Taarifa za kuwepo uhasimu kati ya Diamond na Ali Kiba, mimi binafsi nilikuwa sizikubali na nilikuwa nauchukulia kama ni uzushi unaopikwa na timu za mitandao ya kijamii ambazo wote waliwahi kusikika wakizikana na kuzituhumu kwa kutaka kuwagombanisha.

Nilikuwa nawachukulia kama mafahari wawili wanaotamba zizini bila kugusana, hadi Oktoba 9 mwaka huu, nilipothibitisha kuwa kweli wawili hao ni mahasimu ambao sio tu kwamba hawapiki chungu kimoja lakini pia wanaamini wanaweza kuwa wanashikana miguu katika mbio za biashara ya muziki.

Uthibitisho wangu juu ya hili unatokana na kile alichokisema Ali Kiba baada ya kuzimiwa kikuza sauti chake (microphone) kwenye tamasha kubwa lililomhusisha Chris Brown Oktoba 8 mwaka huu, Jijini Mombasa nchini Kenya.

Punde baada ya tukio hilo, Ali Kiba aliangaza kuona nani mbaya wake, na mwisho akataja hadharani kuwa anahisi meneja wa Diamond, Salam anaweza kuwa sababu ya yeye kuzimiwa mic kwakuwa alikuwa nyuma ya jukwaa wakati anaimba, kitu ambacho kilinifungua macho kuhusu uwepo wa uhasimu huo.

Hata hivyo, kama mtu mwenye jicho la ziada, huangalia kila kitu kwa jicho la faida zaidi na kuzikimbia hasara mithili ya mchaga aliyepewa mtaji wa chang’aa huku akiwaza kupata faida kama Bakhresa. Yaani hata kama kuna kitu kibaya, unatafuta namna ya kibaya hicho kuzaa kizuri kama haiwezekani kukibadili.

Kwakuwa sitaki kuzungumzia hasara kubwa wanayoipata hasa wanapokutana kwenye majukwaa ya kimataifa kama MTV MAMAs ambapo uhasimu wao unaweza kuwa ulichangia kuwapa nafasi washindani wao wa nje kuwashinda kirahisi, naamini kupitia uhasimu huo wanaweza kujiimarisha kwa kujifunza zaidi kutoka kwa kila mmoja wao kuliko kujifungia na kile walichonacho.

Kwa ufupi, Ali Kiba ana kitu muhimu cha kujifunza kwa Diamond Platinumz kwa sababu uimara wa Diamond unatokana na hicho ambacho kwake naweza kusema ndio udhaifu unaompunguzia kasi ya kukua. Vivyo hivyo, Ali Kiba ana kitu kikubwa sana ambacho Diamond anapaswa kujifunza kwa nguvu zote kutoka kwake. Hii ni kwa sababu  hicho ndicho udhaifu unaomtesa (Diamond) na kumpunguzia alama muhimu kwenye anga za kimataifa.

Nimekubali kuwa wawili hao wanauhasama, lakini nawashauri sana wasikimbiane bali mwenye akili zaidi aangalie uimara wa mwenzake na ajifunze kuufikia ili ampiku kirahisi.

Nakumbuka kuna falsafa moja nzuri ya kumshinda hasimu wako inasema kwa lugha ya kigeni, “keep your friends close, and your enemies closer”. Kwa tafsiri isiyo rasmi, “waweke rafiki zako karibu, na maadui zako karibu zaidi.” Hii ina maana kuwa una kitu cha kujifunza kwa adui yako. Kujifunza kwa hasimu wako sio ujuha.

Kwa mtazamo wangu, Ali Kiba ni mwanamuziki mwenye kipaji cha aina yake lakini ana mapungufu makubwa ya mbinu za kibiashara, wakati Diamond ambaye naweza kusema ana kipaji cha aina yake lakini kimuziki bado ni mdogo wake Ali Kiba anazijua mbinu za biashara.

Ali Kiba na timu yake, wanapaswa kujifunza sio tu mbinu bali kuwa na uharaka wa kusaka ’connection’ kwa nguvu zote kila wanapopata fursa. Wanapaswa kufahamu kuwa kiini cha mafanikio ya biashara yoyote duniani baada ya kuanza kushamiri ni ’connection’. Kama utafanya biashara ya umimi na kujifungia utabaki na wateja walewale na mwisho itadumaa huku ukiamini inakuwa kwa sababu macho yako yameishia ulipo. Unaweza kuchukua hii ukaiweka kwenye biashara ya muziki.

Kwa hili, Diamond ameonekana kumzidi Ali Kiba. Kila sehemu ambayo Diamond amekanyaga na akapita msanii mkubwa lazima ainase connection na baada ya siku kadhaa utasikia tu kuna kitu kinakuja kati yao na ziada.

neyo-na-diamond

Mfano mzuri ni jinsi alivyomkamata Davido kwenye Fiesta, alivyoweza kumteka Ne-Yo ambaye alikuwa Nairobi kwenye Coke Studio ambayo hata Ali Kiba pia alikuwepo. Lakini baada ya show, Mondi alifanikisha kufanya collabo yake na mkali huyo wa ‘so sick’. Vilevile alivyotua BET alitoka na connection yenye matunda n.k.

ali-kiba-na-neyo

Juzi, wawili hao walikuwa MTV MAMAs, baada ya siku moja, tunaona Diamond na Mohombi wametangaza uwepo wa collabo yao. Ingawa mwezi mmoja uliopita, Diamond alisema Mohombi na Alaine ni kati ya wasanii wanaosaka kufanya naye collabo. Hii inaonesha jinsi wasanii wakubwa wanajua umuhimu wa ‘connection’. Yaani Mohombi ambaye hakuwa kwenye orodha ya wanaoimba alivyoamua kuhudhuria MTV MAMA kupata connection za Afrika.

Rapper wa Malawi, Tay Grin naye alisafiri hadi Afrika Kusini kwa lengo la kupata baraka ya collabo kati yake na Diamond  na walikamilisha mpango wao rasmi usiku huo wa tuzo.

Diamond akiwa na Tay Grin mwenye fulana nyeusi, msanii wa Sweden mwenye asili ya DRC, Mohombi na wengine

Diamond akiwa na Tay Grin mwenye fulana nyeusi, msanii wa Sweden mwenye asili ya DRC, Mohombi na wengine

Kilichonishangaza, Ali Kiba alipofanya mahojiano na mtangazaji wa Times FM, Lil Ommy akiwa kwenye red carpet, alisema kuwa kutafuta collabo sio focus yake. “Hiyo sio focus yangu, focus yangu ni kufanya muziki mzuri,”alisema Ali Kiba.

Kauli hiyo ya Ali Kiba haikuniingia akilini kabisa kwa sababu hata kilichompa nafasi ya kuwania tuzo hizo mwaka huu ni collabo (Wimbo wa kushirikishwa kati yake na Sauti Sol – Unconditionally Bae), iweje collabo sio focus yake na aangalie kufanya muziki mzuri tu!? Kwani collabo sio muziki mzuri?

Tukio la MTV awards limezaa collabo kubwa kati ya Diamond na Mohombi, wapo wasanii wengi wakubwa Afrika ambao walienda kwenye tuzo hizo kwa lengo tu la kupata connection na wasanii wengine waliofika pale.

Collabo na wasanii wakubwa wa eneo fulani linakuongezea soko katika eneo hilo ambalo wewe usingeweza kufika kirahisi. Hivyo, mnakuwa mnabadilishana masoko na kuongeza wigo wa kibiashara.

Najua timu ya Ali Kiba ina njia yake nzuri ya kumsapoti msanii wake, lakini inaweza kujifunza pia kwa timu ya Diamond, sio vibaya kama nilivyosema. Salam (meneja wa Diamond) aliporushiwa lawama na Ali Kiba aliyehoji kwanini alikuwa nyuma ya jukwaa la show ya Chris Brown wakati Kiba akiimba, alijibu vizuri sana. “Mimi ni meneja wa msanii mkubwa, nilikuwa pale kujifunza na kupata connection na wasanii waliofika pale,” Salam anakaririwa.

Kumbe haya matunda ya collabo kubwa za Diamond haziji hivihivi, wanasaka connection kwa nguvu zote. Ndio maana sikushtuka sana nilivyoskia Diamond ana mradi unaokuja kati yake na Usher Rymond baada ya Ne-Yo. Of-course, kinaweza kuwa sio kitu kigeni kwa Ali Kiba ambaye alishafanya kazi na Mfalme wa RnB, R-Kelly.

Tunasikia collabo nyingi kubwa zinakuja za Ali Kiba, lakini sio sababu ya kujifungia connection ili kuongeza kasi ya ukuaji wa biashara yake ya muziki.

Nirudi kwa Kile nilichosema Diamond anapaswa kutulia na kujifunza kwa kaka yake Ali Kiba

Najua Diamond alianza muziki kwa kufuata nyayo za Kiba ingawa kwa wafutiliaji tunajua alikuwa amepania kukaa kwenye nafasi yake tangu siku ya kwanza.

Lakini Diamond hupaswi kuvimba ukadhani unamzidi Ali, bado yuko mbali kimuziki zaidi yako ingawa kibiashara unamzidi mbali. Hapo nieleweke kama nilivyoandika.

Imefikia wakati ambao Diamond anapaswa kuanza kufanya muziki wa ‘Live’ kama Ali Kiba. Ukubwa wake sasa unapaswa kuongea kitu zaidi jukwaani. Hakuna asiyejua kuwa Diamond anajua kutumbuiza (dope performer), lakini anapungukiwa alama muhimu sana za kufanya muziki wa ‘live’. Hizi playback zina mipaka yake.

Kama umewahi kushuhudia show ya Ali Kiba akiimba na bendi lazima utakubaliana na mimi kuwa utamu wa muziki wa kuimba sio ‘playback’ na kucheza sana na wanenguaji lukuki, sauti ya Kiba unayoisikia ikitoka moja kwa moja itakufanya uamini kweli huyu ni msanii mwenye hadhi ya kimataifa.

Kwa utajiri alionao Diamond, ni rahisi kuamka na kununua vifaa vya bendi tena vya kisasa, iwe kwa mkopo ama fedha taslimu. Lakini pia, anapaswa kufanya mazoezi ya kutosha kuhakikisha angalau anaufikia uwezo wa kufanya ‘live show’ kwa saa mbili.


Diamond akifanikisha hilo na ukiongeza uwezo wake wa kupiga show kali jukwaani (dancing) ataanza kuushangaza ulimwengu na atawanyoosha zaidi. Natamani aanze hili kwenye hiyo tour ya Ne-Yo aliyopewa shavu. Atawakalisha kwekweli mtoto wa Tandale.

Ingawa hata ukiimba kwa kufuatisha CD (playback) bado mashabiki watashangilia sana, lakini kuna jicho la ukubwa wa muziki wako litakumulika kivingine.

Akishindwa kuiga hilo kwa kaka yake Ali Kiba, basi amuangalie mshindi wa tuzo ya MTV MAMA, Wizkid ambaye hata alipotua Mwanza kwa ajili ya Fiesta, aliweka sharti la kuimba na ‘live band’ na waandaaji wakafika bei anayotaka.

Yote kwa yote, Ali Kiba na Diamond, mkijifunza hayo kutoka kwa kila mmoja, hatuwalazimishi kupatana lakini tunawaona mkitoka nduki zaidi na kuwafunika akina Davido na Wizkid.

Iker Casillas Apingana Na Waliotoa Habari Zake
Picha: Majaliwa ahutubia kwenye kilele cha maadhimisho miaka 55 ya UDSM