Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya iliyotengewa sh. bilioni 2.72 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa akizungumza na wananchi wa Halmashauri za Rungwe na Busokelo katika mikutano ya hadhara aliyoifanya Kandete na Tandale katika wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.

Amesema kuwa mkakati huo unatekelezwa kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo, wananchi katika maeneo yote nchini watapata huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.

Aidha, amesema kuwa mkoa wa Mbeya umetengewa sh. bilioni 10.383  kwa ajili ya utekelezaji miradi mbalimbali ya maji, ambapo kati yake sh. bilioni 2.72 zinatarajiwa kutumika katika utekelezaji wa miradi ya maji kwenye wilaya ya Rungwe.

“Hatuwezi kuruhusu Taifa likaangamia kwa ajili ya watu wachache wanaoharibu mazingira kwa kuendesha shughuli za kibinadamu ndani ya vyanzo vya maji. Ni marufuku kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka katika vyanzo vya maji, atakayekutwa atachukuliwa hatua za kisheria.”amesema Majaliwa.

Hata hivyo, Majaliwa amewataka wananchi kuzingatia sheria ya Mazingira inayozuia kufanya shughuli za kibinadamu pamoja na kujenga kwenye maeneo yote ya vyanzo vya maji ndani ya mita 60 ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.

 

 

Mabawa aja na kampeni ''Magufuli Baki'' nchi nzima
Heri ya siku ya kuzaliwa komando 'Anold Schwarzenegger'