Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka wazi kuwa suala la kutangaza nyongeza za mishahara kwa watumishi wa umma hadharani husababisha athari kwa jamii nzima na kwa wale ambao siyo watumishi.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa bungeni jijini Dodoma kwenye kipindi cha maswali na majibu kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbunge Suzani Lyimo aliyehoji ni kwa nini serikali ya awamu ya tano inakiuka sheria ya utumishi wa umma ya kutoa nyongeza kwa watumishi wake.

Majaliwa amesema kuwa siyo kwamba serikali haikusudii kuongeza mshahara kwa watumishi wake, lakini kutumia siku kama Mei 1 kutangaza nyongeza za mishahara husababisha athari kwa wananchi wote kwani vitu vinaweza kupanda bei na kusababisha usumbufu kwa watu wengine wasiopokea mishahara.

“Suala la mshahara ni siri ya mtu. Siyo lazima litangazwe hadharani. Ndiyo maana hata tunapolipa madeni hatutangazi lakini wanaodai wanaona kwenye mishahara yao kwamba malipo yanaingia. Lengo la serikali ni kupunguza na gharama za maisha,”amesema Majaliwa

Tuzo za Mo Dewji kuchochea ushindani Simba SC
Ramos atakiwa kulipa fidia ya £874m kwa Mohamed Salah