Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza kufukuzwa kazi na kufikishwa mahakamani kwa watumishi wote wa sekta ya afya watakaobainika kula fedha zinazochangwa na wananchi kwa ajili ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

Ameyasema hayo katika ziara yake Mkoani Rukwa na kumuagiza mkuu wa mkoa huo, Zelothe Stephen pamoja na Mganga Mkuu wa mkoa huo, Dk. John Gurisha kusimamia na kulinda fedha  za CHF zinazochangwa na wananchi  na kuhakikisha zinatumika kama zilivyokusudiwa.

Mh.Majaliwa ametoa agizo hilo leo  wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye jimbo la Kwela, Tarafa ya Mtowisa wilayani Sumbawanga.

“Kitendo cha kula fedha zinazochangwa na wananchi kwa lengo la kupata huduma za afya kinawafanya wakatetamaa ya kuendelea kuchangia mfuko huo. Kama wako watumishi wenye tabia hizo waache mara moja,” alisema.

Mbali na agizo hilo kwa uongozi wa mkoa wa Rukwa, pia Waziri Mkuu amewataka wananchi kujiunga na CHF kwa sababu mfuko huo utawawezesha  kupata huduma za matibabu bure wao na familia zao katika kipindi cha mwaka mzima.

 Waziri Mkuu  pia amesema barabara ya kutoka Ntendo hadi Muze ye urefu wa kilometa 85  itajengwa kwa kiwango cha lami ili iweze kupitika kwa urahisi na kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa wakati.

“Mimi nilidhani mlima wa Kitonga ndio mkali kuliko yote na eneo la Sekenke ndio linatisha zaidi!. Kumbe barabara ya kuja huku Mtowisa ndiyo inatisha zaidi kuliko zote. Lazima tuweke lami ili iendelee kupitika kwa urahisi zaidi,” amesema.

Akizungumzia ombi lililotolewa na mbunge wa jimbo la Kwela, Ignas Malocha la kutaka tarafa hiyo ya Mtowisa kuwa wilaya au halmashauri, Waziri Mkuu amesema analichukua na kwenda kulifanyia tathmini na majibu atayapata kupitia uongozi wa mkoa.

Mh. Malocha alisema jimbo la Kwela linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya miundombinu ya barabara hali inayosababisha wananchi kushindwa kusafirisha mazao yao kwa urahisi.

Hata hivyo Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Rukwa, Mhandisi Masuka Mkina ameelezea mkakati wa kuboresha miundombinu ya barabara mkoani hapo ikiwemo ya kutoka Ntendo hadi Muze wilayani iliyopo wilayani Sumbawanga

Kesi Ya Tundu Lisu Yapigwa Kalenda
Majaliwa;Atakayevamia Misitu Faini millioni 70, Au Jela Miaka Saba