Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka asasi za kiraia nchini (AZAKI), kuendelea kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa ulipaji kodi ambazo mbali na utekelezaji wa miradi pia huchangia ukuaji wa sekta mbalimbali.

Ametoa wito huo Novemba 4, 2019 wakati akizindua na kuhutubia wananchi na washiriki wa maonesho ya wiki ya asasi za Kiraia (AZAKI) nchini inayofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ambayo yanatarajia kufikia kilele chake ijumaa Novemba 8, 2019.

Amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa mashirika yasiyo ya Kiserikali katika kusukuma gurudumu la maendeleo nchini ikiwemo kuwajengea uwezo viongozi wa Serikali za Mitaa wakiwemo Madiwani, viongozi wa vijiji na mitaa kutekeleza majukumu yao.

“Serikali inatambua mchango wa AZAKI katika kuhamasisha wananchi kushiriki shughuli za maendeleo, kupata ujuzi wa utoaji huduma za kijamii kama elimu, afya, upatikanaji wa maji, huduma za kisheria na kaadhalika lakini pia msiache kuendelea kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa kulipa kodi,” amesema Waziri Mkuu.

Majaliwa amefafanua kuwa AZAKI imekuwa ikichangia mambo mbalimbali kwa ustawi wa jamii na kuitaka kuleta teknolojia mpya na rahisi kwa wananchi pale wanapoona kuna uhitaji na kwamba wawe mstari wa mbele kuisaidia Serikali kupinga mila potofu na kandamizi hasa kwa makundi yenye mahitaji maalum.

Aidha Waziri Mkuu pia ametumia fursa hiyo kuzitaka AZAKI nchini kuzingatia sheria iliyofanyiwa marekebisho ya mashirika yasiyo ya Kiserikali Na. 24/2002 na kanuni zake, ambayo ilipitishwa na Bunge kwa sheria Na. 3/2019 na kusisitiza kuwa marekebisho hayo yalilenga kuboresha sekta hiyo.

“Niwahakikishia kuwa marekebisho hayo yalilenga kuboresha sekta ya NGOs na siyo kuyabana mashirika yasiyo ya Kiserikali kama ambavyo imekuwa ikipotoshwa na baadhi ya watu na yalizingatia misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,” amesema.

Kuhusu mapato ya AZAKI Waziri Mkuu amesema yanaweza kusaidia ujenzi wa miradi mikubwa inayoonekana kwani kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka huu Serikali ilifanya mapitio ya ufadhili wa fedha wazopata AZAKI kwa taasisi 92 na kubaini kuwa zilipokea kiasi cha shilingi bilioni 261.059.

Ameongeza kuwa kwa mwaka 2016 /2017 Serikali pia iliangalia mapato ya NGOs 51 na kugundua kuwa katika kipindi cha miaka miwili zilipokea shilingi trilioni 2.5 ambazo kama fedha hizo zingeratibiwa vizuri kwa kupunguza matumizi yasiyo na umuhimu zingefanya jambo kubwa la kimaendeleo.

“Matumizi sahihi ya fedha hizo yangetufikisha mbali kimaendeleo tumieni fedha hizi vizuri badala ya kulipana posho na mambo mengine yasiyo ya kimaendeleo maana fedha hizi za ufadhili zinaweza kusaidia ujenzi wa miradi mbalimbaki inayoonekana,” amesisitiza.

Kuhusu suala la ajira kwa vijana Waziri Mkuu Majaliwa amesema ni kundi lenye umuhimu mkubwa kwa Taifa katika kutekeleza shughuli mbalimbali za kimaendeleo kwa nchi na binafsi licha ya kuwa eneo hilo linakabiliwa na uhaba wa upatikanaji wa ajira.

Amesema sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 inaonesha asilimia 35 ya watanzania wote ni vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 na kwamba kwa matokeo hayo utafiti wa nguvukazi ya Taifa wa mwaka 2014 vijana wamebainika kuwa ndio kundi kubwa la nguvukazi ya Taifa kwa asilimia 56.

“Kila mwaka, kumekuwa na ongezeko la vijana wanaoingia kwenye soko la ajira kwa mfano taarifa ya hali ya ajira ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) ya mwaka 2019 inaonesha kuwa asilimia 11.8 ya nguvukazi ya vijana duniani ambao ni takribani vijana million 59.1 hawana kazi,” amesisitiza Majaliwa.

Kwa upande wake Waziri wa nchi ofisi ya Rais tawala za mikoa na serikali za mitaa Seleman Jafo alizishukuru asasi zote za kiraia ambazo zinafanya kazi nchini kwani zimekuwa zikiwahudumia wananchi kwa ukaribu na kusisitiza ziendelee kutimiza majukumu yao kwa weledi ili kufanikisha malengo kusudiwa.

“NGOs hizi zimekuwa zikisaidia kutoa elimu kwa wananchi kuhimiza mambo ya kimaendeleo kiafya, kielimu na hata kutoa ajira hivyo tunazishukuru kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa maeneo mengi nchini Tanzania kwa kushirikiana na ofsi ya Rais TAMISEMI,” amesema Jafo

Awali akimkaribisha Waziri Mkuu na washiriki wa maonesho hayo Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Ummy Mwalimu amesema kwa mwaka huu wizara yake imesajili mashirika yasiyo ya kiserikali 617 ikilinganishwa na mashirika 385 yaliyosajiliwa kwa mwaka 2017.

Amesema kati ya mashirika hayo 617 yaliyosajiliwa 44 ni yale ya ngazi ya kimataifa, 551 ngazi ya kitaifa, saba ngazi ya mikoa na 15 ni katika ngazi ya wilaya ambapo hadi kufikia Oktoba 30, 2019 wamesajili mashirika 19,318.

Maonesho ya wiki ya asasi za Kiraia (AZAKI) nchini yanayofanyika katika uwanja wa Jamhuri uliopo jijini Dodoma yamezinduliwa rasmi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na yanatarajia kufikia kilele chake siku ya ijumaa Novemba 8, 2019.

Mawimbi ya runinga mbioni kufikisha huduma ya intaneti vijijini
LIVE BUNGENI: Tazama Maswali na Majibu, Bungeni Dodoma leo Novemba 5, 2019 katika Bunge la 11