Alikuwa mtoto mwenye kipaji cha hali ya juu, ‘Messi anasubiri’. Mithili ya jogoo aliyepata nafasi ya  kutoka nje ya banda mapema, sauti yake iliposikika alfajiri, iliwashtua majirani ambao walinogewa na mvuto wa sauti yake na kumpa nyota nyingi begani kwa namna ambavyo mirindimo ya sauti hiyo iliweza kuyakuna masikio yao na kuwaamsha usingizini.

Kama ilivyo hali ya ubinadamu, wakaazi wa eneo hilo waliponogewa zaidi na sauti yake, walianza kumshindanisha na jogoo aliyekuwa anatamba katika eneo hilo. Jogoo ambaye sauti yake ilikuwa imefika karibu kona zote za bara la Afrika. Ukaanza kusukwa mgogoro. Kwa lugha ya kigeni ‘beef’. Watu wakauivisha na maandishi yakaanza kusambazwa kuwa majogoo hao wawili wana ugomvi mkubwa kwani kila mmoja anajua ‘yeye huwika vyema zaidi ya mwenzake’.

Hata hivyo, alfajiri moja, wakati ambapo wakaazi wa eneo hilo walikuwa wamekaa mkao wa kutaka kusikia ni jogoo yupi atawika vizuri zaidi ya mwenzake na kuanza kutabiri nani zaidi, ghafla walisikia majogoo hao wamekubaliana kushirikiana kuwika kwa pamoja na yote yaliyokuwa yanasukwa ‘Ikabaki Story’. Yaani wa pili ameamua kuwa chini ya yule aliyesikika hadi nje ya bara. Sauti ya majogoo hao wawili zilisikika kwa kishindo kikuu walipoamua kuwika pamoja ‘Kokoro’. Afrika ilisimama dede.

Akiwa chini ndani ya banda lenye majogoo wengine ‘Wasafi’, banda ambalo ni maarufu kwa sauti zenye ladha ya aina yake ambazo kila zikisikika zinafunika na kuzua gumzo, jogoo huyo alishirikiana pia na mmoja aliyemkuta ndani ya banda, wa kwanza kuingia na mwenyeji wa banda hilo aitwaye Harmonize  na wakasikika wakiwika ‘Show Me’, Hakika walifanikiwa.

Kishindo cha mwaka kilisikika pale ‘Banda Zima la Jogoo Wasafi’ walipoamua kuwika kwa pamoja ‘Zilipendwa’. Amsha-amsha yao ya pamoja alfajiri hiyo imeweka historia ya kukusanya views zaidi ya milioni 18. Mavoko pia alichangia!

Lakini waswahili husema ‘ya ndani ya nyumba’ ayajuaye ‘panya’ na waishio ndani!

Mara paaap! Rich Mavoko, jogoo aliyeingia ndani ya banda akiwa anamashabiki wengi wanaoamini uwezo wake wa kuwika, alijiondoa kwenye banda hilo na kudai anaonewa, kwamba hapati mrejesho unaolingana na namna anavyowika. Kwamba kuna kupe ndani ya banda, hivyo anaomba asaidiwe asiendelee kunyonywa. Hata kabla ya kupata majibu yote, tayari aliamua kuanzisha banda lake la awali ‘Bilionea Kid’, ambapo atakuwa anawika mwenyewe na kualika majogoo wapya.

Kupitia picha hiyo, uamuzi wa Rich Mavoko sio tu kwamba umepokelewa kwa mitazamo tofauti, bali pia umesababisha mashabiki wa WCB na waliokuwa mashabiki wa Mavoko kuwa kwenye sintofahamu ya nini kinachofuata. Kisha wamemuandalia mzani wa aina yake.

Kikubwa, Mavoko amekuwa kwenye ‘spotlight’, wengi wakisubiri kuona nini ambacho atafanya na madhara yake kwenye ulimwengu wa muziki.

Hali hiyo imesababisha wimbo wake mpya ‘Ndegele’ kuvuta maoni mengi, wengine wakimpongeza na wengine wadai amepotea na kwamba ni bora angebaki WCB. Ni dhahiri kwamba karata hii ya kwanza kutupa akiwa peke yake, ukiacha ‘Happy’ inayodaiwa kuvuja, haikupata mapokezi makubwa kama ilivyokuwa kwa nyimbo zake nyingine kabla na hata akiwa ndani ya WCB.

Sio kwamba wimbo huo sio mzuri, la hasha. Ni kwa sababu sasa mashabiki wengi wanampima Rich Mavoko aliyekuwa anawika ndani ya Banda la Wasafi, na Rich Mavoko anayewika akiwa peke yake. Hii ni changamoto kubwa kwake kwani ni vigumu kwake kuwika kwa sauti kubwa zaidi ya sauti ambayo ilikuwa ikisikika ikisaidiwa na nguvu ya waliokuwa wakimlea ndani ya Banda hilo. Sasa anajitafutia. Matarajio ya mashabiki wake ni makubwa kupita kiasi!

Alipowahi kuulizwa anaona utoauti gani kuwa peke yake na kuwa ndani ya WCB, Mavoko aliwahi kukiri kuwa akiwa ndani ya WCB amekuwa na wakati mzuri zaidi kwani anachotakiwa kufanya ni kuandaa ‘ngoma kali tu na kupanga jinsi ya kuwika’. Lakini alipokuwa nje, ilibidi awaze yote yeye mwenyewe, jinsi ya kufanya nyimbo na jinsi ya kufanya promosheni ya nyimbo hizo.

Kutaka kumfananisha Mavoko na kundi la WCB kwa siku chache hizi tangu atoke, ni sawa na kumshindanisha mtu aliyekuwa amekabidhiwa duka kubwa aweke bidhaa zake tu halafu kuna timu ya kuuza bidhaa hiyo, na mtu ambaye anabidhaa zake chache mkononi na yeye ndiye muuzaji na mtaji wake haulingani na ule wa duka.  Kisha ukataka kushindanisha mauzo/mapato.

Ufananishaji huo ndio umewafanya wengi kuanza kuzipima ubavu ‘Nibebe’ na ‘Ndegele’, zilizotoka ndani ya siku kadhaa. Unaweza kujua nini kitatokea. Zote kali lakini…!

Rich aliwahi kueleza kuwa wakati watu walitaka kumshindanisha na Diamond kabla hajaingia WCB, walisahau kuwa yeye alikuwa na nyimbo chache kubwa, huku mwenzake alikuwa na mrundikano wa nyimbo hizo zinazotosha Albam. Pia, Mondi alikuwa na timu nzuri na kubwa pamoja na mtaji.

Leo, Kokoro iliyotoka mwaka 2016 imetazamwa zaidi ya mara milioni 4, ‘Show Me’ akiwa na Harmonize imetazamwa zaidi ya mara milioni 9.

Lakini kutangulia sio kufika, kwa kipaji na uwezo mkubwa alionao Mavoko, lolote linaweza kutokea. Huenda tukawa na WCB nyingine kwenye ‘Bilionea Kid’, hakuna aijuaye kesho. Hakuna mwenye utambuzi mzuri wa muziki atakayethubutu kusema Rich hajui, wengine wanamuita Messi wa Bongo Fleva.

Lakini, kwakuwa ni ngumu kuzima nia ya mashabiki kutaka kupima kila wimbo wa Mavoko utakaotoka na nguvu ya WCB, ngome ambayo hivi sasa ni ‘Barcelona’ ya Bongo Fleva; au kulinganisha madhara aliyokuwa nayo kwa ngoma alizotoa akiwa WCB, ni dhahiri kuwa hivi sasa “Mavoko Kazi anayo”.

Wengi wanasubiri kuona anavuka mstari wa ‘Show Me’, ‘Kokoro’, ‘Rudi’, Imebaki Story’, ‘Sheri’.

Tuanopenda muziki mzuri bila kujali mengineyo, tunamtakia kila la kheri.

 

Ndugulile apiga marufuku watu kujipima Ukimwi
Video: Ngoma mpya ya Harmonize 'Atarudi'