Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha limewaua watu watatu wanaosadikika kuwa ni majambazi, baada ya majibizano ya risasi katika eneo la Fire jijini humo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa watu hao walibainika baada ya kutajwa na mwenzao Athumani Kassim aliyetiwa mbaroni na kukutwa na bunduki eneo la Engosheraton.

Kamanda Sabas alieleza kuwa majibizano ya risasi kati ya polisi na watu hao yalianza ghafla baada ya mtuhumiwa aliyekuwa akiwaelekeza kuwapa ishara watu hao, lakini mbinu za polisi ziliwezesha kuwapiga risasi na kuwajeruhi vibaya watu hao.

“Saa 5 usiku, askari wetu wakiwa wameambatana na Kassim, walipofika jirani kabisa na nyumba hiyo eneo la Fire, alitoa ishara na wenzake wakaanza kuwashambulia polisi kwa risasi,” alisema.

Alisema kuwa katika purukushani za kupigana risasi, walimpiga risasi mwenzao na wao walifariki wakati wakikimbizwa hospitalini.

Alisema kuwa baada ya kuwapekuwa waliwakuta na silaha mbalimbali pamoja na ujumbe wa vitisho kwa aliyekuwa Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleimani Kova.

“Nasaha kwa Kova, mzee andaa kamati ya mazishi ya vipolisi vyako tukiwamaliza tutakufikia wewe.”

Alisema kuwa mbali na silaha, walikutwa na vitu vingine ikiwa ni pamoja na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vazi la karate, kofia za kuficha uso na pikipiki yenye namba bandia.

 

 

 

 

 

Kuziona Twiga, Zimbabwe Elfu 2000/=
January Makamba aikosoa Serikali ya JK