Katika kuhakikisha kuwa Shirika la Nyumba Tanzania (NHC) linafika katika maeneo mbalimbali ya nchi, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameliagiza Shirika hilo kwenda kujenga nyumba bora za makazi katika maeneo yote mapya ya utawala ikiwemo mikoa na wilaya ili kusaidia kutatua changamoto ya makazi kwa watumishi.

Ameyasema mapema hii leo wakati akiweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa nyumba 20 za watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Momba Mkoani Songwe zinazojengwa katika kijiji cha Tindingoma, unaojengwa na Shirika la Nyumba Nchini (NHC).

Majaliwa ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Naming’ongo wilaya ya Momba akiwa katika ziara yake ya kikazi Mkoani Songwe.

“Nalipongeza Shirika la Nyumba kwa mikakati waliyonayo ndani ya shirika hilo na kwamba waendelee na utekelezaji wa mipango hiyo ya ujenzi wa nyumba ili maeneo yote mapya ya utawala yaweze kuwa na makazi bora ya kuishi watumishi.”amesema Majaliwa.

Hata hivyo,  Majaliwa amewataka wakazi wa kata ya Chitete yaliko makao makuu ya wilaya ya Momba  kuhakikisha wanachangamkia fursa ya uwepo wa makao makuu wa wilaya kwenye kata yao kwa kujenga nyumba za kisasa kwa ajili ya kupangisha watumishi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu amesema kuwa mradi huo wenye thamani ya sh. bilioni 2.2 ulianza kujengwa Machi 2016 na unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu.

 

 

Katibu wa habari Ikulu ajiuzulu kupinga uamuzi wa Rais Trump
Majaliwa awapa miezi mitatu kubomoa nyumba zao kwa hiari