Na Ghati:

Hakujua alichokuwa nacho, alikitumia siku zote kuchungia ng’ombe na kondoo. Alipopewa jukumu la kuwatoa Waisrael Misri, alikuwa mnyonge, alijiuliza angeweza vipi mbele ya Farao? Alitegemea Mungu angemletea silaha za kumsaidia, lakini aliambiwa fimbo aliyokuwa nayo siku zote ndiyo jibu la yote, na kweli ilianza kumshangaza.

Ni fimbo ileile iliyomeza nyoka wa wachawi wa Farao, ikapasua bahari kuwavusha Waisrael na kuwameza wanajeshi wa Farao, ikapasua mwamba na kutoa maji jangwani. Lakini baadhi ya Waisrael wale walioneemeka na matokeo ya fimbo ile, wakala wakashiba vizuri na kunywa maji yatokanayo na kazi ya fimbo ile, walipopata nguvu nyingi wakampiga mawe mmiliki wa ile fimbo, Musa.

Wakapata akili, wakajua kuhoji. Iweje umbali kati ya Misri na Kanaan, Km 8482 watumie miaka 40? Walimlaumu Musa. Nadhani walijua anafaidika na mwendo ule wa mzunguko… wakamtukana sana, wakasahau ile shortcut ya bahari kupasuka kwa kutumia pigo moja la fimbo.

Wakawa wajanja… si wameshashiba! Shibe ikawalevya, wakafanikiwa kutengeneza fimbo zao nyingi, na wao sasa wanaweza. wakachonga hadi miungu yao, wakaiabudu. Lakini mwisho walianguka tena vibaya, wakaikumbuka fimbo ile… “Musa tuokoe.” Musa aliyeishika fimbo ile, hakuchoka. Aliitumia tena fimbo ile kuwaongoza kwenda Kanaan.

Utanisamehe kama hautaunganisha vipande vya picha kuipata picha kamili. Simulizi hili la fimbo ya Musa na Waisrael lilinijia ghafla nilipokuwa namsikiliza Mbaki Mutahaba, mdogo wake Ruge Mutahaba ambaye ni Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, alipokuwa akiwaomba Watanzania kuchangia matibabu ya kaka yake. Ruge anahitaji shilingi milioni 5 kila siku kwa ajili ya matibabu nchini Afrika Kusini. Hadi sasa matibabu yake yameshatumia Sh. 650 Milioni.

Tunahimizwa kunyoosha mkono kusaidia kurejesha afya ya Ruge nitakayemuelezea hapa kama ‘fimbo ya muujiza wa muziki wa kizazi kipya’, kwa kutuma fedha kupitia namba 0752-222210 jina ni Kemilembe Mutahaba.

Sentensi nzito iliyobeba zaidi usikivu wangu, aliyoisema Mbaki  ni, “Ruge ni Mali ya Watanzania.”

Ni kweli. Ndio sababu leo, Mkurugenzi Mtendaji wa E-FM na E-TV, Francis Ciza maarufu kama Majizo ambaye wengine walidhani ni hasimu wake, amechukua jukumu la kuunda kamati ya kuchangia matibabu ya Ruge.

Majizo anajua Ruge ni ile Fimbo tuliyokuwa nayo hatukuijua hadi hapo ilipoanza kutenda tulipohitaji kuvuka. Ni DJ wa muda mrefu, anajua muziki wa kizazi kipya na mchango wa Ruge, wamewahi kufanya biashara ya kukodishiana jukwaa la kisasa kwa ajili ya tamasha la Fiesta na matamasha mengine.

“Lengo ni kuhakikisha Ruge anarudi mtaani kwani game bila yeye linakuwa halina ushindani,” alisema Majizo.

‘Game’ linakosa ushindani, ile ‘fimbo ya kuonesha njia’ ya muziki wa kizazi kipya nchini iliyotumika kwa takribani miaka 20 sasa inatuhitaji sisi. Majizo amethibitisha hilo pia.

Majizo amekumbuka mwaka 2015, Ruge aliweka kando ushindani na akampa mbinu ya kutengeneza pesa wakati wa kampeni.

“Katika kampeni ya 2015, alinieleza kuwepo kwa fursa, akanishika mkono kunielekeza namna ya kuingia huko. Nashukuru Mungu nilifanikisha, hali ambayo kwa watu wengine ambao wana ushindani wa kibiashara ni ngumu kulifanya hilo.

Fimbo hii ilituneemesha kwa kipato, tukaajiriwa wengi kwenye muziki, ikatusaidia kuuvusha muziki wetu bahari ya Hindi hadi ughaibuni. Ikasaidia kuifanya sanaa kuwa kazi ya kutengeneza vijana matajiri badala ya kuwa ngazi ya kutengeneza masikini wenye majina makubwa.

Ikawavusha wale tuliokuwa tunawaona kwenye runinga, ikawaleta kwetu na kusaidia kuwaunganisha na wa kwetu. Tukawaona wa kawaida na wao wakatuona mali, leo tunashindana nao kwenye tuzo za kimataifa na mara kadhaa tunawapiga mitama.

Leo sio ajabu tena kumuoa Rick Ross aliyekuwa na Jay Z akiwa na Mswahili yeyote wa Pwani ya Tanzania kisa ni msanii. Tunaendesha magari na kumiliki majumba. Ni tofauti na zamani tulikuwa tunajivunia kumiliki wachumba na ‘pamba kali’. Lakini Je, tunaikumbuka fimbo iliyotuvusha?

Ukweli ni kwamba ingawa anatajwa kuwa mbunifu na wengine wakimpa majina kama ‘Akili Kubwa’, ‘Mzee wa Fursa’, ‘Master Mind’; Ruge hakuanzisha Bongo Fleva. Lakini ndiye muhuishaji mkubwa wa biashara ya Bongo Fleva.

Kwa bahati mbaya amewahi kushambuliwa na wengi ambao ni wafanyabiashara ya muziki huo wakimtuhumu kwa mengi ya kibiashara. Lakini ukweli unabaki palepale kuwa alichonga barabara, aliona mbali na hakutaka kuwapitisha njia ya mkato kuingia Kanaan, aliamini njia ndefu ndio jibu la kudumu.

Kwa faida ya wengi, hasa waliozaliwa miaka ya 1990 na kuendelea, ambao hivi sasa kiuhalisia ni watu wazima lakini hawakushuhudia harakati za awali za Bongo Fleva… awali muziki haukuwa biashara ya kutegemea hata kidogo. Master J, mtayarishaji mkongwe amewahi kukumbushia mara kadhaa kuwa kiasi kikubwa cha fedha alichowahi kulipwa enzi hizo ni Sh. 50,000 ya kurekodi albam nzima ya Joseph ‘Sugu’ Mbilinyi.

Kwa kuzingatia pia juhudi za wadau wengine, Ruge akiwa na Bosi wake Joseph Kusaga ndio waliowekeza zaidi rasilimali zao kuhakikisha Bongo Fleva inakuwa biashara kubwa. Walianzisha tamasha la Summer Jam lililowakutanisha wasanii wengi na umati mkubwa wa watu ufukweni, wakalipwa elfu kadhaa na safari ikaanza.

Miaka 15 iliyopita, walianzisha tamasha la Fiesta baada ya kuongezeka kwa wasanii na kutumia redio yao, Clouds FM kuongeza nguvu ya kutengeneza mastaa.

Watayarishaji nguli wa muziki, P-Funk Majani, Master J, Ludigo walizipika hits kibao na Clouds FM ya Ruge na Kusaga ilizipa nafasi kubwa kuwafanya wasanii hao kuwa mastaa. Ilikuwa ngoma yako ikisikika Clouds Fm baasi ‘umeshatoka’. Foleni ya nyimbo za wasanii ikawa kubwa, na lawama nazo zikaunga tela.

Miaka michache baadaye, tulianza kuona watayarishaji na wasanii wakiwa na nguvu za kufanya ziara ya utambulisho wa albam zao na walijaza nyomi kwelikweli. Mtakumbuka uzinduzi wa albam ya Juma Nature ‘Ugali’ ilivyopigwa promo na Clouds Fm na kutikisa. Vipi kuhusu albam ya ‘Nitakufaje’ ya King Crazy G.K? Ilikuwa kila kinachopeperushwa na Clouds FM kinapepea kweli na kuwa dhahabu. Albam kibao zikaingia sokoni, na watu wakapiga mpunga taratibu. Yalizaliwa majina mengi makubwa, ingawa hivi sasa nasikia wengine hawataki hata kuitwa ‘legends (wakongwe)’. Ukweli ni kwamba wakongwe wengi wakikumbuka walikotoka, jina la Ruge halikosi kwenye simulizi lao.

Ruge akathubutu tena, kupitia Fiesta, akavunja mipaka na kuanza kuwaleta wasanii wakubwa kutoka Marekani. Mara paap! Buster Rhymes, Shaggy, T.I, EVE, Brick and Lace, Fat Joe na wengine kibao. Akaingia pia Afrika, akaanza kuwaleta P-Square, J-Martins, Blacket na wengine.

Ingawa wasanii tulifaidika, bado tuliamini yeye anapata zaidi. Tulianza kumuita majina ya unyonyaji, zikaanzishwa harakati. Tukaanza kumkosoa kwa kuleta ‘wasanii wa nje’ na kuwalipa mamilioni huku akiwalipa wa ndani laki kadhaa. Lakini hakuacha, aliendelea kwa miaka kadhaa. Kumbe alikuwa anaendelea kuchonga barabara na alijua mwishoni tutamuelewa. Alituletea shule na fursa nyumbani. Wasanii wetu wakajifunza mengi kwa kupanda jukwaa moja na Wamarekani wale.

Miaka michache baadaye, wasanii aliokuwa anawaleta wakaanza kufanya kazi na wasanii wa ndani. Tukaanza kuona AY feat. P – Square, Ommy Dimpoz feat. J Martins, orodha ikawa ndefu hadi mwaka 2014 alipomleta Davido kwa ajili ya Fiesta. Diamond Platinumz akaitumia hiyo kama fursa na akampa shavu Davido, ikapikwa ‘Number One Remix’ iliyomfungulia dunia na kufungua milango ya kimataifa, Diamond akawa mkubwa na sasa anatuwakilisha kimataifa. Zikaanza kufanyika collabo hadi za Wamarekani. Leo sio jambo la ajabu tena tukisikia Joh Makini Feat. Fat Joe.

Diamond na Davido, kwenye jukwaa la Fiesta Dar es Salaam

Akaona Bongo Fleva imekuwa kubwa aliyoitaka, hakuna haja tena ya kuwaleta wale wa ughaibuni, sasa anagawanya mamilioni yale kwa wasanii wa ndani. Fiesta ikawa na 100% wasanii wa ndani, wakalipwa mamilioni. Wengine wakiimaliza Fiesta kama wamepita mikoa yote wananunua magari. Ikaitwa sikuu ya Taifa ya Wasanii. Lakini wakulalama nao hatukukosa, bado mamilioni tuliendelea kusema, “hayatoshi, yeye anapata zaidi!”. Binadamu sisi hatuna kingi cha kutosha!

Jukwaa la Fiesta likawa jukwaa kubwa zaidi Afrika Mashariki lakini lina wasanii wa ndani pekee. Zaidi ya watu 60,000 walikusanyika Dar es Salaam kuwashuhudia wasanii wao. Idadi hiyo inakaribia idadi ya mashabiki wanaofulika Wembley Stadium nchini Uingereza kuangalia soka au pambano la Anthony Joshua.

Hakuishia hapo, alihakikisha ubora, akawahangaikia wasanii kuhakikisha wanaimba ‘Live’ na bendi. Walikosea mara kadhaa na hakuacha.

Kuna rafiki yangu aliyewahi kuwa kwenye kamati ya Fiesta alisema Ruge aliwahi kulalamikiwa na uongozi wa Clouds Media Group kwa kuhangaika na Live Band inayotumia ‘mahela’ mengi, lakini hakukoma, alisema ipo siku wataelewa. Leo wasanii wa Bongo wanafunika huko nje kwa ‘Live Band’, wamezoa uzoefu kwenye Fiesta.

Waliokuwa wanadhani Ruge anavuna sana kwenye Fiesta kwa kipindi cha miaka yote 15, walipata mshangao Novemba mwaka jana, baada ya mmiliki wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga kueleza kuwa hawapati faida kabisa kwenye Fiesta, ni kutoa fursa na jukwaa kwa wasanii.

Kukosekana kwa Ruge kwenye Fiesta ya mwaka jana kuliwafanya wengi kumkumbuka. Waliona pengo lake kwenye mengi. “Angekuwepo Ruge tunaamini haya yasingekuwa hivi,” wasanii, mashabiki na watangazaji walisema kwa nyakati tofauti ilipotokea changamoto.

Makala hii inaweza kuwa na kurasa laki moja kama tutapitia mchango wa Ruge kwenye muziki tu tena kwa ufupi. Bado hatujamgusia kwa kuwa ‘mzee wa fursa’, aliyefanya mengi pia kwenye mambo ya kijamii. Si mnakumbuka kampeni za ‘Malaria haikubaliki’, ‘Fursa’, ‘Malkia wa Nguvu’, ‘Kipepeo’, ‘Sambaza Upendo’, ‘Mimi na Wewe’. Kila mmoja nchini aliguswa na kimojawapo. Hata viongozi wa Serikali wanafahamu hilo.

Wasanii wengi wakubwa leo wanakiri kuwa bila Ruge wasingekuwepo. Ali Kiba ni mmoja wao, anasema, “bila Ruge leo nisingekuwa hapa.” Najua wasanii wengi pia wanasema hivyohivyo hata kimoyomoyo. Roma Mkatoliki yeye anasema Ruge alikuwa anampigia simu usiku na kumtaka afike studio warekodi wimbo.

Wengine walidhani Ruge alijikita zaidi kwenye mradi wake wa Nyumba ya Wasanii Tanzania (THT), lakini hata wa nje aliwaona na kuwashika mkono. THT imezaa mastaa wengi, ila Clouds FM imezaa mastaa wote wa muziki.

Pamoja na kujitoa hivi, hakuwa anajigamba kwenye mitandao kama sisi wengine. Ruge hayuko Instagram, hapost kazi kubwa anayoifanya. Anasubiri ionekane dhahiri na ndio furaha yake.

Wasanii karibu wote wanamuita ‘Bosi Ruge’, wengine wanamuita ‘Baba’, ‘Mshauri’, ‘Mwamba uliopitia mengi bila kutikisika’. Sijawazungumzia watangazaji na wengine. Tena watangazaji hadi wa redio nyingine tofauti na Clouds FM/TV.

“Ruge ananipa michongo mingi sana, naomba tumheshimu katika kazi yetu,” aliwahi kuniambia mtangazaji wa EATV niliyekuwa namfanyia kazi fulani mwaka 2013.

Ana mapungufu yake kama binadamu, lakini kwenye jamii hasa sekta ya muziki nchini, anatumika kama ile ‘fimbo ya Musa’. Amebadili mchezo, sasa hivi muziki sio tu ajira, ni biashara kubwa.

Ametutumikia, ameivusha Bongo Fleva, ametupatia ujanja wa kutengeneza pesa kupitia fursa, amewatetea wasichana kupitia ‘kipepeo’, amewajali wanawake na kuwatuza kupitia ‘Malkia wa Nguvu’, amehimiza uzalendo kwa kutunga nyimbo za kizalendo. Kwa ufupi ametufungulia dunia kuwa tunachotaka.

Leo yuko kitandani baada ya kulitumikia taifa. Tumuombee na tumchangie fedha za matibabu kwa moyo mkunjufu, Mungu atatubariki mara dufu. Kumbuka “Ruge ni Mali ya Watanzania.”

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Februari 21, 2019
Video: Bavicha wazungumzia kesi ya Mbowe