Majirani wanaoishi na Dk. Louis Shaka aliyevuruga mnada wa uuzaji wa majumba ya kifahari ya Lugumi wamemtaja kama mtu mwenye roho ya kipekee.

Mmoja wa majirani hao aliyejitambulisha kwa jina la mama Lucky, amesema kuwa kwa miezi minne aliyoishi na Dk. Shaka kama mpangaji mwenzake eneo la Tabata Mawenzi jijini Dar es Salaam, amemshuhudia kama mtu mwenye roho nzuri na ya kipekee ingawa hakuwa na fedha.

Amesema kuwa Dk. Shaka ambaye yeye alikuwa anamuita ‘Babu’, alikuwa anakaa ndani hata wiki nzima na mara kadhaa alikuwa akimpelekea chakula kwani hakuwahi kumuona akinunua wala kupika chakula zaidi ya kunywa maji ya bomba.

“Alikuwa anakaa ndani hata wiki nzima, mnaweza msijue kama yumo ndani hadi mnaposikia mtu anakohoa kwa mbali. Ndio unajua Babu yuko ndani angalau unampelekea chakula,” Aliiambia Ayo TV.

Ameeleza kuwa Dk. Shaka alidhoofu kutokana na kutokula chakula kwa muda mrefu na kunywa maji ya bomba pekee.

Alisema Dk. Shaka aliyekuwa anaishi chumba kimoja ambacho pia kilikuwa kama stoo, aliishi peke yake bila kuwa na mke au ndugu yeyote kumtembelea.

“Niliwahi kumuuliza, ‘Babu kwanini wewe hauna mke au mtoto, ina maana wewe kipindi cha ujana wako haukuwahi hata kuwa na mke?’ Akaniambia, ‘ni stori ndefu, haya maisha yana mambo mengi sana’. Basi nikanyamaza,” jirani alieleza.

Alisema kuwa hakuamini kusikia Dk. Shaka yuko kwenye vyombo vya habari akitaka kununua majumba ya Lugumi yenye thamani ya mabilioni ya fedha.

Dk. Shaka anashikiliwa na jeshi la polisi kwa utapeli na kuvuruga mnada wa majumba matatu ya Lugumi, ambapo aliweka kiwango kikubwa cha fedha na kuwashinda wateja wengine lakini hakuwa na fedha ya kutanguliza ambayo ni asilimia 25.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema kuwa Dk. Shaka anaendelea kuhojiwa.

Switzerland, Croatia zafuzu kombe la dunia
Ndege yakwamishwa hotuba ya Nyalandu Mtwara