Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema serikali imetenga zaidi ya shilingi Bilioni 9 kwa ajili ya kuendeleza mafunzo ya uanagezi yanayotolewa kwa vijana kwa lengo la kuwapa ujuzi wa kufanya shughuli mbalimbali na kujiajili.

Akizungumza katika uzinduzi wa awamu ya tatu wa mafunzo hayo, mkoani Mbeya, Waziri Mkuu amesema, tayari serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuendeleza mafunzo hayo ambayo yamekuwa na mwitikio chanya kwa vijana wengi hapa nchini.

Waziri Mkuu Majaliwa, amesema kuwa mafunzo hayo yanawawezesha vijana kupata ujuzi na kuwawezesha kuanzisha shughuli zao kwa kutumia ujuzi wanaopatiwa wakiwa vyuoni.

Ameongeza kuwa, stadi za mafunzo hayo zimeonesha kusaidia wananchi ambao baada ya mafunzo hayo huajiriwa ama kujiajiri wenyewe katika fani walizosomea wakiwa vyuoni.

Pia amezitaka taasisi za fedha kuona namna ya kuwawezesha mikopo viajana hao ili waweze kuendeleza ujuzi wanaoupata kwa manufaa yao na jamii kwa ujumla.

Sambamba na hayo pia amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri zote hapa nchini kuhakikisha wanawasimamia vijana hao na kuwawezesha kupata mitaji itakayowaendeleza baada ya kuhitimu mafunzo

Hii ni awamu ya tatu ya mafunzo ya Uanagezi kwa vijana ambapo zaidi ya vijana elfu kumi na nne wanapatiwa mafunzo hayo katika vyuo zaidi ya 70 katika mikoa yote ya Tanzania Bara.

Tanzania, Rwanda kuendeleza uhusiano uhamiaji,elimu,afya
Waziri Jr ataka kiatu Kagame CUP