Wakati wa furaha kuna mambo unayotarajia kuyasikia kama ilivyo wakati wa majonzi, lakini katika nyakati zote hizi hakuna kitu kibaya kama kutaka kusikia ‘unachotaka kusikia wewe’ hata kama kinakinzana na uhalisia ili kuridhisha hisia zako tu.

Hali hii ndiyo iliyojitokeza ndani ya saa 12 zilizopita, saa zilizotanguliwa na takribani saa 24 za majonzi, taharuki kuu na sintofahamu ya walipo wasanii Roma Mkatoliki na wenzake watatu.

Saa chache baada ya kupata taarifa kuwa Roma na wenzake wamepatikana na wako mikononi mwa Polisi, hali ilikuwa shwari na kila mmoja mwenye nia njema alifungua vifungo vya moyo wake na kuhema huku akimshukuru Mungu. Lakini pia baadhi ya maswali yasiyo na majibu yalianza kutawala, hali ambayo ni ya kawaida.

“Wamefikaje Oysterbay Polisi, nani kawapeleka, walikuwa wapi, nini kiliwatokea, kwanini kuna usiri n.k.”

Maswali hayo yaliwekwa kiporo kusubiri kauli ya Roma ambaye baada ya kuhojiwa na kufanyiwa vipimo katika hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam alieleza kwa ufupi kuwa wako salama kiafya na kuomba akapumzike, lakini angeeleza ‘YOTE’ siku ya Jumatatu.

Hata hivyo, Roma huyo aliyedai afya yake iko sawa alionekana akichechemea na mwenye sura ya taharuki, hali iliyokinzana na neno la kuwatoa hofu watanzania kwa ujumla.

*Dosari kuu ilianza kutokea kwenye mitandao ya kijamii baada ya ahadi ya Roma akitaka watu kusubiri kutoka Jumamosi hadi Jumatatu kupata ukweli, subira ikawashinda wengi na kuanza kuandika fikra zao.

Kwa wataalam wa habari na mawasiliano wakati wa majanga tunafahamu kuwa kwenye ‘crisis’ usiache ‘pengo (gap)’ kwa sababu watu watakusemea. Hilo ni kosa la kitaalam lililotokea, na baadhi ya watu wenye nia mbaya walilitumia kupanda mbegu mbaya.

Mbegu hiyo mbaya iliwakuta hata wasanii wakubwa na watu wenye ushawishi ambao walidai kuwa ‘Roma alishiriki kupanga tukio hilo kama filamu na kwamba alilipwa fedha’. Cha ajabu ni kwamba hao ni miongoni mwa waliopaza sauti kumtafuta.

Yaliyoandikwa mtandaoni yalimliza zaidi Roma ambaye wakati wa mkutano wake na vyombo vya habari ilimpasa kuanza nalo kwa uchungu akilaani vikali mtazamo huo.

Roma aliyeketi karibu na Waziri wa Habari, Dkt. Harrison Mwakyembe na pembeni mkewe, Nancy alisimulia kilichowasibu huku akionesha majeraha yaliyotokana na vipigo na mateso wakiwa chini ya watekaji wao, akiweka mipaka ya maelezo ambayo alisema yangeharibu upelelezi wa polisi.

Cha kushangaza, ingawa Roma ameonesha majeraha yanayosikitisha na kueleza jinsi walivyoteswa na wavamizi wenye silaha za moto na kuachiwa baadae hadi walivyofika Polisi, bado kutosema ‘YOTE’ kumewafanya baadhi ya watu kuendelea kuandika ‘upuuzi’ mzito wakidai ni ‘FILAMU’! Hali hii ni kama kumcheka mfiwa au aliyenusurika kifo ukidai ni maigizo.

Tusiishie kwa Roma na kumhukumu kwa kutosema ‘YOTE’, tukumbuke yaliyomkuta Dkt. Steven Ulimboka mwaka 2012, baada ya maelezo ya awali ya namna alivyotekwa na kuteswa, mengine aliviachia vyombo vya dola na hakujitokeza tena kueleza. Je, naye alijiteka na kufanya filamu?

Wengine wanadai Roma anajiua kimuziki baada ya kuonekana kutosema wanachotaka kusikia wao. Huu pia ni ‘upuuzi’ mwingine mzito zaidi. Yaani baada ya kunusurika kifo, kutekwa na hata sasa kiakili bado atateseka na kuishi kwa hofu, kuna mtu anadai anajimaliza kimuziki.

Kumbuka alitekwa kwa silaha za moto akiwa anafanya muziki na mtu huyo hukuwepo wakati huo, hajui alikuwa anarekodi nini na nini kingetokea kwenye maisha yake ya muziki. Usiyatumie maumivu yake kutabiri maisha ya muziki wake kwa kejeli kwani hujui kesho yako.

Roma anadai mtayarishaji wa muziki ‘Bin Laden’ aliyetekwa naye bado hayuko sawa kisaikolojia na hupiga kelele wakati mwingine akikumbuka tukio hilo. Kwa waliohudhuria walishuhudia hata baada ya mkutano huo Roma alikuwa akilia machozi, ina maana nayeye pia kisaikolojia anaendelea kuteseka na tukio hilo.

Baadhi ya watu wameenda mbali na kukosoa kitendo cha mkutano wake wa vyombo vya habari kuandaliwa na ofisi ya Habari Maelezo chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na uwepo wa Waziri mwenye dhamana pamoja na namna ulivyoendeshwa kwa baadhi ya maswali kuzuiliwa.

Hili lilikuwa nje ya uwezo wa Roma na uongozi wa Tongwe Records ambao pia ulihudhuria kwani tatizo hili tayari lilikuwa mikononi mwa Serikali na ni tukio nyeti, hivyo Serikali ilichukua nafasi ya kuhakikisha msanii huyo anakuwa kwenye mikono salama na ilibeba umuhimu wa mkutano huo.

Tukumbuke Roma na wenzake walikuwa chini ya watekaji, hakuna mtekaji duniani anayekuachia bila masharti, huenda na narudia huenda walipewa masharti fulani yanayoathiri wanachozungumza. Lakini pia kuna utaratibu walipewa na polisi ambao  pia unaweza kuwa sehemu ya athari ya wanachozungumza.

Pamoja na yote, nikiri tu kuwa mkutano huo pamoja na maelezo ya Roma ulizua maswali mengine mengi zaidi na wengi hawakuridhishwa. Lakini ukweli unabaki palepale kuwa tukio hilo la kusikitisha na kuudhi halipaswi kuchukuliwa kama filamu tena na baadhi ya wasanii ambao tasnia yao imeguswa.

Hali sio shwari, Mbunge Hussein Bashe jana ameweka wazi taarifa yake kuwa ametishiwa kutekwa na kwamba yuko kwenye orodha ya wabunge 11 huku Ben Saanane pia akiwa hajulikani alipo hadi leo. Suala hili halipaswi kuchukuliwa kwa kejeli. Tuendelee kusimama pamoja na kuachana na ‘upuuzi’.

Tukumbuke kuwa nguvu ya mitandao ya kijamii ilisaidia sana kupaza sauti kumpata Roma na wenzake, tusitumie nguvu na mitandao ileile kupuuzia suala hili na kuziumiza zaidi familia za waathirika.

Kumbuka kauli ya mwisho ya Roma kuwa hadi sasa hawana uhakika na usalama wao. Je, wewe una uhakika na usalama wako?

Kusema Roma anafanya filamu ni upuuzi unaopaswa sio tu kupuuziwa bali pia kulaaniwa vikali. Tukio la utekaji kwa namna yoyote ile, linapaswa kulaaniwa tena kwa kutumia nguvu zaidi ya iliyotumika awali.

Tuungane kutatua tatizo sio kupunguza ukali wa tukio la Roma na wenzake kwa hisia zetu binafsi. Wote tunaishi kwenye ‘nyumba za vioo’ tusimfumbie macho kichaa aliyeshika mawe!

Ole Nasha apigilia msumari wa moto biashara ya mayai
Magazeti ya Tanzania leo Aprili 11, 2017