Na Hassan Rajabu

Wakati Dunia ikitazama machafuko na kashfa mbalimbali za kisiasa zinazotokea katika Nchi kadhaa katika Dunia hii zikiwemo Brazil , Syria ,Israel na Palestina. Leo tujikite katika Soka ndani ya Brazil ambayo haijatulia kisiasa huku ikikutana na mechi muhimu katika Soka.

Tutazungumzia kuhusu Brazil ya Dilma roussef, Brazil ambayo imekumbwa na kashfa ya rushwa hivi karibuni na Rais akituhumiwa kuhusika na kashfa hiyo.

Ngoja nianze na mfano huu, ni kama filamu ya kuigiza ambapo tajiri anafilisika, kisha mfanyakazi wake anakuwa bosi wake. Ni mfululizo wa matukio ya kawaida ya maisha, lakini ni fedheha kwa bosi kufilisika. Naweza kusema hicho ndicho kimeikumba Brazil ya kizazi hiki cha Dilma roussef  mwenye kashfa rukuki za rushwa .

Brazil ya sasa si kama ya zamani,  ile ambayo ilianza kwa kina Garincha, ikaja kwa Pelle, na kumalizikia kwa vizazi vya kina Romario, Rivaldo, Bebeto, Ronaldo de Lima na Ronaldinho ‘Gauncho’. Haya majina hata kuyataja unapata utamu fulani wa kumbukumbu nzuri za soka lililotukuka la Brazil.

Brazil

Brazil hii ilikuwa ni moto wa kuotea mbali kwa kadri vizazi vilivyokuwa vinakuja, walitoka watu wenye vipaji vya ajabu na hivyo kuipa umaarufu timu yao ya Taifa na kutwaa makombe makubwa kama Kombe la Dunia na Copa America.

Utakumbuka kuwa Brazil wamechukua Kombe la Dunia mara tano (mara nyingi zaidi kuliko taifa lolote duniani), huku wakiiweka kibindoni ndoo ya Copa America mara nane, nyuma ya Uruguay (15) na Argentina (14).

Brazil 2

Wakati michuano ya Copa America ikifikisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwake, huku ikiendelea kutimua vumbi katika  Nchi ya Marekani katika viwanja mbalimbali, kuna maajabu yaliyojitokeza katika michuano hiyo. Timu kubwa kama Brazil, Uruguay na Colombia zimeshindwa kujihakikishia nafasi ya kuendelea mbele katika michuano hiyo.

Brazil ya kizazi hiki haina maajabu tena, imekosa ubunifu,mbinu na morali wa kutafuta matokeo, imekuwa  si ya dhahabu tena wala si lulu tena, imekuwa ni timu ya maigizo.

Brazil hii imefilisika kisoka inashindwa hata na Peru kwenye michuano ya Copa America, Brazil hii inatolewa na Peru? Ama kweli mpira unadunda na Dunia inazunguka na hapa ndipo mfanyakazi anapomuajiri bosi wake.

Brazil  hii imebaki jina tu na wachezaji wengi wanalipwa pesa ndefu katika vilabu vyao, hivyo kujikuta wanakuwa ‘mabishoo’ wasio na ari ya kulitumikia taifa lao.

Wanakosa nuru ya soka katika miguu yao na badala yake wanabaki kuuza  sura zao, hawana tena njaa ya makombe kama vizazi vya Brazil iliyopita wamekosa morali na bashasha katika sura zao na mioyoni mwao  kama kina enzi za kina Ronaldo na Ronaldinho.

Mimi ni mmoja kati ya mashabiki wa filamu hii ya Soka ya Brazil lakini naumia macho kuona ilianza na utamu na shangwe lakini inakoelekea inazidi kunichosha, inanifanya nikose raha na kunyong’onyea. Siwezi kuacha kuifuatilia ingawa ukweli ni kwamba inaniumiza macho. Labda itarudi mahala pake baadae, ngoja niwe mvumilivu ..!

Brazil hii itakuwa mwenyeji wa michuano ya Olympic, sijui itakuaje? Maana ni maajabu yatakayotokea. Najiuliza tu kama imeshindwa kufanya vema katika michuano ya Copa America, itakuwaje kwenye michuano hiyo? Majibu yatapatikana… tusubiri maajabu. Tuendelee na filamu yetu.

Fellaini, Lukaku Watukanwa Hadharani, Kisa Mabao Ya Giaccherini, Pelle
Stand Utd Kufanya Uchaguzi Wa Viongozi Juni 26