Mtayarishaji mkongwe wa muziki nchini, P-Funk Majani ameona dalili za kuongezeka kwa ubora wa muziki wa Tanzania baada ya kushuhudia vifaa vya muziki vilifyofungwa katika studio mpya za kimataifa za ‘Wanene Entertainment’, hali iliyopelekea kuziona nyimbo hizo kwenye chart kubwa zaidi za muziki duniani za ‘Billboards’.

Akizungumza jana usiku kwenye uzinduzi wa studio hizo, Majani alisema kuwa muziki wa Tanzania ulikuwa na changamoto ya ubora wa sauti wa kiwango cha kimataifa, changamoto ambayo ameona itatatuliwa kupitia studio hizo.

“Kwa ufupi, kama tutatumia nafasi kama hizi na kuweza kutumia facilities hizi, nadhani hii game inaweza ika-elevate upande wa sound quality (ubora wa sauti) na tunaweza tukapata kitu ambacho kinaweza kikaa kwenye kiwango cha kimataifa na kinachoweza kushindana kwenye charti za billboards,” Majani aliuambia mtandao wa Bongo5.

Alisema kuwa uwekezaji uliofanywa na wamiliki wa studio hizo ni mkubwa sana kwani hata spika moja tu ina gharimu $6,000 (zaidi ya shilingi milioni 12 za Kitanzania).

Studio hizo zilizinduliwa rasmi jana usiku na kuwakaribisha wadau wa muziki kuweza kufanyiwa mastering yenye kiwango cha kimataifa.

Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo.

Mahafali Chuo Kikuu Muhimbili yasitishwa, Wanafunzi walimualika Lowassa
Mh. Possi Awataka Vijana Kuhakikisha Wanatumia Elimu Zao Kujiajiri