Unapoanza kusoma Makala hii, ningependa ujiulize maswali ya awali na kutafakari kwa kutumia misemo nitakayokutajia. Kwanza, Kwanini ukimya wa Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, na tetesi za kupanga mkakati wa hujuma 2020 zimeiamsha CCM? Pili, Kwanini CCM katika hili imezingatia na kufanyia kazi tuhuma zilizoibuliwa na mtu anayeitwa Syprian Msiba?

Kwenye masumbwi kuna msemo ‘it’s the punch you don’t see coming that knocks you out’ (Ni konde usiloliona ndilo litakayokumaliza). Lakini pia, kuna msemo wa kumzingatia asiyeaminika unaosema ‘Even a broken clock is right twice a day’ (hata saa mbovu huwa sahihi angalau mara mbili kwa siku).

Katika majina yaliyotajwa zaidi kwenye mitandao ya kijamii nchini ndani ya wiki hizi mbili, ni jina la aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye hata hivyo kauli yake imekuwa adimu katika kipindi cha miaka mitatu sasa.

Bernard Membe (katikati), Mama Salma Kikwete wakimsalimia mzee na mwanachama wa CCM 2015

Jina la Mwanadiplomasia huyu ambaye ni ‘kada mwandamizi’ wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), liliibuka tena baada ya kutajwa kwenye orodha ya mtu anayefahamika kama Syprian Msiba, na baadaye kutua mezani kwa Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally ambaye alizingatia tuhuma hizo na kutamka hadharani kuwa anamuita ofisini kwake ili azungumze naye.

Katika sakata hilo, Membe anatuhumiwa kupanga mikakati ya ‘kuhujumu’ uchaguzi wa ndani ya chama hicho wa nafasi ya urais, kumpata mgombea wake mwaka 2020. Tukiweka kando mjadala wa njia na utaratibu uliotumika kumuita Membe ofisini na sintofahamu ya uhalali wa aliyejibu wito wa Dkt. Bashiru kupitia Twitter, mjadala wa kona nyingine unaofukuta ni kile kinachoitwa ‘nguvu ya Membe’ ndani ya CCM.

Kwa hakika, hauwezi kupima nguvu ya mwanasiasa huyo bila kuhusisha namna ambavyo alitikisa katika mchakato wa kumpata mgombea Urais wa CCM mwaka 2015. Jina la Membe aliyeshiriki mchakato huo lilikuwa jina shindani zaidi kwa kada aliyekuwa anatajwa kuwa na nguvu kubwa  zaidi, Edward Lowassa.

Kwa ufupi, kwa kutumia maneno yaliyokuwa yanatumika zaidi wakati huo, mvutano mzito ndani ya chama hicho kwa wafuasi ulikuwa kati ya Timu Lowassa na Timu Membe. Hivyo, nguvu ya Membe kupitia wafuasi wa chama hicho, ilikuwa inaonekana dhahiri kwa kuangalia namna alivyokuwa anaweza kumtikisa Lowassa aliyekuwa anatajwa kuwa kisiki kigumu zaidi.

Hata hivyo, ni uamuzi wa busara na jicho la wazee wa chama hicho lililoangalia mbali na kukiokoa chama dhidi ya mpasuko mkubwa uliokuwa unaelekea kutokea kutokana na mvutano mzito wa makundi, hasa makundi mawili (Timu Lowassa & Timu Membe).

Kwa kutumia vigezo na utaratibu wa chama, Kamati Kuu ilifanya uamuzi wa kuyakata majina hayo mawili, na katika hali isiyotegemewa na wengi alichaguliwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ambaye hakuwahi kutajwa kujihusisha na kundi lolote na uchukuaji fomu wake ulikuwa wa kipekee na ulipewa jina la ‘kimyakimya’. Mzee wa kimyakimya alipenya katikati ya msitu na kusawazisha hali ya hewa ndani ya chama.

Kitu cha msingi kukiangalia wakati unauliza ‘iko wapi nguu ya Membe’, ni kwamba nguvu hii iliishia kusikojulikana. Wafuasi wake hawakuwa na njia mbadala na aliwasihi kuungana na chama chao kuhakikisha kinashika dola kupitia mgombea wao, Dkt. Magufuli. Alishiriki ipasavyo kumnadi Dkt. Magufuli ambaye sifa zake na kazi alizofanya kama Waziri wa Ujenzi zilikuwa dhahiri na alikubalika.

Kitendawili cha kipimo cha nguvu ya Membe kinabaki kwakuwa kitendawili cha nguvu ya Lowassa kilitenguliwa na kufahamika baada ya kuamua kuhama CCM na kuonesha misuli yake kupitia kambi ya upinzani. Lowassa alishindwa uchaguzi, lakini mzani wake ulisoma vizuri na tuliweza kupima nguvu yake haswa. Wafuasi wake wengi walihama naye, na alibakiza ‘mamluki’ wengi waliohujumu CCM na kubainika baada ya uchaguzi huo ambapo waliadhibiwa.

Lakini Membe, yeye alibaki kuwa ‘CCM damudamu’, na nguvu yake haikuwahi kupimwa kwa mchakato wa kura ya aina yoyote ndani au nje ya chama hicho katika nafasi aliyoiota. Lakini CCM wenyewe wanaweza kutupatia mtazamo kuwa kwa mvutano wa nguvu za Membe na Lowassa makundi yangeweza kukipasua chama hicho, hivyo alikuwa na nguvu kubwa ambayo hadi sasa kipimo chake ni ‘isiyojulikana’.

Je? Hivi sasa Membe ni tishio ndani ya Chama? Imedhoofishwa?

Katika kujibu maswali haya ya msingi, tukumbushane tu kuwa nguvu ya Membe na Lowassa ndani ya CCM ilishika hatamu kupitia wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama hicho Taifa na katika ngazi mbalimbali.

Katika kutafakari haya, tukumbuke kuwa Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Magufuli ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametumia miaka miwili kukifumua chama hicho hali ambayo inaaminika kuwa inalenga kudhoofisa makundi, kupunguza gharama na kuondoa watu wenye nguvu.

CCM inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli ilipunguza idadi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kutoka 388 hadi 158. Wajumbe wa Kamati kuu ni 24 badala ya 34. Panga hilo limeenda hadi ngazi ya shina.

Pia, CCM hii imewapunguza nguvu viongozi wake wa kuchaguliwa ambao hivi sasa hawapaswi kuwa na vyeo vingine vya kiutendaji. Lakini pia, hata wanachama sasa wanahakikiwa na kusajiliwa kwa njia ya kielekroniki ili kudhibiti uhalali wao.

Lakini pia, kwa mujibu wa Dkt. Bashiru mchakato wa kuwapata wagombea wake umeongezewa lenzi ya kuwatazama na chujio la kuwachuja limeongezwa nyavu ndogo ili watakaopita wasipite kwa nguvu ya pesa, makundi, hujuma au fitna.

Lakini pia, Dkt. Bashiru ametuaminisha zaidi kuwa CCM ya sasa, wale waliokuwa wanaitwa vigogo na wenye nguvu hawapo tena, wanachama wote wana haki sawa na wanalingana isipokuwa historia yao tu ndani ya chama hicho.

“Mimi nimemtaja Membe kama mwana CCM. Kwa sababu hana nguvu kuliko CCM. Hana tofauti kabisa na hawa wanachama walioingia leo. Lakini tofauti yake amewahi kuwa Waziri, Mbunge na kiongozi wa chama ambaye kwa wanayosemwa mtaani kuhusu yeye ningehitaji kukutana naye tukazungumza,” alisema Dkt. Bashiru.

Aidha, kinachoonekana dhahiri kuwa ni kitendawili kizito kinachomuweka Membe kwenye mabano dhidi ya CCM ya sasa, ni kile nilichoeleza kuwa nguvu yake na uwepo wake ndani ya chama hicho ‘kutojulikana’, kwani hashiriki shughuli za chama lakini bado anakumbukwa kwa alama za miguu yake ndani ya chama hicho hasa mwaka 2015 na zinatakiwa kuzingatiwa.

“Ndugu Membe sikuwahi kupata simu yake, wala mchango wake, wala mawazo yake. Hata anapoenda Lindi anakotoka na alipokuwa mbunge, nimekaa pale siku tatu naomba kura sikumuona. Nikasema yuko wapi na namsikia wanamzungumza hivi na vile…. aje tuzungumze,” alisema Dkt. Bashiru.

Je, kwanini kinachosemwa ‘mitaani’ kuwa anapanga kuingilia mchakato wa 2020 ndani ya chama hicho yanapaswa kuchukuliwa kwa umakini na kufanyiwa kazi kwa nguvu zote.

Hakuna mwenye jibu sahihi zaidi ya kudhani… na mimi nadhani ni kwa sababu ‘ana nguvu isiyojulikana na ukimya unaotiliwa shaka’. CCM wanahakikisha hakuna konde litakalokuja bila kuliona, kwa sababu, “it’s the punch you don’t see coming that knocks you out’.

Joto kuongezeka Dar hadi Januari
Modric avunja ufalme wa Messi na Ronald Ballon d'Or