Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kuhakikisha viongozi wa Halmashauri za Wilaya zilizokuwa na makao makuu mijini na kutakiwa kuhamia katika maeneo yao kuhamia mara moja katika maeneo yao ya kazi.

Agizo hilo la Waziri Mkuu linafuatia swali la Mbunge wa Geita vijijini Joseph Kasheku Msukuma wakati wa kipindi cha maswali na majibu kwa Waziri Mkuu, katika kikao cha tatu cha Mkutano wa Pili wa Bunge, jijini Dodoma.

Msukuma alihoji kuhusu utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la Oktoba 24, 2019 kutaka Halmashauri za vijijini zilizokuwa zinakaa mijini kurudi maeneo yao husika ndani ya siku 30 ili kuweza kutoa huduma kwa wananchi.

“Wamehamisha ofisi lakini makazi bado wanarudi kulala mjini, na inapelekea halmashauri mzigo wa kugharamikia mafuta kila siku kurudisha watumishi kwenda kulala mjini, je, ni nini kauli ya serikali kwenye halmashaurui hizo ambazo zimerudi vijijini na watumishi wanarudishwa kulala mjini,? amehoji Msukuma.

Waziri Mkuu amejibu swali hilo kwa kuagiza, ” Nataka niwaagize Wakuu wa Mikoa, Katibu Tawala wa Mkoa ambaye pia ni Mtendaji Mkuu kwenye Mkoa huo kwenye Halmashauri zenye mazingira hayo ambako watumishi wametakiwa kwenda kwenye makao mapya hawajaenda, waondoke mara moja”.

“Kipindi cha kuondoka kilishatamkwa na mheshimiwa Rais, hatuna sababu ya kuwapa muda tena, ni kuondoka mara moja baada ya tamko hili” amesisitiza Waziri Mkuu.

Aidha Waziri Mkuu ameipa siku mbili Wizara ya TAMISEMI kuhakikisha halmashauri hizo zinahamia kwenye makao mapya na kuagiza kupelekewa ofisini kwake taarifa za wasiotekeleza agizo hilo kufikia Jumamosi Februari 6 saa 4 asubuhi.

Mtihani wa kwanza kwa Didier Gomez Da Rossa
Katibu Tawala Arusha afariki kwa ajali