Na: Josefly Muhozi

Kama ulishtushwa na kipigo cha manyanyaso cha Andy Ruiz Jr. alichomshushia Anthony Joshua Julai 1, 2019 katika ukumbi wa Madison Square Garden jijini New York, basi wewe ni mmoja kati ya wale wengi waliokuwa hawamfahamu bondia huyo raia wa Mexico, na huenda ukawa na matumaini yanayoweza kuzikwa kesho, Desemba 7, 2019 mabondia hao watakapopanda tena ulingoni jijini Diriyah, Saudi Arabia.

Ni Ruiz Jr. anayefahamika kwa jina mbadala ‘aka’ rasmi kama ‘Destroyer’ aliyeharibu rekodi za wengi akiwemo Anthony Joshua, huenda akaendelea mbele na kuharibu maisha ya bondia huyo mwenye asili ya Nigeria kesho usiku. Hivi sasa anatajwa kuwa bondia namba mbili kwa ubora (uzito wa juu) baada ya Deontay Wilder.

Nimeanza na utangulizi huu nikifahamu dhahiri kuwa kama ilivyokuwa kwenye pambano la kwanza la uzito wa juu, Ruiz Jr. ambaye Tanzania ilimbatiza jina la ‘kibonge mwepesi’ anapanda ulingoni kesho akiwa anapewa nafasi ndogo zaidi ya kushinda (underdog). Joshua anapewa hadi 71.43% za kushinda huku Ruiz Jr. akielezwa kuwa alibahatisha pambano la kwanza; hivyo mwisho wake umefika.

Mabondia wote wametangaza vita nzito wakati huu, walipokutana jana kwenye mkutano na vyombo vya habari. Wakati Anthony Joshua akiahidi kurekebisha makosa yake yote, Ruiz Jr. yeye ameahidi “I’m willing to die in the ring, I’m not here to take part, here to take over.” Akimaanisha kuwa yuko tayari kufia ulingoni na kwamba hayuko hapo kushiriki bali kushinda.

Wakati mara ya kwanza ilikuwa rahisi hata kwa mabondia wengine kutabiri mshindi, wakati huu imekuwa ngumu sana kwa wajuzi wa ndondi kutabiri. Mike Tyson yeye amepata kigugumizi kikuu, “sijui kwakweli nini kitatokea sasa hivi, kwa sababu naona kama chochote kinawezekana.”

Lenox Lewis yeye anaamini kuna nafasi kubwa ya Ruiz Jr. kushinda tena. “Kama hawatarekebisha walipokosea, Ruiz Jr. atashinda kirahisi tena mikono yake ikiwa chini.”

Kama ulikuwa haumjui, Ruiz Jr. ambaye anarejea ulingoni kutetea mikanda minne ya ubingwa wa dunia wa uzito wa juu aliyomvua Joshua kwa kipigo cha KO katika raundi ya 7; huyu ni Simba aliyekuwa akiwatafuna wenzake kimyakimya. Hakufahamika kwa wengi hadi alipomtafuna Joshua aliyeitwa ‘mbabe wa wababe na Simba’ aliyejenga ngome yake Uingereza, akiujaza uwanja wa mpira wa ‘Wembley’ karibu kila pambano.

Hii haikuwa mara ya kwanza kwenye historia ya Ruiz Jr. kuwawekea doa wababe kama Joshua, baada ya kuingia ulingoni akiwa anachukuliwa poa.

Tupitie mapito yake kidogo: Julai 27, 2013, Ruiz Jr. alisafiri hadi Macau nchini China, alipoenda kupambana na Mmarekani Joe Hanks ambaye alikuwa na rundo la mashabiki na rekodi ya kutopigwa katika mapambano 21(21-0, 14KOs). Ruiz aliwashangaza mashabiki baada ya kumpiga chini Hanks mara mbili katika raundi ya nne na kusababisha mwamuzi kusimamisha pambano. Ruiz akaondoka na mkanda wa ‘WBO – Intercontinental heavyweight’.

Baada ya miezi mitatu, alilazimika kutetea ubingwa wake kwenye ulingo uleule lakini akapewa mbabe mwingine, Tor Hamer. Ruiz Jr. alitembeza kipigo kikali na kusababisha muamuzi kusimamisha pambano baada ya raundi ya tatu, baada ya mpinzani wake kugoma kurejea ulingoni akiwa kwenye kona yake. Alijua akirejea tu ‘kibonge mwepesi’ atammaliza.

Hii ni mifano miwili tu kati ya mapambano 22 ambayo Ruiz Jr. aliwazimisha wapinzani wake tena wababe tangu mwaka, Machi 28, 2009 alipoingia rasmi kwenye ngumi za kulipwa (professional) akiwa na umri wa miaka 19. Nikueleze tu kuwa hata pambano lake la kwanza alimzimisha mpinzani wake katika raundi ya kwanza tu.

Tangu alipoingia kwenye ngumi za kulipwa, amewahi kushindwa mara moja tu kati ya mapambano 34. Pambano pekee alilowahi kupoteza, lilikuwa dhidi ya Joseph Parker. Ruiz alimfuata Parker nyumbani kwao Auckland, New Zealand, Desemba 10, 2016. Parker alikuwa mbabe, hakuwahi kupoteza hata mchezo mmoja wakati huo akishinda mapambano yote 21, na 18 kwa KO (21–0 (18 KOs). Ruiz Jr. pia alikuwa hajawahi kupoteza, alikuwa na rekodi ya kushinda mapambano yote 29, na 19 kwa KO (29-0,19Kos).

Nikukumbushe tu kuwa huyu Parker ndiye mbabe pekee ambaye amewahi kupambana na Anthony Joshua na kumaliza naye raundi 12, yaani hakupigwa KO. Pambano lao lilifanyika Machi 31, 2018.

Sasa, katika pambano la Ruiz Jr. na Parker mwaka 2016, hadi pambano linamalizika wengi waliamini Ruiz Jr. ndiye mshindi. Hata hivyo, mcheza kwao hutuzwa, Parker alitangazwa kuwa mshindi kwenye pambano hilo kali. Majaji wawili walimpa ushindi Parker kwa tofauti ya raundi mbili (115-113), na jaji mmoja aliamua kuwa ilikuwa sare (114-114).

Andy Ruiz Jr. akimshambulia Joseph Parker

Wakati dunia ya masumbwi ikiwaangalia zaidi Anthony Joshua, Tyson Fury, Luis Ortiz raia wa Cuba na Deontay Wilder kama wababe na Simba kwenye masumbwi ya uzito wa juu, ilifanya kosa la kufumba macho na kumchukulia poa Ruiz Jr., Kibonge mwepesi.

Huyu ni jamaa ambaye aliingia kwenye ngumi za kulipwa akiwa na uzoefu wa kutosha na rekodi nzuri aliyoipata katika ngumi za ridhaa (armature). Alimaliza armature akiwa na rekodi ya kushishinda mapambano 105 akipoteza mapambano matano tu (105-5). Hivyo, ushindi ni sehemu ya maisha yake.

Hata hivyo, Ruiz Jr. aliendelea kuwatafuta wababe kimyakimya na kuwawekea doa. Aliamini kuwa ili uwe bora zaidi ni lazima uwapige mabondia bora zaidi (to be the best you need to beat the best). Aliendelea kuzitafuta fursa za kupambana na wale wanaotajwa zaidi na vyombo vya habari lakini jina lake halikuwa linatajwa hata kidogo. Hadi ilipotokea zari la mentali alipoinasa nafasi ya kupambana na Anthony Joshua, hali iliyowafanya wengi kuamini atapigwa kama begi la mazoezi (punching bag). Waliendelea kufumba macho wasitake kumjua huyu Simba anayewatafuna wenzake kimyakimya.

Alivyopata kimiujiza pambano dhidi ya Anthony Joshua:

Anthony Joshua alipanga kupambana na Jarrell Miller, bondia mbabe kutoka Marekani. Lilikuwa pambano kubwa, Joshua alitundika mikanda yake minne (WBA (Super), IBF, WBO, and IBO). Hata hivyo, ilitangazwa habari mbaya, baada ya Kamisheni ya Michezo ya New York kutangaza kuwa Miller alishindwa vipimo na aligundulika kuwa anatumia dawa zisizokubalika kwenye michezo.  Hivyo, hakuwa na sifa ya kuendelea na pambano.

Chaguo la pili la timu ya Joshua ilikuwa Luis Ortiz, mbabe mwingine hatari kutoka Cuba. Lakini baada ya muda, kambi ya Ortiz ilitangaza kujiondoa kwa madai kuwa hawakuafikiana kwenye suala la malipo. Hapo Joshua alibaki hana mbadala, akiendelea kutafakari nani apande naye ulingoni.

Ruiz Jr. aliiona hiyo fursa, akamtumia ujumbe kupitia intagram (DM) meneja wa Joshua, Eddie Hearn. Yeye malipo kwake haikuwa ‘issue’ kubwa. Hiyo ikawa tiketi ya yeye kupata nafasi, wakakaa chini wakakamilisha mkataba akatangazwa kuwa ndiye atakayechukua nafasi.

Kabla ya pambano, Ruiz alimuonya mara kadhaa Joshua kuwa asimchukulie poa kwa kumuangalia umbo lake. “don’t underestimate this little fat (usimchukulie poa huyu mvulana mdogo-mnene.” Ujumbe huu haukuwa na maana sana kwa Joshua hadi baada ya pambano hilo.

Katika pambano hilo la kwanza, Joshua ndiye aliyekuwa wa kwanza kumpiga chini Ruiz katika raundi ya tatu kwa konde zito lililofumua kidevu chake. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Ruiz Jr. kudondoshwa chini katika mapambano 33, akiwa ameshinda kwa KO mara 22 na kushindwa mara moja tu. Akiwa chini asimini kilichokuwa kinamtokea, aliinuka akiwa na nguvu zaidi na kumshambulia Joshua kwa makonde mazito yaliyompeleka chini akiwa ameumia zaidi. Alimuongeza kipigo kingine baada ya kufanikiwa kuamka kilichompeleka tena chini mbabe huyo na kuhesabiwa kwa mara ya pili lakini alifanikiwa kuinuka na kuendelea. Hapo alianza kuona dunia inamtendea ndivyo sivyo, asiamini aliyekuwa anamtesa muda huo ni kibonge mfupi.

Kama ilivyokuwa kwa wababe wengine, kasi ya ngumi za Ruiz Jr. ilimshinda Joshua katika raundi ya saba ya pambano hilo akipigwa chini na kuonesha dalili zote za kupotea hadi mwamuzi alipoamua kumaliza pambano na ushindi ukaenda kwa ‘Kibonge Mwepesi’. Hii ikatajwa kuwa ni ‘the biggest upset in boxing history’.

Silaha za ushindi za Ruiz Jr.

Ruiz Jr. ambaye amepita mikononi mwa kocha Freddie Roach (kocha wa Manny Pacquiao), Abel Sanchez (kocha wa Gennady Golovkin) na sasa anafuliwa na Rob McCracken, silaha yake muhimu zaidi ya ushindi siku zote ni ‘kasi ya ngumi zake’.

Kasi ya masumbwi mazito anayoyarusha ndiyo tatizo kubwa linalowakabili wapinzani wake. Ingawa ni bondia wa uzito wa juu, kasi ya masumbwi yake ni kama wa uzito wa kati. Uwezo wake wa kukwepa masumbwi na kuvumilia pia (ndio sababu hakuwahi kuangushwa chini hadi alipopigwa na Anthony Joshua).

Hivyo, ili Anthony Joshua apone kwenye mikono ya huyu ‘Kibonge Mwepesi’ ni lazima akae mbali na asijaribu hata kidogo kujibizana masumbwi ya papo kwa papo (trading shots). Akijaribu matokeo yatakuwa kama ya awamu ya kwanza.

Yote kwa yote, aliyepewa nafasi zaidi ya kushinda na Anthony Joshua, lakini kivipi bado wajuzi wanakuwa na mashaka pia.

Bingwa wa zamani wa Dunia wa masumbwi ya uzito wa juu, Muingereza David Haye, yeye anamshauri Joshua mbinu ya kushinda akisisitiza kuwa anapaswa kuhakikisha anamfanya Ruiz Jr. anabadili mbinu ya kupambana la sivyo itakuwa ngumu.
“Kama Joshua atafanikiwa kujenga uwezo wa kuongoza kwenye raundi za awali, ninategemea Ruiz abadili mbinu na kuanza kuthubutu kujiingiza kwenye hatari (to take risk). Kama itakuwa hivi, Joshua atakuwa na nafasi nzuri ya kumpiga kwa KO kati ya raundi ya 10 na 12.

Maneno yote yatahitimishwa kesho usiku baada ya vitendo kuzungumza. Lakini kama mchambuzi, naamini pambano hili halitafika raundi 12. Ruiz ameahidi kufia ulingoni, Joshua ametangaza kurudisha heshima yake. Tusubiri.

TCRA yasisitiza simu zisizosajiliwa kuzimwa Desemba 31, Wasichana waonywa kuhonga wanaume
Mbinu ya kugeuza kuku wa kisasa kama wakienyeji yafichuliwa