Na Ghati:

Waliosema, “mzigo mzito mpe Mnyamwezi” ndio haohao waliokamilisha na “neno zito mpe Msukuma.” Vyote vitafika hata kwa mbinde!

Juma hili la Pasaka lilikuwa na mambo mengi na muda mchache. Wakati tunatafakari Simba alivyonywea mbele ya shamba la miwa la Kagera Sugar, huko bungeni jijini Dodoma Mbunge wa Geita vijijini, Joseph Kasheku maarufu kama ‘Msukuma’, alianzisha Ligi yake akitetea maslahi ya tasnia ya filamu nchini maarufu kama Bongo Movies kwa namna iliyozua sintofahamu.

Ni kama Msukuma alihamisha mpira wa ‘faulu’ akautenga kwenye eneo la penati na kubutua shuti kali, ‘liwalo na liwe ili mradi tupate goli la maana’. Nadhani aliona wenzake wanazunguka na mpira kulitafuta goli, wakati yeye analiona liko wazi.

Ni mkwaju huo alioufyatua wakati akichangia hoja ya Bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ya Mwaka 2019/2020 ndiyo iliyowaamsha wachezaji, waamuzi na mashabiki wa Bongo Movies.

Huku mtaani kumekuwa na sauti mchanganyiko zinazotokana na goli la Msukuma, wengine wanashangilia, wengine wanalilaani, wengine wanasema ‘inauma lakini bora kupata goli’; na wengine wamebaki wamepigwa butwaa tu mithili ya mtu anayeangalia filamu ya kininja yenye mapigo yasiyofikirika. Kipi ni kipi?

Msukuma aliamua kuwatetea kwa nguvu zote wasanii wa Bongo Movies, akaanika kile kinachozungumzwa mtaani na mitandaoni ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano. Alinena kwa sauti ya mamlaka, akasema anaweza kuwataja baadhi ya wahusika.

Mbunge huyo machachari alielezea kile anachoamini ndio uhalisia wa maisha ya wasanii wengi wa Bongo Movies, akimsihi Waziri wa wizara husika, Dkt. Harrison Mwakyembe kusaidia tasnia hiyo ili awakomboe kama alivyofanya kwa wasanii wa muziki.

Lakini sentensi zake zilipenya kwenye mishipa ya tasnia hiyo mithili ya ‘sumu’ inayoponya.

“Tasnia ya filamu iko hoi, sasa hivi wanategemea michango ya misiba wakusanye michango wapige cha juu; na kufungua madangulo pamoja na kuwa makuwadi kwa wanaume,” Msukuma alifunguka ndani ya Bunge Tukufu.

Mbunge huyo pia alitupa makombora kwa Bodi ya Filamu nchini kuwa ndio chanzo cha kuzorota kwa tasnia hiyo. Aliwakumbusha wabunge kuwa uchaguzi umekaribia na kwamba ni wasanii hao ndio watakaotumika tena kuwasaidia kuomba kura jukwaani.

Baada ya shuti hilo, Bodi ya Filamu ikaona amecheza rafu. Ikalaani mistari niliyoiandika hapo juu kutoka kwa Msukuma. Ikawataka wasanii kuilaani kwani inawadhalilisha na inawafanya waonekane kuwa hutegemea misiba ya wenzao ‘kupiga’ wajipatie kipato.

Sentensi hiyo pia iliwafanya watu wamuwaze Mwenyekiti wa zamani wa Bongo Movies, Steve Nyerere. Lakini kwa Steve aliipokea kama vile ‘bora limekuwa goli hata kama linauma’. Steve hakuungana na Bodi ya Filamu kulaani, aliamua aivumilie ‘sindano kali’ aliyoamini ndiyo inayoponya.

“Tuna watu wangapi ambao tumezunguka nao nchi nzima lakini hawajawahi kusema kama alivyosema Msukuma. Kwahiyo msema kweli ni mpenzi wa Mungu, awe ametupiga, awe ametuvua nguo lakini kwa faida ya wote mimi nadhani Msukuma anahitaji pongezi. Saa ya ukombozi ni sasa, twendeni mbele,” Steve Nyerere ameiambia Global TV huku akieleza kuwa asilimia 90 ya wasanii wa Bongo Movies wako hoi.

Niliyapima yote kama msanii, mwananchi na mdau kwa ujumla wa Bongo Movies, nikaona shoka lililoshushwa na Msukuma kwenye huu ‘mbuyu unaoumiza Bongo Movie’ limeingia kwelikweli. Lakini huenda likawa limeingia sehemu ambayo sio itakayouangusha mbuyu huu wa matatizo. Nikaamua kudadisi kidogo.

Kwa kuanzia tu, nilitaka kufahamu kiini cha kilio na hata ‘kupararaizi’ kwa Bongo Movies. Ukijua chanzo utajua tatizo na hata namna ya kulitatua. Nikaona niwapitie wadau wawili watatu.

Lakini kabla ya hayo nikakumbuka pia Msukuma aliliambia Bunge kuwa hii tabia ya kutafsiri tamthilia za Kigiriki na Kikorea kama ‘Sultan’, kuruhusu filamu za Kikorea kuingia bila kukaguliwa wakati za Bongo zinakaguliwa na waliovaa mini-skirt wanakataliwa ni sehemu ya chanzo cha soko la Bongo Movies kuzorota.

Ukweli ni kwamba hapo niliguna kidogo..! Nikaanza kuwaza huenda mheshimiwa Msukuma anampiga nyoka kwa bidii lakini hajampatia kumpiga kichwani.

Nikapitia mafaili yangu kidogo. Nikakutana na sauti ya Zamaradi Mketema, mmoja kati ya watayarishaji wa Bongo Movies ambaye aliifanya filamu ya ‘Kigodoro’ kuwa gumzo. Huyu ni mdau muhimu, alifanya kipindi cha Take One cha Clouds TV kwa muda mrefu, akiwahoji wasanii na kufanya nao vikao kwa upande mwingine kama mdau. Hivyo, kwa namna moja au nyingine anajua tunapokwama.

Nikamsikia akikiri kuwa Bongo Movies imeporomoka na sababu akaanza kuzianisha.

“Kwahiyo ukweli ni kwamba Bongo Movies imeporomoka kutokana na sababu nyingi sana. Lakini pia kutokuwa na wasambazaji ambao wanaeleweka. Zamani tulikuwa na Steps, tulikuwa Proin [Promotions]. Lakini sasa hivi mtu anafanya tu filamu lakini anabaki nayo tu ndani. Kwahiyo huenda kuna filamu mzuri ambazo watu wameshajiongeza kuzifanya lakini naziuza wapi?” Zamaradi alifunguka kwenye The Playlist.

Zamaradi anaamini tatizo sio stori nzuri tena wala kazi nzuri, tatizo sasa ni usambazaji wa kazi nzuri zinazotayarishwa.

Nikadadisi tena sasa kama kuna filamu nzuri zaidi ya awali, kwanini wasambazaji wamekimbia? Nafahamu kilichobadilika ni uwepo wa stika za TRA kwenye kila CD ya Bongo Movies na ukuaji wa teknolojia na mitandao ya kijamii. Kuhusu soko naamini linazidi kutanuka kuliko ilivyokuwa awali.

Lakini pia, tukumbushane tu kuwa kumekuwa na maendeleo makubwa hivi karibuni, filamu kadhaa za Bongo Movies zimepewa hadhi ya kuzinduliwa na kuoneshwa kwenye Movie Theaters kama ‘Cinema Century’ pale Mlimani na sehemu nyingine. Yaani baada ya ‘Black Panther’ unalipia kuangalia filamu ya ‘Mama’ ya Auntie Ezekiel. Hii haikuwepo kabisa enzi zile. Sasa kulikoni?

Pili, nikajiuliza, Je, tukizuia kutafsiri filamu za nje au hata kuzuia kuingiza filamu za nje ndio tutauza zaidi Bongo Movies? Nikaona hili nimuulize rafiki yangu Isaya. Jamaa anazijua Bongo Movies balaa… lakini ukimuuliza kuhusu zile za Kikorea atakutajia kama 50 kwa mpigo, na bado anazijua zile za ‘Action’ za Marekani. Ndiye aliyenipa kwa mara ya kwanza series ya ‘Prison Break’ na huyuhuyu ndiye aliyenishtua kuhusu ‘Siri za Familia’.

“Aisee, sidhani kama unapaswa kuzuia nyimbo za Chris Brown na Tyga zisichezwe Tanzania ili nyimbo za Bongo Fleva zipande thamani. Ukijifungia hivyo utajidanganya, dunia imekuwa kijiji na soko ni zaidi ya huria. Bongo Movies zinaweza kuuza Marekani… ona marehemu Kanumba alikuwa ameanza kuuza hadi Nigeria. Soko linahitaji filamu nyingi zaidi na bado hazitatosha, Bongo Movies wazidi kufanya kazi nzuri tu sio kuzuia kazi za wengine,” Isaya aliniandikia kwenye Whatsapp.

Nikamuuliza tena, “kwani tatizo unadhani ni kwa sababu Bodi ya Filamu inakagua sana filamu zetu hatupati zile za ‘umate-umate’?. Isaya bwana… akanijibu, “ulishawahi kuiona 12 Years A Slave? Mbona ni utumwa ndio mwingi hakuna vimini wala umate-umate huo, humo ndani Lupita Nyong’o amechakaa, lakini ilishinda Oscar [Academy Award] na ikatikisa dunia hadi Tanzania.”

Nikaendelea na udadisi… Nikampigia simu mmoja wa maafisa waandamizi wa Bodi ya Filamu, hakutaka nimtaje. Nilifahamiana naye wakati fulani nilienda ofisini kwao kudadisi mambo fulani. Nikamuuliza “mkuu umemsikia Mheshimiwa Msukuma? Mbona mnashambuliwa, nyie inaonekana mna mfumo mbovu mnafanya Bongo Movies inakufa.”

Akanijibu, “tatizo sio mfumo hata kama una changamoto ndogo ni kawaida, tatizo wasanii wa Bongo wengi hawataki kuingia kwenye mfumo waliowekewa, yaani mtu hataki kujisajili, hataki kuwasilisha CV yake, hataki filamu yake ikaguliwe ili ipewe daraja na kutangazwa, anapenda vikao lakini hahudhurii mafunzo tunayotoa, anajitenga na mfumo lakini anataka kula matunda ya mfumo; kisa ni staa!”

Wakati naendelea kumsikiliza kwenye hili nikaikumbuka kauli ya Steve Nyerere, alisema kuna wanaofanya mambo ya hovyo kukwepa mfumo, na sababu ni kuwa wanataka kujipatia kipato wakiamini ‘hawana namna’. Sijui alimaanisha pia yale aliyoyasema Msukuma!? Lakini mimi nilielewa kuwa ni kukwepa utaratibu wa kimfumo.

“Mimi sitaki kulaumu kwamba kuna watu wanafanya mambo ya hovyo-hovyo tu, hali ikisha kufika hata hayo mambo ya hovyo-hovyo kama yanakuingizia kipato unaona bora uende nayo,” Steve aliambia Global TV. Kama Steve ana maanisha kuwa wasanii wanapita kando ya mfumo kufanya ya hovyo ili tu wapate kitu, sasa hapa unamlaumu vipi Mama Joyce Fissoo, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu?

Yule Afisa wa Bodi ya Filamu aliendelea kusema wao ni wasimamizi wa Sheria inayotungwa Bungeni. Na wasanii ni wadau walioshiriki vikao vya kuipitisha sheria husika, lakini wanalalamikia Bodi kwa kusimamia sheria hiyo. Hapo nikaona pana jambo kiudadisi!

Afisa huyo akanipa mfano kuwa kuna wakati walikuja watayarishaji kutoka nje ya nchi wakitaka kufanya filamu Tanzania. Bodi ikawaambia hawawezi kuwapa kibali bila kuwapa nafasi wasanii wa Tanzania ikiwa ni pamoja na ‘crew’.

“Tuliwaambia ‘yaani hadi mtu wa kushiika Boom mic mlete kutoka nje! Wapo watu wengi Tanzania tutawapa wawasaidie..’,” alisema.

“Aisee! Walitushinda kitu kimoja tu, wakatuambia wanaomba Profile au CV ya hao wataalam wetu wa filamu ili wao wachague. Huwezi amini, hiyo ni changamoto kubwa, wasanii asilimia karibu 90 hawajawahi kuletea CV zao Bodi ya Filamu. Sisi tunawasaidiaje, tunawaomba hawataki… hata unavyotaka kupromoti kazi zao inakuwa kuna ugumu wanaousabanisha wao,” alinijibu.

Aliniambia kuhusu kukagua, hakuna filamu yoyote duniani ambayo iko kwenye mfumo ambayo haijakaguliwa na kupewa daraja na mamlaka husika. Huo ndio mfumo wa kimataifa, hivyo kukaguliwa ni lazima na sio chanzo cha kuua soko la filamu. Ila kila filamu ina daraja lake kulingana na walengwa na yaliyomo.

Nikabaki mimi mwenyewe, nikajiuliza kuhusu kutafsiri ‘Sultan’. Nikasema hili nalo linaweza kuwa chanzo cha kuua Bongo Movies. Nikajiuliza tena kwani wakati watu walikuwa hawahemi vizuri bila kuangalia ‘Siri ya Mtungi’ hakukuwa na tamthilia nzuri za Kikorea?

Nadhani hata bila kutafsiri zipo tamthili nyingi za nje ziliwahi kutikisa Tanzania. Nakumbuka ‘dada’ ambaye alikuwa hajui hata kidogo kiingereza lakini alikuwa shabiki mkubwa wa tamthilia za ‘Timeless na The Long Wait’ za Kifilipino, sijui alikuwa anaelewa nini. Lakini alikuwa anasikitika na anafurahi pia, hadi anakusimulia. Kweli sanaa ni ‘universal language’. Nikajiuliza, ‘Sultan’ inaweza kweli kuzuia Bongo Movies zisikiki? Nitamsikiliza tena Mheshimiwa.

Sasa mchawi wa Bongo Movies ni nani? Isije kuwa yale ya Bongo Fleva, walikuwa wanalalamika kila siku wanaibiwa… ooh wanaibiwa. Juzi, Master Jay, mtayarishaji mkongwe ametumbua jipu akieleza kuwa miaka zaidi ya 10 iliyopita kuna wasanii wa Bongo Fleva walikuwa wanalipwa ‘advance’ Shilingi Milioni 100 (Ndio ni Sh. 100,000,000) kwa albam moja. Master Jay anasema fedha hizo kiasi kikubwa zilikuwa zikiishia kwenye mitungi, pamba na mikasi. Kisha lawama zote ‘Mawingu FM’, ‘Wasambazaji’ na Basata.

Master Jay aaliiambia XXL ya Clouds Fm wiki hii ya Juma la Pasaka kuwa wasanii hao walikuwa hawaambiliki hawashauriki kuhusu matumizi ya mamilioni yao. Lakini miongoni mwao ni wale ambao walisikika kwenye ile mixtape (kandamseto) fulani wakishambulia kituo kikubwa cha redio na uongozi wake kuwa kinawanyonya, kinaua tasnia.

Kama aliyoyasema Master Jay ni ya kweli, huenda mmoja kati ya wachawi wa Bongo Movies ni wasanii wenyewe pia. Huenda wanaukimbia mfumo na kuishia kuutupia lawama badala ya kuu-fix.

Kabla sijamaliza, nikumbuke Mheshimiwa Msukuma alisema wasanii wa Bongo Fleva wao wanafanya shows wanapata pesa, ila wa Bongo Movie wanategemea filamu. Nikasema ni kweli kabisa asemayo mheshimiwa, lakini hawa wa Bongo Movies ya sasa ndio wengi wao ‘hawataki kufanya shows’. Nakumbuka enzi zile wasanii wa ule mchezo wa ‘Kidedea’ walikuwa wanazunguka nchi hii wakifanya matamasha na wanajaza nyomi.

Rafiki yangu anaitwa Alliwah, ni Mkenya aliyeshiriki sana matamasha ya maonesho na Mrisho Mpoto, anasema bado Kenya Sanaa ya maigizo jukwaani inalipa sana. Ni namna ya uwasilishaji na ubunifu tu.

Basi kwa tafakuri hii, wasanii wa Bongo Movies tuwe wakweli, tushirikiane kumsaka mchawi wetu. Msukuma ametusaidia kupaza sauti hata kwa kuhamisha mpira wa faulu na kuutenga eneo la penati, ‘lakini bora amefunga goli’. Sisi tunajua ukweli zaidi… tusiukimbie mfumo, tuishi ndani ya mfumo ili tuurekebishe kwa faida ya leo na kesho.

Nimalize kwa kumpa pongezi Dkt. Mwakyembe kwa kuitendea haki wizara yake, juhudi zake zinaonekana, nakumbuka mara ya mwisho nilikuwa mmoja kati ya waandaaji wa tukio la uzinduzi wa Kampuni ya Filamu na Muziki ya Starline Films iliyoko Mikocheni B, na Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe alikubali mwaliko wa kuwa mgeni rasmi, na alipotingwa alimtuma Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Mama Fissoo akasoma hotuba yake nzuri iliyotoa matumaini na ushauri kwa wasanii. Kweli anajali.

Dkt. Mwakyembe ametembelea makampuni mengi ya filamu akiongozana na Mama Fissoo, wanawatia moyo na kuwasikiliza, naamini tukishirikiana kwa pamoja kuurekebisha mfumo tutavuka hadi kufikia tuzo za Oscar.

Monalisa ametuonesha mfano wa kushinda tuzo ya Afrika bila kuwa na skendo. Kesho… Inshallah, tutamuona yeye au mwingine akikabidhiwa Oscar (Academy Award).

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe (watatu kushoto) akimkabidhi bendera msanii wa filamu nchini Yvonne Cherrie maarufu kama Monalisa kabla ya kwenda nchini Ghana (Aprili 2018) ambapo alishinda tuzo ya The African Prestigious Awards katika kipengele cha Msanii Bora wa Kike Afrika, wa pili kulia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa Bibi. Leah Kihimbi na wa kwanza kushoto ni Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Bibi. Joyce Fissoo.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Aprili 22, 2019
8,004 wafariki, 35,231 wajeruhiwa kwa ajali za bodaboda

Comments

comments