadau wa Pamba mkoani Shinyanga.

“Nataka kila mtu akaandae taarifa kuhusu mali za ushirika zilipo, au zimeenda wapi na kama mlizikopea, mseme ni wapi, lini na kwa ridhaa ya nani. Nataka maelezo ya kutosha kuniridhisha mali za ushirika zimeenda wapi,” amesema Waziri Mkuu.

Badala ya kuchukuliwa na RPC ili wakatoe maelezo kwenye mahojiano na polisi lakini Waziri Mkuu ametaka akutane nao ofisini kwake Dodoma ifikapo Januari 15, 2018 saa 3:30 asubuhi.

Majaliwa amewataja viongozi hao kuwa ni Murtazar Alloo ambaye ni mnunuzi wa maghala matatu mali ya NCU, Bw. Samson Ng’halida (mnunuzi wa New Era Oil Mills), Bw. Amos Njite Lili (mnunuzi wa ghala la Igogo), Bi. Antonia Zacharia (mnunuzi wa jengo la KAUMA), Bw. Timothy Kilumile (mnunuzi wa jengo la KAUMA).

Wengine ni Bw. Robert Kisena (mnunuzi wa pili wa New Era Oil Mills), Bw. Peter Ng’hingi (aliyekuwa Mjumbe wa Bodi), Bw. Daniel Lugwisha (aliyekuwa Mhasibu Mkuu – NCU), Bw. George Makungwi (aliyekuwa Afisa Miliki – NCU) na Bw. Sospeter Ndoli (aliyekuwa Afisa Utumishi -NCU).
 

Video: Mwalimu asimulia mateso ya mtoto aliyefanyiwa upasuaji mara kumi
Manara: Ni aibu ya mwaka