Na: Ghati

Mashindano ya urimbwende wa Dunia ambayo hukusanya warembo zaidi ya 100 waliopewa bendera za nchi zao kutoka kona zote za dunia kuwania taji la ‘Miss World’, yaliyofanyika pia jana jijini Sanya nchini China, ni zao la wazo la kijana mmoja aliyethubutu kuwashindanisha warembo kwenye ufukwe wa bahari, kutangaza ‘kivazi’.

Mwaka 1951, Eric Morley, kijana Muingereza aliyekuwa na umri wa miaka 33 na mtangazaji wa Televisheni, alianzisha tamasha kubwa ambalo lilijumuisha mashindano ya warimbwende, likilenga kutangaza vazi la ufukweni (bikini), ambapo warembo wote walitakiwa kuvalia mavazi hayo. Kama lilivyokuwa lengo lake, Morley aliliita shindano hilo ‘The Festival Bikini Contest’ (Tamasha la Mashindano ya Vazi la Ufukweni).

Kabla hatujaendelea na harakati zake za matamasha ya warimbwende, tumfahamu japo kidogo Eric Morley na harakati zake za maisha.

Ingawa alikuwa na uthubutu wa biashara, historia ya maisha yake ilikuwa ya majonzi, kwani alikuwa yatima wa malezi aliyewapoteza mama yake na baba yake wa kambo aliyekuwa akimlea, akiwa na umri wa miaka 11 tu.

Maisha yake yalikumbwa na changamoto nyingi katika umri mdogo hali iliyomlazimu hata kuwauzia watoto wenzake chocolate ili ayamudu maisha. Kwa ufupi alisoma kwa kuungaunga, lakini alifanikiwa kutokipoteza kipaji chake cha kutumbuiza hata alipojiunga na Jeshi na kufikia ngazi ya Kapteni.

Akiwa jeshini alijiunga na bendi na alikuwa akiwaburudisha wanajeshi wakati wa Vita ya Pili ya Dunia, huku akiendelea kuifikiria ndoto yake ya kuwa mfanyabiashara mkubwa kwenye kiwanda cha burudani. Na mwaka 1946 aliachana na kazi ya jeshi na kuanza rasmi biashara zake kuifukuzia ndoto aliyoiota miaka yote. Katika harakati zake aliwahi pia kushiriki siasa akimuunga mkono Waziri Mkuu, Margaret Thatcher.

Eric Morley, Muasisi wa mashindano ya ‘Miss World’

Turejee kwenye tamasha lake la warembo la ‘Festival Bikini Concert’;

Tamasha hilo lilipata umaarufu kutokana na kutangazwa kwa nguvu kubwa na vyombo vya habari ambavyo vililibatiza jina la ‘Miss World’. Ingawa Morley alikuwa amepanga shindano hilo kuwa maalum kwa ajili ya Uingereza tu, nguvu ya media iliyolikuza ilimfanya apanue wigo na kulifanya kuwa tamasha la kila mwaka likijumuisha washiriki kutoka nje ya Uingereza.

Hata hivyo, shindano hilo liliingia doa katika mwaka wake wa kwanza tu, baada ya picha ya mshindi wa taji hilo, Kerstin “Kiki” Hakansson, kusambaa kwenye magazeti na Televisheni zikimuonesha akiwa kwenye vazi la ufukweni (bikini).

Nchi nyingi hususan zinazofuata maadili ya kidini zililaani vikali shindano hilo. Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani (Papa) naye alitoka hadharani kulaani vikali uvaaji wa bikini kwa mshindi wa shindano hilo. Kadhalika, nchi nyingi zilitangaza kutoshiriki shindano hilo na hata kutaka lisioneshwe kupitia vyombo vya habari vya nchi hizo.

Wajuzi wa mambo wanasema ‘There is no such a thing as bad publicity’ (hakuna kitu kinachoitwa kutangazika vibaya). Msemo huo ulifanya kazi vizuri kwa Morley ambaye aliona utata wa kivazi cha ufukweni licha ya kuleta matatizo, kimelitangaza shindano hilo duniani kote, ndipo alipolisajili jina la ‘Miss World’, kama jina rasmi la biashara la mashindano hayo ambayo awali yalikuwa ‘Festival Bikini Contest’.

Katika kujaribu kubadili kulaaniwa kuwe kubarikiwa, Morley aliyafanyia kazi malalamiko na ukosoaji mkubwa wa mavazi dhidi ya shindano hilo ili aishawishi dunia nzima, ambapo mwaka 1976 vazi la ufukweni liliondolewa rasmi na kuwekwa vazi la jioni (evening gown). Hivyo, mrembo wa Sweden, Hakansson anabaki kuwa mshindi pekee aliyevishwa taji la urimbwende katika historia ya mashindano hayo akiwa amevalia bikini bila vazi lingine.

Mwaka 1959, kwa mara ya kwanza, Shirika la Habari la Uingereza (BBC) lilianza kulitangaza shindano la Miss World na matangazo hayo yalisikika kwenye vituo vingine vikubwa na vidogo.

Hatua hiyo iliongeza nguvu na kulikuza zaidi shindano hilo. Matokeo yake, katika miaka ya 1960 na miaka ya 1970, Miss World ilikuwa ikitajwa kuwa kipindi kilichoangaliwa zaidi kwenye televisheni kwa mwaka husika.

Hata hivyo, kutokana na mgongano wa tamaduni, nchi kadhaa ikiwemo Tanzania ziliyapinga mashindano hayo na kujitenga nayo kwani ziliamini hakuna cha maana zaidi ya kushindanisha uzuri wa wanawake.

Lakini, Morley na timu yake walikaa chini na kutafuta namna ya kuboresha mashindano hayo ili mataifa mengi zaidi yaingie na kupunguza ukosoaji. Hivyo, waliamua kuanzisha kauli mbiu ya ‘Beauty with Purpose’ (urembo wenye kusudi). Iliongeza vigezo vya wigo wa uelewa/ufahamu wa mshiriki na namna anavyoweza kupanga kutatua matatizo ya jamii pamoja na kuibua vipaji vya washiriki.

Alienda mbali zaidi na kuhakikisha mshindi wa taji hilo anashiriki kwa namna ya kipekee katika kuendesha kampeni kubwa zinazogusa maisha ya watu na kuwa sehemu ya msaada kwa wahitaji pamoja na mazingira ya dunia.

Mabadiliko hayo yalizaa matunda na nchi nyingi zaidi zilijiunga kwenye mashindano hayo. Tanzania pia ilifungua tena njia mwaka 1967 ikimpata mrembo wake wa kwanza anayetambulika kama Miss Tanzania, Theresa Shayo (marehemu).

Kwa bahati mbaya, mwaka 2000, Morley alifariki dunia. Mkewe Julie alibeba mikoba yake yote akiiongoza kamati ya Miss World ambayo ilianza kufanya kazi kwa kuzingatia mabadiliko ya kidunia ya Karne ya 21. Alitanua wigo zaidi, akiyapeleka mashindano hayo kwenye mabara karibu yote.

Nigeria ilimtoa mrembo wa kwanza Mwafrika Mweusi, Agbani Darego Aliyeshinda taji la Miss World 2001. Mwaka uliofuata, Nigeria ilipewa nafasi ya kuandaa mashindano hayo jijini Abuja. Mashindano hayo yalifanyika Abuja kwa sababu maalum, kujaribu kutumia ukubwa wake kupinga adhabu ya kupigwa mawe hadi kufa kwa mwanamke Amina Lawal aliyekutwa na hatia ya kuzini, kwa mujibu wa sheria kali za kidini. Mashindano hayo yalitumika kupaza sauti kumuokoa Amina dhidi ya adhabu hiyo.

Agbani Darego, Miss World wa kwanza Mwafrika Mweusi

Hivi sasa, Festival Bikini Concert iliyogeuka Miss World imesaidia kwa kiasi kikubwa kutatua matatizo ya jamii. Tangu kuanzishwa kwake, imetumia zaidi ya £250 milioni kusaidia watoto wenye mahitaji maalum.

Zaidi ya nchi 100 zinashiriki kikamilifu kwenye mashindano haya. Mwaka huu, washiriki kutoka nchi 118 walichuana nchini China, akiwemo Queen Elizabeth kutoka Tanzania.

Mrembo kutoka Mexico, Vanessa Ponce ndiye aliyefanikiwa kutwaa taji la mwaka huu, huku Afrika ikiwalishwa vizuri kwenye nafasi tano za juu na mrembo kutoka Uganda, Quiin Abenakyo.

Wazo lako linaweza kuibadili dunia, usilitunze, thubutu kama Morley unaweza kutengeneza historia itakayodumu vizazi na vizazi kama ilivyo Miss World.

Endelea kuitembelea Dar24 kwa habari za uhakika na makala.

Tumeanzisha benki ya kilimomili kutoa mitaji wa wakulima - Majaliwa
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Desemba 9, 2018