Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali imeweka mikakati ya kutosha itakayowezesha pamba yote inayolimwa nchini kununuliwa na tayari imeshaanza mchakato wa kutafuta masoko ya ndani na nje ya nchi.

Ameyasema hayo Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa Sumve, Richard Ndassa wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo.

Ndassa alitaka kujua Serikali imejipangaje kuwasaidia wananchi walioitikia wito wa kulima pamba iwapo wanunuzi watashindwa kununua pamba yote.

Majaliwa amesema ni kweli kuwa mwishoni mwa mwaka jana, Serikali iliwaita viongozi hao ambao ni Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya ambao walipewa maelekezo ya kwenda kuhamasisha kilimo cha zao hilo na kuwasaidia wakulima kuanzia ngazi ya awali.

“Mimi mwenyewe mwezi huu nitakuwa na ziara ya kikazi mkoani Mwanza, kwa hiyo kati ya tarehe 15-17, nimeitisha mkutano wa wafanyabiashara wote wa pamba nchini iwe ni wanaosokota nyuzi, kuchambua pamba au kukamua pamba, ili mradi wanajihusisha na pamba,” amesema Majaliwa.

Aidha, amesema Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Kampuni ya Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) inawasiliana na mataifa mbalimbali ili kuhakikisha pamba yote iliyolimwa nchini inanunuliwa.

Hata hivyo, ameongeza kuwa hapo awali wakulima wa mazao makuu matano ya biashara nchini likiwemo na zao la pamba walipunguza uzalishaji baada ya kukosa usimamizi hali iliyoilazimu Serikali ichukue uamuzi wa kuyafufua kwa kuwa historia inaonyesha kuwa mazao hayo yanachangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

 

Magereza yaeleza sababu za kumzuia Profesa Jay kumuona Sugu gerezani
Mahakama yamnyeshea aliyemuua mwanamke kwa ngumi moja