Kumekuwa na vutankuvute kati ya vyama vya upinzani na serikali ya CCM iliyoko madarakani kuhusu uamuzi uliotangazwa kwanza na Jeshi la Polisi nchini na baadae kupigiwa mstari na Rais John Magufuli, kupiga marufuku mikutano ya kisiasa nchini.

Ingawa Jeshi la Polisi lilieleza kuwa marufuku hiyo inatokana na taarifa za kiintelijensia za kuwepo kwa harufu ya vitendo vya uvunjifu wa amani na uhamasishaji wa watu ili wasitii sheria za nchi, Rais Magufuli alieleza kwa upana zaidi akiwataka wanasiasa kusitisha na kufanya siasa kwa nguvu zaidi baada ya miaka 5, yaani 2020.

“Niwaombe wanasiasa wenzangu wafanye siasa za ushindani kwa nguvu zote baada ya miaka mitano ili wananchi watuhoji tuliyowaahidi kama tumeyatekeleza au hatukuyatekeleza,” alisema Rais Magufuli baada ya kupokea ripoti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhusu uchaguzi mkuu uliopita.

“Haiwezekani mkawa kila siku ni siasa, watu watalima saa ngapi? Kila siku ni siasa, ni vyema tukatimiza wajibu wetu tuliopewa na wananchi na watatupima kwenye hilo,” aliongeza.

Baada ya kauli hiyo, vyama vya upinzani nchini pamoja na wanaharakati walikosoa vikali wakidai kuwa huo ni mpango wa kutaka kudhoofisha upinzani nchini. Ni dhahiri kuwa huo ni mtazamo ambao wengi, hata wa CCM wanaweza kuchukulia.

Wakati Rais Magufuli anatoa tamko hilo, vyama vya upinzani vilikuwa tayari vimekumbana na misukosuko ya kutosha bungeni ambayo hawajawahi kukutana nayo kwa kiwango hicho tangu kuanzishwa kwa vyama vingi nchini. Hata matendo yao ya kupinga pia yalikuwa ya aina yake kuwahi kuonekana kwenye historia ya Tanzania. Wengine walidai ilikuwa ‘Burudani inayoongea makubwa’.

Wengi wanaamini kuwa hayo yote yametokana na njia zinazotumika kuzuia nguvu ya upinzani kutokana na upinzani mkali katika historia ulioonekana katika uchaguzi mkuu uliopita, ambapo upande wa vyama vya upinzani vilivyounda Ukawa, ulimsimamisha mgombea mmoja, Edward Lowassa (Chadema).

Lowassa aliyepata kura nyingi zaidi katika historia ya vyama vingi kama mgombea wa upinzani, alikuwa tayari ameshaongoza katika tafiti mbalimbali za awali alipokuwa CCM akioneshwa kuwa ndiye kada mwenye nguvu zaidi.

*Nguvu ya Lowassa ilionekana tangu akiwa kada wa CCM ambaye tangu alipojiuzulu nafasi ya Uwaziri Mkuu mwaka 2008, hakuwahi kufanya mkutano wa hadhara wa kitaifa kujinadi hadi wakati wa mchakato wa kura za maoni mwaka 2015.

Wakati huo, katika kipindi cha miaka 6, vyama vya upinzani vilitumia nguvu kubwa ya mikutano ya hadhara kuwaponda makada wa CCM, huku Lowassa akiwa muathirika zaidi. Kwa mtazamo wao waliamini walikuwa wakififisha nguvu ya Lowassa na CCM.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa akikabidhiwa fomu na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa akikabidhiwa fomu na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.. katika mkutano huo, jina la Lowassa lilishambuliwa ipasavyo

Naomba ikumbukwe pia kuwa tangu Lowassa ajiuzulu, amewahi kuongea Bungeni sio zaidi ya mara mbili tu. Nakumbuka zaidi kuwa ni mara moja tu aliposema kuhusu ‘nchi ya watu wanaolalamika inayohitaji mtu mmoja mwenye maamuzi magumu’.

Lakini ilipofika mwaka 2015, tafiti zote bado zilionesha kuwa Lowassa ndiye mgombea mwenye nguvu hata zaidi ya waliowahi kuwa wagombea urais wa Upinzani ambao kila mwezi walikuwa majukwaani wakiikosoa serikali na kumkwaruza Lowassa.

Alionekana ana nguvu kubwa zaidi hata zaidi ya wale wa CCM ambao walikuwa na nafasi ya kukaa jukwaani kwa saa kadhaa na kujinasibu na kuchambua CV zao kwa miaka yote. Waliweza kuzungumza bungeni zaidi ya mara zote wakipata nafasi.

Baadae, Lowassa alihamia Chadema baada ya jina lake kukatwa na Kamati Kuu ya CCM na kukosa nafasi ya kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho.

Hata hivyo, mchakato wa kampeni za uchaguzi Mkuu na kuibuka kwa jina la Dk. John Magufuli ambaye wengi hawakumtegemea, kulibadili picha nzima na kuleta ushindani mkali hadi kushinda uchaguzi huo na kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nirudi tena kwenye reli ya kichwa cha Makala hii baada ya kukupa picha nzima. Kwanini Lowassa alikuwa na nguvu kubwa bila mikutano ya hadhara;

Lowassa alikuwa bingwa wa kujijenga kimyakimya ama chinichini kuanzia ngazi za matawi, shina na hata nyumba kwa nyumba. Alikuwa na timu nzito ambayo hata siku moja haikuwahi kumnadi kwenye mikutano ila ilikuwa inafanya kazi kubwa chinichini, hadi leo inadaiwa kuwa ameacha ‘masalia’ wanaoitafuna CCM.

Kwa maana hii, marufuku inayotolea hivi sasa kuhusu mikutano ya hadhara, haiwezi kuwa sababu ya kumdhoofisha Lowassa ambaye ni kada wa Chadema. Huenda ikadhoofisha ‘harakati’ za kisiasa zilizozoeleka kwa vyama vya upinzani nchini. Lakini sio Lowassa ambaye sasa hivi ni Chadema!

Kwa bahati nzuri, jana Lowassa amewaweka wazi Chadema akiwataka kutotetereka na marufuku hizo bali kukijenga chama katika ngazi zote za mashina na matawi. Hii ina maana anaanza kuwaambukiza mbinu yake ya kujikuza chini chini.

“Wana hofu kwakuwa wanajua walichokipata katika uchaguzi uliopita. Ndio kinachowafanya waendelee kuogopa. Chadema nawaomba msifanye kazi kwa mazoea, tuendelee kushikamana na wananchi na tusifikie mahala wananchi wakasema afadhali CCM,” alisema Lowassa.

Mwanasiasa huyo mkongwe aliwashauri kutohangaikia mikutano ya hadhara na kuja na mbinu mpya, “kuzuia mikutano ya kisiasa ni kinyume cha sheria. Lakini hawawezi kutuzuia, sisi tutafanya mikutano na kuhutubia kwa kutumia mitandao ya kijamii na tutawapa wananchi fursa ya kuuliza maswali na tutawapa majawabu.”

Lowassa alisisitiza kuwa Chadema ‘hivi sasa’ imehitimu kutoka kwenye uanaharakati kuwa chama cha siasa chenye lengo la kushika dola.

*Mtazamo wangu ni kwamba, inawezekana kabisa kwamba baada ya miaka mitano, bila hata mikutano hiyo ya hadhara, kama haitakuwa vinginevyo, uzoefu unaonesha kuwa Lowassa atakuwa na nguvu huenda zaidi ya ile ya awali kwani sasa atakuwa hana wa kumkwaruza jukwaani kama ilivyokuwa awali.

Ukimya wa Lowassa kwa uzoefu ni hatari kwa upande wa pili zaidi hata ya anapozungumza mara kadhaa. Lowassa ni kama simba anayeishi kwenye nyasi ndefu, haungurumi mara kwa mara lakini haimaanishi kuwa amedhoofika.

Ureno yatwaa kombe la Ulaya, yaacha kilio Ufaransa
Mourinho ang’oa ‘hirizi’ za Van Gaal uwanja wa mazoezi, apachikwa jina jipya