Na Ghati:

Sauti yenye Mamlaka ya kijeshi ilisikika ikiongoza kiapo cha utii katikati ya umati wa askari wakakamavu. Ingawa Mkuu wa jeshi la kupambana na wahalifu alikaza koo lake kuhakikisha kiapo kinakuwa na nguvu, uso wake ulitoa ujumbe tofauti. Macho yake yalibubujikwa na machozi. Mitetemo ya mashavu na mikunjo ya sura ilianza kuchomoza. Hakuna siri tena! Hisia zilimzidi nguvu.

Taratibu sauti yenye Mamlaka ilianza kusikika kama sauti ya mtu anayesimulia mkasa mzito uliomtoa machozi kwa kuelemewa na kumbukumbu ya yaliyomfika.  Kulikoni!?

“Ninaahidi sasa na daima… kuendelea kupambana na wahalifu hadi pale saratani yangu yote itakapotokomea.”

Ni mkuu wa Idara ya Polisi katika jimbo la Texas nchini Marekani, Ray Garivey aliyekuwa akimsaidia msichana mwenye umri wa miaka sita tu, Abigail Arias kutimiza ndoto yake ya kuwa Afisa wa Jeshi la Polisi. Mtoto huyo mwenye saratani ya figo isiyo na tiba, alionesha ushujaa wa kushinda hofu ya kifo akiwa na furaha kubwa ya kutimiza ndoto yake ya kuwa Afisa wa Polisi.

Mtoto Abigail, aliamini kuwa chanzo cha maradhi yake ni wahalifu walio ndani ya mwili wake, hivyo alitaka kuwa afisa wa polisi ili akabiliane nao.

Akiwa ndani ya sare za jeshi la polisi alizoshonewa maalum kwa ajili yake, kwenye tukio hilo lililohudhuriwa na familia yake pamoja na idadi kubwa ya maafisa wa polisi wa jimbo la Texas walioonesha heshima kubwa kwa askari huyo mpya… Abigail, alikuwa kwenye kilele cha mafanikio ya maisha yake, akitimiza ndoto yake katika umri wa miaka sita tu. Ndoto ya ‘kupambana na wahalifu.’

Kwa mujibu wa taratibu na sheria za Texas, ili mtu ajiunge na jeshi la polisi, anapaswa kuwa na umri sio chini ya miaka 21 au miaka 18 kama ana elimu ya kiwango cha shahada. Lakini Februari 10, 2019 mtoto Abigail, shujaa aliyeshinda hofu ya kifo, alivunja rekodi na miiko na kutunukiwa nafasi hiyo kwa heshima.

Mtoto huyo, aliishangaza dunia kwa imani yake kuwa kutimiza ndoto yake ndio mafanikio ya maisha hata kuliko kuishi miaka mingi isiyofikia malengo. Hata baada ya kufahamu kuwa hataweza kuishi kutokana na ugonjwa wa saratani uliokuwa unamtafuna, kwake msiba haukuwa maisha yake binafsi bali kutotimiza ndoto yake akiwa duniani.

“Ari yake, uimara wake na utayari wa kuishi na kutimiza ndoto yake ndicho tunachokiamini,” alisema mkuu wa Polisi, Garivey.

Hakuna binadamu anayeishi asiye na ndoto, na kama huna ndoto na unapumua basi wewe hauishi bali uko hai tu! Kila mwenye utashi, bila kujali umri wake ana malengo (ndoto) katika maisha yake, na hayo ndiyo yanayomfanya aishi ili ayatimize. Kama unataka kumsaidia mtoto kuishi, msaidie kutimiza ndoto yake… ana ndoto ambayo kwayo anaishi.

Lakini utatambua vipi ndoto ya mtoto? Hapo kuna jambo la kufanya, mpe sikio na umakini kama alivyofanya Mkuu wa polisi Garivey kwa Abigail naye atakushangaza na ataishangaza dunia.

Garivey alifikiria nje ya box la hofu ya kifo dhidi ya mtoto Abigail, akampa usikivu wa dakika chache na kuyatilia maanani aliyoyasema. Na baada ya hapo mambo yalibadilika.

Garivey kama ilivyo kwa watu wengine, walisikia tatizo la saratani isiyopona lililokuwa linamkabili mtoto Abigail. Mtoto huyo alianza kupata matibabu tangu mwaka 2017. Ingawa madaktari walifanya juhudi kubwa kuokoa maisha yake, miezi mitano baadaye saratani ilirejea kwa kasi zaidi ikishambulia figo na mapafu; na madaktari waliweka wazi kuwa hakuna uwezekano wa kumtibu tena.

Desemba 2018, Garivey, Mkuu wa polisi, alimtembelea mtoto Abigail na kumpa usikivu. Alishangazwa na uwezo wa kujieleza wa mtoto huyo mwenye umri wa miaka sita tu. Ingawa alikuwa anakabiliwa na kifo, hakuonesha hofu bali tabasamu lake lilikuwa silaha pekee iliyowavutia wengi. Katika mkutano wao, alimueleza Garivey kinagaubaga ndoto yake yake ya kuwa Afisa wa Polisi.

“Tabasamu lake zuri na utayari wake wa kupambana na ‘wahalifu’ ulio ndani yake – nilitaka kuifanya ndoto yake itimie. Unapaswa kukutana naye kujua ni jinsi gani alivyo msichana bora, mwenye hamasa na anayehamasisha,”alisema Garivey.

“Aliniambia ‘nataka kuwa afisa wa polisi’, nilimgeukia baba yake nikamwambia, ‘huenda hakupaswa kabisa kuniambia hili’. Lakini nikamwambia tutalifanya hilo liwezekane,” aliongeza Garivey.

Baada ya mkutano huo, Garivey alianza kuhangaika, kutafuta namna gani anaweza kuvunja miiko ya taratibu za kujiunga na jeshi la polisi ikiwa ni pamoja na suala la umri, mafunzo na kiwango cha elimu, ili mtoto Abigail aweze kutimiza ndoto yake angalau kwa siku moja tu.

Haikuwa rahisi, baada ya kuhangaika kwa muda, aliishirikisha taasisi ya eneo la Pearland iitwayo ‘Cop Stop’, akiiomba msaada ikiwa ni pamoja na kutengeneza sare maalum za polisi kwa ajili ya Abigail.

Hatimaye, alifanikiwa… Abigail aliapishwa kuwa askari polisi kwa heshima kubwa. Ni kama unavyosikia wapo viongozi au watu wenye mchango mkubwa kwenye jamii ambao hutunukiwa shahada za heshima ikiwa ni pamoja na Shahada ya uzamivu (PhD).

“Ukimsikiliza na kumuangalia, ni msichana aliyetumwa na Mungu. Simulizi lake leo limewakusanya maafisa wa polisi kutoka maeneo yote, wamekutana kwenye chumba hiki na ulikuwa muda wa miujiza kwa wote waliohudhuria,” alisema Mkuu wa polisi, Garivey.

Baada ya tukio hilo, akiwa mwenye furaha kuu, Abigail alifanya kazi kwa siku moja, akizungushwa na gari la polisi la zamu ‘kuwasaka wahalifu’.

“Ninajisikia msafi ndani ya moyo wangu na ndani ya mwili wangu. Najisikia furaha, ninajisikia kupendwa,” alisema Abigail aliyevalia sare za polisi. “Ninataka kusaidia kuwaondoa kabisa wahalifu, ninataka kusaidia saratani hii iondoke mara moja ndani ya sekunde tano,” aliongeza akiwa anatabasamu.

Wazazi wake, walitokwa na machozi ya furaha. Kama ujuavyo, uchungu wa mwana aujuaye mzazi, mama yake aitwaye Eileen aliyekuwa anatokwa machozi akimuona mwanaye kwenye sare za polisi, alisema kuwa wameishinda vita ya hofu na anaamini mtoto wake atapona licha ya madaktari kusema ‘haiwezekani’.

“Tuko imara katika imani. Uimara wetu ni kuikataa hofu, tunamuamini Mungu. Madaktari wanaweza kusema imeshindikana, lakini tunajua mwisho wa maisha yake uko mikononi mwa Mungu,” alisema mama Abigail.

Amini, kila mtoto ana ndoto ambayo kwayo inamfanya aishi. Ukimsaidia kuifikia umemsaidia kutimiza lengo lake la kuishi duniani. Je, umewahi kumsikiliza mwanao na kufuatilia ndoto yake ili umsaidie kuitimiza? Au unamlea bora akue tu?

Wapo akina Abigail wengi duniani na wana ndoto! kuna Abigail Afrika, yupo Tanzania, yupo Mkoani kwako, Wilayani kwako, mtaani kwako na hata nyumbani kwako.

Je, umejifunza nini kwa mkuu wa polisi Garivey ambaye hakuchukulia poa maelezo ya Abigail, hakuishia kumuonea huruma na kumsikitikia kwa hali aliyonayo? Unamsaidiaje Abigail katika eneo lako!? Kwanza, mpe usikivu ujue ndoto yake. Pili, chukua hatua kwa namna inayofaa kutokana na uhalisia wake; na tatu, shirikisha wadau kukuza hatua uliyoichukua kumsaidia mtoto.

Wapo akina Abigail wanaotuzunguka. Utakumbuka pia simulizi la aina yake la mtoto Bradley Lowery, aliyekuwa na umri wa miaka mitano, mwenye ndoto kubwa kwenye ulimwengu wa soka lakini alikabiliwa na mtihani wa saratani inayojulikana kitaalam kama ‘neuroblastoma.

Desemba 2016, mtoto Bradley, shabiki mkubwa wa klabu ya Sunderland alifanikisha ndoto yake ya kuichezea klabu hiyo. Akiwa na umri wa miaka mitano, alipigiwa kura za mashibiki na kushinda tuzo ya goli bora la mwezi kwa mkwaju wake wa penati dhidi ya Chelsea. Aliwashinda wachezaji wakubwa kama Alexis Sanchez. Goli lake la mkwaju wa penati uliompita mlinda mlango, Asmir Begovic lilikuwa sehemu ya kilele cha mafanikio ya ndoto zake.

Bradley Lowery (Sunderland) akiwekana sawa na Diego Costa (Chelsea) kuhusu mchezo kati yao

Bradley aliyekuwa rafiki mkubwa wa Jermain Defoe, hata baada ya kufariki Julai 7, 2017 akiwa na umri wa miaka sita tu, maisha yake yalikuwa mbegu ya matumaini kwa ndoto za watoto. Iliundwa taasisi ya Bradley Lowery Foundation ambayo itadumu zaidi ikilenga kuwasaidia watoto wenye ndoto wanaokabiliwa na changamoto ya maradhi.

Bradley na rafiki yake Defoe wakitoka nje ya uwanja katika mchezo kati ya Sunderland na Everton

Hapa nchini, yapo makampuni na watu binafsi ambao wamewahi kujaribu kuwa Garivey kwa akina Abigail. Mfanomzuri ni kampuni ya Data Vision International iliyoko Mikocheni jijini Dar es Salaam. Imeshawafikia akina- Abigail wengi kuwasaidia kutimiza ndoto yao, lakini nikupe mfano mmoja tu ulio karibu.

Desemba 2017, Kampuni ya Data Vision International, ilisikia simulizi la mtoto Mariam Mwema (16) kupitia kampeni ya ‘Tuko Pamoja’ ya Dar24. Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kawe Ukwamani jijini Dar es Salaam, ambaye alilazimika kukatisha masomo yake akishindwa kufanya mitihani ya kidato cha nne kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa unaofahamika kama ‘Intestinal Obstruction’. Mariam alikuwa amefanyiwa upasuaji wa tumbo mara kumi hapa nchini bila mafanikio kutokana na utumbo kujikunja.

Data Vision walimpa Mariam usikivu, waliguswa na ndoto yake ya kuwa daktari bingwa wa upasuaji. Walichukua hatua ya kukusanya kiasi cha Sh.44 Milioni, kwa kushirikiana na wadau wakampeleka mtoto Mariam nchini India, katika hospitali ya Apollo kwa ajili ya matibabu zaidi.

“Mariam ana ndoto ya kuwa daktari, lakini atafikia vipi hatua hiyo kama anasumbuliwa na maradhi hayo, tumeona tuna kila sababu ya kumsaidia apone ili arejee darasani kama watoto wengine,” alisema Teddy Qirtu, Mkurugenzi wa Masoko wa Data Vision International.

Machi 2018, Mariam alirejea nchini kutoka kwenye matibabu nchini India akiwa na tabasamu la nguvu na matumaini ya kuweza kutimiza tena ndoto yake ya kuwa daktari bingwa wa upasuaji.

Je, wewe umemfanyia nini Abigail kwenye mazingira yako. Kila mtoto ana ndoto, mpe usikivu, huisha ndoto yake, jaribu kutatua tatizo linalokwamisha ndoto yake.

Ndoto ni sababu kuu ya ‘maisha’ ndio sababu watu huhangaika kuzifikia ndoto zao, na hicho ndicho kiitwacho maisha. Kumbuka bila kuwa na ndoto binadamu anapoteza sifa za kuwa mtu anayeishi na anabaki kuwa kiumbe uliye hai.

Nakuacha na msemo wa mwandishi nguli wa Ujerumani, Johann Wolfgang von Goethe aliyeishi katikati ya Karne ya 18 hadi mwanzoni mwa Karne ya 19, “What is not started today is never finished tomorrow.”  kwa tafsiri isiyo rasmi, “ambacho hakikuanzishwa leo hakiwezi kukamilishwa kesho.”

Anza leo na ndoto ya mtoto, ili kesho ikamilike.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Februari 12, 2019
Bandari Mpya yajengwa Muleba