Waswahili wa Pwani ya Afrika Mashariki husema, “hakuna mwiba unaoutisha mguu wa ‘Mfalme’ zaidi ya kile kilichomuweka madarakani au kinachomuongezea nguvu ya kuwa Mfalme”.

Huenda sentensi hii ikatumika kutujengea picha japo kwa mbali, ya Diane Shima Rwigara, mwanamke shupavu ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mfadhili mkuu wa kifedha wa chama tawala cha Rwanda cha ‘Rwandan Patriotic Front’.

Assinapol Rwigara, tajiri aliyetumia fedha nyingi kukifadhili chama hicho tawala kinachoongozwa na Rais Paul Kagame, aliwekeza pia katika elimu ya mwanaye akiamini huenda familia yake, akiwemo mwanaye Diane ingekuwa rafiki wa karibu zaidi wa Chama tawala, lakini mambo yalikuwa tofauti punde alipofariki.

Mbali na urithi wa mali na fedha, Rwigara alimuachia mwanaye Diane urithi wa elimu ya uhasibu aliyoipata katika chuo kimoja cha California nchini Marekani, na huenda hakufahamu kama alikuwa na damu machachari ya siasa na uthubutu wa kukitunishia misuli chama tawala alichowahi kukifadhili kupitia miradi yake.

Tajiri huyo alimsomesha Diane Shahada ya Uzamili ya Uhasibu katika Chuo Kikuu cha San Francisco State, hiyo ni baada ya kuhitimu na kufaulu Shahada ya Usimamizi wa Fedha katika Chuo Kikuu cha Sacramento State.

Msigano kati ya chama tawala cha Rwanda na familia ya Diane, ulianza baada ya familia hiyo kudai kuwa wanaamini kifo cha baba yake kilichotokana na ajali ya gari kilitengenezwa kwa misingi ya chuki za kisiasa. Familia hiyo ilishikilia msimamo wa imani hiyo, licha ya ripoti ya vyombo vya dola kuonesha wazi kuwa Mzee Rwigara alikufa baada ya gari yake ya kifahari aina ya Mercedes Benz kugongwa na roli la mizigo, Februari 4 mwaka 2015 katika eneo la Gacuriro jijini Kigali.

Ajali yake iliibua maswali mengi na kesi dhidi ya kifo chake ilivuta usikivu wa mataifa mbalimbali, na maswali mengi kutawala mitandao ya kijamii.

Lakini yote yalikuwa maswali ya watu waliokuwa na kiu na shaka kuhusu ajali hiyo. Vyombo vya usalama vinavyotumia utalaam wake vilitoa vielelezo vyake kufunga mjadala ikieleza kuwa alifariki wakati akiondolewa kwenye gari hilo kwa lengo la kumuokoa, lakini wengi walibaki na maswali ikiwa ni pamoja na familia ya marehemu.

Katika kile ambacho wengi wanaamini kuwa ni kujaribu kuchota maji ya Tsunami kwa koleo au beleshi kwa lugha sahihi ya Kiswahili, Mei 3 mwaka 2017 ambayo ni miaka miwili tu tangu kifo cha baba yake, Diane ambaye alikuwa ameanza kuvuma kama mwanaharakati na mtetezi wa haki za binadamu, alitangaza kuwania nafasi ya Urais kuchuana na Rais Paul Kagame.

Mwanamke huyo, akiwa na umri wa miaka 36 alianza kugeuka kuwa tishio la kutaka kuking’oa madarakani chama hicho tawala, na tangu siku hiyo Tsunami la matatizo ya kisheria, kijamii na vyombo vya dola lilianza kuikumba familia yake kwa ujumla.

Kwanza, siku chache baada ya kutangaza nia ya kugombea, zilivuja picha za utupu kwenye mitandao ya kijamii zikidaiwa kuwa ni za kwake. Hatua hiyo, ilitazamwa kama njia ya kutaka kumpotezea heshima kwa wananchi.

Julai 7 mwaka 2017, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilimuondoa katika kinyang’anyiro cha urais ikieleza kuwa amekutwa na hatia ya kugushi sahihi za wafadhili wake, kinyume cha sheria. Tume hiyo ilieleza kuwa Diane aliwasilisha sahihi 572 badala ya sahihi 600 zilizokuwa zinahitajika huku baadhi zikiwa zimegushiwa na kwamba nyingine ni za watu waliokufa.

Diane alipinga vikali tuhuma hizo, akieleza kuwa aliwasilisha sahihi 958, na kwamba aliongeza tena sahihi 120 baada ya baadhi ya sahihi kukataliwa na Tume hiyo.

Hata hivyo, malalamiko ya Diane yalikuwa kama kelele za chura dhidi ya Tume ambayo ilikuwa imeanza mchakato wa kunywa maji (kufanya uchaguzi mkuu). Wapinzani wengine wawili wa Rais Kagame walienguliwa kwa kukosa sifa, na mwisho Rais huyo anayesifika kwa kurejesha hali ya utulivu na maendeleo makubwa ya nchi hiyo alishinda uchaguzi mkuu kwa 98%, kupitia chama tawala cha Rwanda Patriotic Front.

Aidha, Tsunami iliendelea kuikumba familia ya Diane hata baada ya uchaguzi huo, ambapo Agosti 30 mwaka 2017, jeshi la polisi lilivamia nyumbani kwao kwa kile walichoeleza kuwa ni kufanya ukaguzi dhidi ya tuhuma za kugushi na ukwepaji kodi wa familia hiyo kupitia biashara zao. Saa chache baadaye, familia yake iliripoti kuwa mwanaharakati huyo alikuwa amepotea baada ya kuchukuliwa na watu wawili walioaminika kuwa ni askari jeshi waliokuwa na mavazi ya kiraia.

Baada ya kufanyika kampeni kubwa kupitia mitandao ya kijamii kutaka aachiwe huru, vyombo vya dola vilikiri kumkamata yeye, mama yake pamoja na watu wengine wanne na kuwafungulia mashtaka. Mwanasiasa huyo na wenzake walisota rumande kwa tuhuma za uchochezi, kugushi nyaraka na kukwepa kodi na walikuwa wanakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 22 jela.

Juni 2018, Mamlaka ya Mapato nchini humo ilipiga mnada mali za familia hiyo zilizokuwa sehemu ya biashara ya tumbaku kwa $2 milioni, kwa kile walichodai ni hatua ya kutaka kurejesha deni la malimbikizo ya kodi la $7 milioni wanalodaiwa.

Katika hatua zote hizo, Mashirika ya Kimataifa ikiwa ni pamoja na Amnesty International, waliendelea kukosoa vikali hatua hizo na kuitaka Mahakama ya Rwanda kuhakikisha kuwa haiendeshwi kwa msukumo wa kisiasa kuwaadhibu wakosoaji wa Serikali.

Hata hivyo, Rwanda ilijibu kwa kuvitaka vyombo hivyo kutoingilia mambo ya ndani hasa mchakato wa kimahakama na kuuacha mhimili huo wa haki ufanye kazi yake kwa uhuru.

Nguvu ya mitandao ya kijamii, ilibaki kuwa nguvu pekee ya kusaidia kupaza sauti kuwatoa gerezani Diane na Mama yake kwa kutumia hashtag #FreeDianeRwigara. Nchi iliyoongoza kwa kupaza sauti kupitia mtandao wa Twitter ni Kenya, nchi ambayo ina ‘jeshi kubwa la Twitter’ ambalo liliwahi kuitikisa hata Serikali ya Marekani. Anyways, tusihamie huko.

Oktoba 5, 2018, takribani mwaka mmoja baada ya kukaa rumande, Mahakama iliamuru Diane na mama yake, Adeline kuachiwa kwa dhamana, wakipewa masharti ya kutovuka mipaka ya jiji la Kigali bila kupata ruhusa ya Mahakama.

Lakini jana, Mahakama ilitoa amri ya kuachiwa huru kwa Diane, mama yake na watu wengine wanne ikieleza kuwa Serikali imeshindwa kuthibitisha bila kuacha shaka, mashtaka dhidi yao.

Diane, ameendelea kushikilia msimamo wake kama nguzo ya chuma isiyopindishwa na upepo wa Tsunami, kwani punde baada ya kuachiwa huru, alisisitiza kuwa anaendelea na safari yake ya siasa.

“Nimefurahishwa na uamuzi wa mahakama. Ninaendelea na safari yangu ya siasa kwani kuna mengi yanatakiwa kufanyika ndani ya nchi yetu,” alisema Diane.

Aliongeza kuwa anaamini uchumi wa nchi hiyo umeshikiliwa na watu wachache ambao ni vigogo wanaounga mkono chama tawala na sio wananchi kwa ujumla.

Wachambuzi wa siasa, wanaimulika Rwanda ya mwaka huu kama nchi iliyoamua kubadili upepo wa kisiasa na kujaribu kuruhusu Demokrasia ichukue nafasi. Miezi michache iliyopita, Serikali ya Kagame iliwaachia huru wafungwa 2,140 wakiwemo Kizito Mihigo na Victoire Ingabire ambao walikuwa wanashtakiwa kwa kupanga njama za kumuua Rais Kagame.

Diane anarejea uraiani akiwa na nguvu kubwa zaidi, akifahamika hata na jumuiya za Umoja wa Mataifa kama mpinzani wa Serikali ya Rwanda na mwanaharakati hasa baada ya kusafishwa na hukumu ya jana ya Mahakama.

Je, hatua hii itampa nguvu ya kuwa mwanamke wa chuma kuweza kukitikisha au hata kuking’oa madarakani chama tawala cha ‘Rwandan Patriotic Front’ kinachoongoza Serikali chini ya Rais Paul Kagame? Je, ataweza kupenya katikati ya Tsunami la changamoto za kisiasa dhidi ya chama ambacho kilikuwa rafiki wa baba yake mzazi?

Diane ambaye sasa ana umri wa miaka 37, mtoto wa familia ya Watutsi anataka kutimiza ndoto yake ya kuwa Rais wa kwanza mwanamke nchini Rwanda, lakini anayo safari yenye changamoto nyingi za kisiasa.

Tuendelee kuitazama ‘Rwanda Mpya’, hasa baada ya Rais Kagame kuonesha anafungua milango kwa wapinzani wake kufanya siasa kuanzia mwaka huu, akiwaachia huru hata waliokuwa wanatuhumiwa kupanga mauaji dhidi yake. Nchi hii sasa inatajwa kuwa na mazingira bora yanayowavutia zaidi wawekezaji.

Lowassa azifungukia pingu zake Chadema
Video: Membe atua usiku kikachero, Lowasa afunguka hatima yake Chadema