Tanzania imesema janga la Uviko-19 limetoa mafundisho kuu ikiwemo jinsi gani ya kushughulikia majanga yajayo ya kiafya, sambamba na kujenga uwezo wa kitaifa na kikanda wa kuzalisha dawa, vifaa vya matibabu na chanjo dhidi ya magonjwa.

Hayo yamebainishwa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amesema wakati akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA77 jijini New York, Marekani.

Amesema, “Suala la Afrika kuwa limeenguliwa kwenye upataji wa chanjo, lilipatia msisitizo umuhimu nchi za Afrika kushirikiana kuzalisha na kukuza majawabu ya kiasili kupitia tafiti za pamoja na kisayansi na kitabibu.”

Dkt. Mpango ameongeza kuwa, janga la Uviko-19 limeibua umuhimu wa kuwekeza zaidi kwenye elimu ya afya ya umma, hususan elimu yak inga kwa kujenga uwezo wa mwili wa mtu kujikinga kwa kufanya mazoezi ya mwili, lishe bora na mifumo ya maisha.

Aidha, amekiri kuwa ingawa usaidizi wa kimataifa kwa Afrika katika kukabili kusambaa kwa Uviko-19 kwa kupatia vifaa vya uchunguzi, dawa, fedha na chanjo ulichelewa, licha ya kuwa na umuhimu katika kushinda vita dhidi ya janga hilo.

“Tanzania inapenda kushukuru wadau wote wa maendeleo ambao wamekuwa wanashirikiana nasi katika kukabili janga na kuweka nchi katika njia chanya ya kujikwamua kutoka janga la COVID-19 na bado inaendelea na kampeni ya chanjo na hadi tarehe 11 mwezi huu wa Septemba asilimia 60.56 ya watu wanaopaswa kupatiwa chanjo, walishachanjwa.

EAC yazungumzia mchakato wa amani DRC
Licha ya vikwazo tumedhibiti Uviko-19: Rais