Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendeleza mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na haitavumilia aina yoyote ya ukatili wa kijinsia utakaofanywa na mtu yeyote hapa nchini.
 
Majaliwa amesema, Rais Samia Suluhu Hassan tayari amejipambanua na ameweka bayana msimamo wake dhidi ya ukatili wa kijinsia  na kusisitiza umuhimu wa kubadili fikra na kufanya harakati zote kwa ushirika kati ya wanaume na wanawake ili kujenga jamii yenye amani upendo na usawa.
 
“Lazima jamii yetu ijenge msukumo wa kuhakikisha kuwa kila mtu katika nafasi yake anapaza sauti na kuchukua hatua ya kuzuia na kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia hususani ukatili wa kingono kama vile rushwa ya ngono, ukatili baina ya wenza, ubakaji, mimba na ndoa za utotoni”.
 
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Novemba 25, 2021) katika Uzinduzi wa Siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.
 
Amesema vitendo vya ukatili vinatokea katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika ngazi ya Kaya, mahali pa kazi, maeneo ya biashara kama masoko lakini pia shuleni na mahali pengine katika jamii zetu. 
 
“Sote tunafahamu kwamba, licha ya sheria kali zilizopo bado vitendo vya ukatili vinaendelea kuwa ni changamoto kubwa na hivyo nguvu ya pamoja inahitajika katika kukemea vitendo hivyo”. 

Rais Samia: Riba za mikopo benki zitashuka zaidi
 
Majaliwa ametanabaisha kuwa Serikali itaendelea kutilia na kuunga mkono hatua zote stahiki katika kutokomeza ukatili wa kijinsia katika ngazi zote na itaongeza kasi ya kuhamasisha jamii kubadili fikra na mitazamo hasi inayochochea vitendo vya ukatili.
 
“Nitoe wito kwenu wananchi na wadau wa masuala ya jinsia kushirikiana na Serikali katika kuwekeza katika afua za kutokomeza ukatili wa kijinsia”.
 
Akizungumzia kampeni hiyo ya siku 16 za harakati dhidi ya Ukatili wa Kijinsia amesema Tanzania kwa kushirikiana na mataifa mengine itaendelea kuadhimisha kampeni hiyo ili kutokomeza kabisa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.
 
“Ninafahamu kuwa, huu ni mwaka wa 24 wa maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia hapa nchini. Nitumie fursa hii kuwahakishia kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuungana na mataifa mengine kupambana na ukatili wa kijinsia”.
 
Amesema katika kufanikisha Usawa wa Kijinsia kwa jamii ya watanzania Serikali imeendelea kuimarisha u jenzi wa vituo vya kijamii vya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto, Kuanzisha Madawati ya Jinsia na Watoto katika Vituo vya Polisi ambapo hadi sasa yapo madawati 420, Utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto pamoja na Mkakakati wa Taifa wa Kutokomeza Ukeketaji nchini.
 

Wataalamu wa mifugo wanaokiuka taratibu kuwajibishwa
Rais Samia: Riba za mikopo benki zitashuka zaidi