Na: Josefly Muhozi

Nimetumia muda ku-google ili nipate ‘maana ya neno imani’ bila kugusa vitabu vitakatifu. Kila maana ninayosoma kwenye mtandao naona ni nyepesi kuliko nachokifikiria, kinachosimuliwa na kinachotokea. Kabla sijaamua kuachana na Google, nikakumbuka, Mwalimu wangu Denis Mpagaze aliwahi kutuambia kwa lugha ya kigeni tukiwa darasani Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino, “google will make you stupid”! Hapo ni kama alitupiga kofi la uso, tukaona ‘maluelue’. Yeye alikuwa anasoma sana vitabu kwa nakala ngumu (hard copies).

Nikagoogle tena kujua kwanini alisema Google inaweza kutupumbaza!? Google nayo ikaleta nukuu ya mchekeshaji maarufu wa Uingereza John Marwood Cleese akisema, “kama wewe ni mpumbavu kweli, huwezi kujua kuwa wewe ni mpumbavu. Unapaswa kuwa mwelevu na mwenye akili za kutosha kugundua kuwa wewe ni mpumbavu.” Ebana eeh!

Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule aka Profesa Jay kupitia wimbo wake wa Bongo Dar es Salaam, yeye anaamini wenye imani potofu ni wale wanaoamini msemo wa Wahenga ‘aliyeko juu mgojee chini’, anasema, “mtangoja milele na mtakufa bila kelele, kama walivyokufa wafuasi wa Kibwetere.” Sasa huyu Kibwetere ni nani?

Joseph Kibweteere au ‘Kibwetere’ wa Uganda, alikuwa Mwalimu wa shule ya msingi. Lakini aliyejaribu siasa akashindwa kuwashawishi wananchi, akahamia kwenye dini akawapumbaza watu kwa kujiita ‘Nabii na Mtume’. Huko akateka mioyo ya wengi wenye shida akiwaahidi kuwapeleka peponi, lakini mwisho akawaua kwa kuwachoma moto akiwaaminisha kuwa mwisho wa dunia umefika. Aliwateketeza mamia kwa moto wa mafuta ya petrol, wakaonja adhabu ya jehanam waliyosimuliwa wakati wanaahidiwa kuingia ahera. Tukio hili baya kuwahi kutokea Afrika kwa imani iliyojaa udanganyifu, limeacha majonzi makubwa na kupewa jina la Mauaji ya Halaiki ya Kanungu (Kanungu Massacre).

Kibwetere yeye aliitumia Biblia hiyohiyo kupotosha, alisoma vifungu akavipindisha na vikawa kama vimenyooka. Unajua hata Shetani alitumia ‘Maandiko ya Mungu’ kumshawishi Yesu ajitupe kutoka mlimani. Lakini kwakuwa Yesu alikuwa na maarifa alipinga kwa maandiko hayohayo na akamshinda.

Biblia kupitia Methali 31 inasema, ‘mpe kileo aliye karibu na kupotea’ na divai aliye na uchungu nafsini mwake, anywe asahau umasikini wake. Kibweteere yeye akawapa masikini ujinga akijua wazi kuwa masikini na mwenye shida akilewa ujinga na kupumbazika lazima tu ataangamia. Alijua Maandiko ya Mwenyezi Mungu yanasema, “Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa.” Akawanywesha maji ya mchele akiwadanganya kuwa ni maziwa, wakavutiwa na rangi, wakayabugia kisha akawaangamiza.

Lengo lake lilikuwa nini hasa? Fuatilia Makala hii.

Mwanzoni mwa miaka ya 1980, Uganda ilikuwa ikipitia katika wakati mgumu sana wa kujitengeneza hasa baada ya kuondolewa kwa utawala katili wa Idi Amin aliyepigwa akachakaa na majeshi ya Mchonga, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Lakini pia gonjwa la Ukimwi pamoja na magonjwa mengine mazito yaliitikisa nchi hiyo, vilio vilitawala kila kona. Ufukara wa kutupwa ulizikumba kaya nyingi.

Wakati huohuo, ndani ya Kanisa Katoliki aliingia ‘Bundi mweusi’. Kanisa lilipata kashfa nyingi kubwa na nzito. Waumini walikuwa kama kondoo aliyesikia mlio wa baruti, wengi walikimbia hovyo bila kujua wanaelekea wapi. Wenye Subira walitulia kwanza wakatafakari kabla ya kuchukua hatua.

Katika purukushani hizo, aliibuka Joseph Kibweteere, huyu alikuwa msaka tonge haswa. Alikuwa msomi wa kati na mwenye taaluma ya ualimu wa shule ya msingi. Alikuwa akifundisha shule ya Kikatoliki.

Kama nilivyoanza kusema alikuwa msaka tonge, miaka ya 1980 alijaribu siasa. Huko akapigwa upper cut chembe ya kidevu, akakimbia. Siasa zina wenyewe bana! Alikusanya sarafu akawa na ukwasi wa utajiri kwa viwango vya wakati huo nchini Uganda. Kwakuwa alikuwa mwalimu katika shule ya Kikatoliki, alipenya na kuwa katika sehemu ya viongozi wa Parokia. Baada ya muda, akiwa na ndoto ya kuongoza tu watu iwe kwa siasa au kwa imani, akatoa mchango mkubwa katika ujenzi wa shule na kuukabidhi Kanisa Katoliki. Kisha akawa anatoa misaada mbalimbali kwa jamii. Akafanikiwa kuushawishi umma kuwa yeye ni mtu mwema. Akazidi kupenya kwenye nafasi za uongozi katika Kanisa Katoliki. Alivaa vizuri ngozi ya kondoo, ‘ikamfiti’ haswa. Hakuna aliyejua ni mbwa mwitu.

Taratibu… Kibwetere aliyatumia majaribu yaliyolikumba Kanisa Katoliki kama fursa, akaona kufa kufaana. Mwaka 1984, alianza kueleza kuwa amekuwa akimuona Bikira Maria anamtokea ndotoni na kumpa jumbe mbalimbali. Alianza kuwaaminisha watu taratibu, lakini hakuwa na nguvu ya kutosha.

Mwaka huo, alikutana na mwanamke mmoja mrembo aliyefahamika kama Credonia Mwerinde. Huyu aliwahi kuwa mwanamke maarufu kwa ukahaba na bingwa wa kutengeneza pombe ya kienyeji.

Lakini wakati huu Mwerinde alikuwa na familia yake wakijaribu kusambaza imani yao, alisema ameokoka baada ya kukutana uso kwa macho na Bikira Maria, Mama wa Yesu Kristo. Bi. Mwerinde alikuwa na baba yake mzazi wote walikuwa wanasambaza imani ya familia yao kuwa wamekuwa wakiona maono mengi ya kimiujiza na nguvu za kiroho.

Wawili hawa walipoungana wakaanzisha Vuguvugu la ‘Marejeo ya Amri Kumi za Mungu’ (Movement for the Restoration of the Ten Commandment). Baba yake Bi. Mwerinde ndiye aliyekuwa amepewa heshima ya kuongoza kundi. Lakini baada ya mzee huyu kufariki, Kibwetere akakabidhiwa rasmi uongozi wa vuguvugu hilo la kiroho, alipakwa mafuta rasmi kuwa ‘Mtume na Nabii’. Wakiwa tayari wameshavuna mamia ya waumini, Bi. Mwerinde akajitolea, akatoa sehemu ya ardhi ya familia yake katika eneo la Kanungu, kilometa 50 kutoka Mji wa Rukungiri, hapo wakajenga kanisa kubwa.

Mwaka 1992, Kibwetere aliachana na mkewe, sababu hazijulikani. Si unajua tena wakati huo wadaku hawakuwa na ‘kisemeo’ kama sasa hivi Instagram ilivyo. Akaendelea kuhubiri injili akiwa karibu zaidi na Bi. Mwerinde, Mtume mwenzake.

Inaelezwa kuwa Bi. Mwerinde ndiye aliyekuwa na nguvu zaidi na Kibwetere alikuwa amewekwa mstari wa mbele tu. Bi. Mwerinde ndiye aliyekuwa anatoa utabiri wa mengi zaidi na alitegemewa sana na wenzake. Eti baada ya kuwaua waumini wao, Bi. Mwerinde alipewa tuzo mwaka 2011, tuzo gani, endelea kufuatilia.

Imani waliyoipandikiza kwa waumini wao:

Gazeti la New Vision la Uganda, limemkariri mmoja kati ya wahubiri wa zamani wa Kanisa la Kibwetere, Martino Nuwagaba akisimulia kuwa walikuwa wanahubiri kwa mkazo kuhusu kushika Amri Kumi za Mungu na siku tatu za kiama.

Ndugu Nuwagaba alisimulia kuwa kuanzia siku ya Pasaka ya mwaka 1992, walianza kuhubiri kuwa katika siku hizo tatu za kiama, nyoka wakubwa mithili tairi la trekta na matofali makubwa ya sementi/saruji yatashuka kutoka Mbinguni kuwaangamiza wenye dhambi wote.

Walihubiri kuwa kutakuwa na giza nene kwa siku tatu, na kwamba eneo pekee litakalokuwa salama ni makambi ya Watakatifu ambayo yameandaliwa na Kibwetere na wenzake. Kwamba makambi yatakuwa salama kama mbingu. Walisema baada ya siku ya mwisho, waumini wao wote wataanza kuwasiliana moja kwa moja na Yesu Kristo.

Waliwaaminisha waumini wao kuwa itakapokamilika hiyo siku, kila mtu duniani ambaye hayuko kwenye kanisa lao au makambi yao ataangamia isipokuwa wafuasi wa Kanisa hilo. Waliwakumbusha habari ya Nuhu na Safina, wakawaambia hayo ndiyo maono ya siku ya mwisho, na kila mwenye sikio naasikie kuwa ili awe salama anapaswa kuondoka nyumbani kwake na kuingia kwenye makambi waliyoyaanzisha.

Inaelezwa kuwa kwenye hayo makambi waliweka kuta, wakaweka nyaya za umeme na ulinzi wa kutosha. Hakuna aliyeruhusiwa kuingia bila ruhusa yao. Waliwakusanya waumini wao humo wakawapa kazi na kusali wakisubiri siku ya kiama.

Ndani ya Makambi hayo na kanisani, walipiga marufuku watu kujamiiana (no sex), hakuna kufanya ngono wala tendo la ndoa hata kama umeoa na kuolewa. Hivyo, hakuna aliyeruhusiwa kupata ujauzito.

Waumini wao hawakuruhusiwa kwenda hospitalini au kusoma shule, au hata kusomesha watoto wao. Walienda mbali zaidi, wakapiga marufuku kuongea. Ni viongozi pekee ndio waliokuwa wanaruhusiwa kuongea, waumini waliongea kwa ishara tu. Walisema lengo ni kuhakikisha hawavunji amri kumi za Mungu hasa kwa kusema uongo. Kumbe walikuwa wanakata mawasiliano kati ya waumini.

Waliwapiga marufuku waumini wao kujichanganya na watu wasioamini, hata ndugu zao wa karibu. Walihakikisha hawapati nafasi ya kuchanganyikana na watu watakaowavuruga kwa kuwapa elimu tofauti na ya kwao.

Hapo Kibwetere ni kama alikuwa ajenti wa Shetani, alitumia maandiko matakatifu ya Biblia akayageuza atakavyo kwa faida yake. Akaenda kinyume na Maandiko Matakatifu ya Quran 9:122, ambayo inawataka ndugu kutoka katika makundi watoke wakajifunze vyema elimu ya dini kupata maarifa, na kisha watakaporejea wawaonye wenzao ili wapate kujihadhari.

Pia, Quran 39:9 inaeleza, “Je, watakuwa sawa wale wenye maarifa na wasio na maarifa? Hakika wale wanaoelewa ndio watu wenye akili.” Pia, Mtume Muhammad (SAW) amesema kutafuta maarifa ni wajibu wa kila Muislam.

Tuendelee na imani ya Kibwetere na wenzake! Inaelezwa kuwa walitengeneza ratiba ngumu iliyowafanya waumini wao wawe ‘bize sana kiasi kwamba hata kuwasiliana kati yao kwa ishara kama walivyoelekezwa ilikuwa ngumu. Walikuwa bize kuandaa makao yao ya milele.

Waliwataka waumini wao kuuza mali zao na kuwasilisha mapato yote Kanisani. Wakati mwingine walichoma hadharani mali za baadhi ya waumini wao wakieleza kuwa Bikira Maria amechukizwa na wamiliki wa mali hizo, hivyo wanazichoma na kuwaombea heri na msamaha.

Walihakikisha wanatengeneza mfumo unaowalazimu wafuasi wao kutegemea kanisa na kutokuwa na vitu vinavyowafanya warejee kwenye hali yao ya zamani. Waliwadhoofisha ili wasiwe na nguvu au wazo la kurejea walikotoka.

Inaelezwa kuwa, Kibwetere na viongozi wenzake walitoa misaada mingi kwa umma kuwafunga macho maafisa wa Serikali. Wao pia hawakuwa wanamiliki mali zinazoonekana moja kwa moja. Hawakuwa na usafiri wa aina yoyote, wao walikodi usafiri walipotaka kwenda mahala popote; na safari zao nyingi zilifanyika usiku. Hivyo, watu hawakujua sana mienendo yao.

Siku ya mwisho na waumini walivyoteketea kwa moto:

Kibwetere, Bi. Mwerinde na viongozi wenzake waliwatangazia wafuasi wao Mungu amewafunulia kuwa Desemba 31, 1999 – Januari 1, 2000 ndio utakuwa mwisho wa dunia. Walieleza kuwa baada yam waka huo, dunia itaanza mwaka mpya wa dunia mpya.

Hivyo, waliwataka waumini kujiandaa, kufunga na kuomba na kuhakikisha wanakuwa ndani ya kanisa, hasa kanisa kuu la Kanungu. Wakati huo inaelezwa kuwa walikuwa wamefanikiwa kuvuna waumini kati ya 1,000 na 5,000.

Hawakuwa wavivu hata kidogo, kwakuwa timu yao ilikuwa na wasomi wengi pia, waliandika machapisho mengi na kuyasambaza. Waliandika miongozo mingi ambayo imetumika pia kama ushahidi wa jinsi walivyowaaminisha waumini wao kuwa mwaka 2000 utakuwa mwisho wa dunia.

Ilipofika siku waliyoahidi, walihakikisha wanawakusanya waumini wao kwenye kanisa lao lililopo Kanungu. Kwa bahati, walifika mwaka 2000 na hakukuwa na mwisho wa dunia. Kibwetere aliwaambia waumini wakati wowote Kiama kitafika. Kwa haraka wakatoa utabiri mpya kuwa Machi 17, 2000 itakuwa ndio mwisho wa dunia. Mahesabu na maono yalikuwa yanawasilishwa na Bi. Mwerinde, yule aliyesema anawasiliana na Bikira Maria.

Wakati dunia ya wanasayansi wakiwa na hofu kuwa mwaka 2000 huenda program za kompyuta zingeleta shida kutokana na kubadilika kwa tarakimu (99), wakahisi huenda zitashindwa kusoma, ndiyo ile ‘Y2K’; Kibwetere yeye aliwajaza hofu waumini wake kuwa ni mwaka wa mwisho wa dunia.

Iliripotiwa kuwa, katika kipindi hicho Kibwetere na waumini wake walichinja Wanyama wengi na kuandaa tafrija kwa kununua vinywaji vingi vya ‘Coca-Cola’. Hali hiyo haikuwashtua wengi, lakini yalikuwa maandalizi ya sherehe kubwa kabla ya kifo.

Baada ya kuhakikisha waumini wanaendelea na ibada za maandalizi, taratibu Kibweteere, Bi. Mwerinde na wenzake wakaanza kuziba baadhi ya maeneo ya kanisa hilo, kama vile madirisha na vyote vinavyopitisha mwanga. Inaaminika kuwa lengo ilikuwa kutengeneza giza la siku tatu ambalo waliwaahidi watu wao kuwa litakuja kabla ya siku kamili ya kiama.

Machi 17, 2000 haitasahaulika kwenye kumbukumbu za Uganda! Awali, ripoti ilieleza kuwa watu 530 waliokuwa ndani ya kanisa lililoongozwa na Kibweteere waliteketea kwa moto. Lakini baadaye polisi walieleza kuwa ni watu 330. Hata hivyo, kumekuwa na ubishani kuhusu idadi hiyo, baada ya ripoti nyingine kueleza kuwa walikuwa takribani watu 800. Hata hivyo, ripoti isiyo na pingamizi inaonesha kuwa wote waliokuwa kanisani walimwagiwa mafuta ya petrol na hivyo waliteketea kabisa.

Ripoti zilieleza kuwa baada ya tukio hilo, miili mingine takribani 494 walipatikana siku kadhaa baadaye kwenye majengo ya kambi walikokuwa wametunzwa wafuasi wa Kibwetere. Ilidaiwa kuwa wengine walionekana kuwa waliuawa kwa vipigo, na wengine walikutwa wakiwa wamezikwa kwenye makaburi ya pamoja katika maeneo ya Rugazi, Bunyaruguru, Rushojwa na Buziga jijini Kampala.

Majirani wa wafuasi wa Kibweteere walieleza kuwa siku moja kabla ya tukio la kuunguzwa kwa moto, watu hao walipita katika baadhi ya maeneo wakiwaaga ndugu na majirani zao wakiwahamasisha pia kuungana nao.

Kitendawili au fumbo kuu lililosalia, ni kuhusu alipo Kibweteere. Ripoti zilikuwa na maelezo tofauti, wengine walisema alipoteza maisha ndani ya kanisa hilo, wengine walisema kuwa alitoroka na kukimbilia nchini Malawi. Waandishi wa habari, likiwemo gazeti la New Vision waliwakariri baadhi ya ndugu zake wakieleza kuwa Kibwetere alikuwa na ndoto ya kwenda Ulaya hivyo aliamua kutafuta fedha kwa kuuza mali za watu kwa jina la ‘imani’.

Ripoti zinaeleza kuwa Bi. Mwerinde, yeye alitoroka saa chache kabla ya kanisa kuteketezwa kwa moto. Yeye alizaliwa mwaka 1952 na akafanikiwa kuishi miaka 68. Bibi huyu anatajwa kuwa mmoja kati ya wanawake hatari zaidi duniani waliopanga mauaji ya halaiki kwa jina la ‘imani’.

Serikali ya Uganda haikulifumbia macho hili, ilichukua hatua haraka. Ikizingatiwa kuwa Kanisa la Kibwetere na wenzake lilikuwa limesajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Taasisi zisizo za Kiserikali Mwaka 1997. Desemba 2000, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uganda, Moses Ali alimteua Jaji Augustus Kania kuongeza Kamati ya kuchunguza tukio hilo la mauaji, lakini ripoti hiyo haikuwekwa hadharani, na Serikali ilitangaza kuwa inaendelea na uchunguzi zaidi.

Kibwetere alipotea kusikojulikana. Alipotea kimiujiza? Je, alikuwa miongoni mwa majivu yaliyokusanywa kutoka kanisani, au alikuwa miongoni mwa waliofunga mlango na kumwaga mafuta ya petrol kwenye jengo la kanisa na kuwasha kiberiti? Ni Mungu pekee ajuaye.

Lakini kumbe hata Shetani hutuzwa! Utashangaa. Septemba 2011, Bi. Mwerinde alitunukiwa tuzo iitwayo Ig Nobel Prize eti kwa jinsi alivyopanga na kushawishi kuhusu siku ya mwisho wa dunia; eti alitoa funzo kwa dunia kuwa makini wakati wa kufanya mahesabu ya nyakati. Lakini tuzo hii iliyoanzishwa mwaka 1991 ililenga katika kufanya kinyume cha ile tuzo ya heshima ya Nobel. Ig Nobel hii huwatuza watu ambao wamefanya mambo yasiyo ya kawaida, na mara nyingi hutolewa kama kejeli/ucheshi.

Ndugu yangu katika imani, tuamini na tutafute maarifa sahihi tusije kuangamia. Tusiishi kwa kusubiri kupewa kila kitokacho kwa mtu yeyote kwa jina la ‘mtumishi wa Mungu’. Tuwapandiye juu ili tusome na kuelewa.

Nakuacha na kauli fupi ya Mchungaji Anthony Lusekelo, maarufu kama Mzee wa Upako, anasema, “wewe unaamini nini? Baki na imani yako, lakini usivunje sheria za nchi.”

Video: Hatima ya Tundu Lissu kesho, Mkapa 'ajimwambafai
Niger: Magaidi 120 wauawa katika operesheni

Comments

comments