Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezitaka bodi za mazao nchini kujisajili kwenye alama za msimbomilia inayosimamiwa na GS1 Tanzania kwa lengo la wakulima kunufaika na uuzwaji wa bidhaa hizo nje ya nchi. bodi hizo ni za mazao ya chai, korosho, kahawa, pamba na sukari.

Ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa Saba wa Wadau wa Msimbomilia ulioendana sambamba na uzinduzi wa siku maalumu ya Waziri Mkuu na Msimbomilia ambayo itakuwa ikiwakutanisha wazalishaji nchini kujadiliana maendeleo ya viwanda.

Amesema kuwa bodi za mazao zinapaswa kutambua nafasi ya msimbomilia katika kukuza uchumi wa nchi huku akisisitiza kuwa kutokana na kuwa alama hiyo ndio njia pekee ya kirahisi inayoweza kuzitambulisha bidhaa zinazotengenezwa nchini kimataifa.

Aidha, amesema kuwa kukosekana kwa alama hizo kwenye bidhaa za hapa nchini kunarudisha nyuma maendeleo ya wakulima na wazalishaji wengine wakubwa hata kwenye soko la kimataifa na la ndani bidhaa zinashushwa thamani halisi.

Pia ameagiza wizara zinazohusika moja kwa moja na wafanyabiashara ambazo ni Kilimo, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mambo ya Ndani ya Nchi, Viwanda na Biashara, Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) (Tamisemi) kukutana na Kampuni ya GSI.

Amesema, mawaziri, makatibu wakuu na viongozi wengine wakuu kwenye wizara hizo wanapaswa kuelimishwa kwa undani zaidi kuhusu faida ya matumizi ya alama hizo ili nao wawasaidie wadau wa shughuli za wizara zao.

Dkt. Bashiru awafunda CCM, 'Uhuni hautakiwi kwenye siasa'
Serikali yaingilia kati mgogoro wa ardhi kati ya Kambi ya Jeshi na Wananchi