Na Josefly

Karibu kwenye ukurasa huu ambao kila Alhamisi tutakuwa tukikumbushana kuhusu yaliyotokea kwenye muziki ndani na nje ya Tanzania, tukiyafukua kujua uhalisia wake. TBT (Throwback Thursday). Ni alhamisi ya kukumbuka yaliyopita yakaacha alama na kuyadadavua. Wahenga husema, “kama hujui unakotoka, hujui unakokwenda!”

Leo tunaangazia shindano la Mkali/Mfalme wa Rhymes.

Mwanzoni mwa miaka ya 2000, Bongo Fleva ilikuwa juu kileleni huku mtindo wa kufokafoka (hiphop/rap) ukiuacha kwa mbali ule wa kuimba. Tofauti na sasa, wakati huo uandishi bora wa mashairi ulikuwa kigezo muhimu zaidi.

Msanii alipimwa kwa uandishi na uwasilishaji huku watayarishaji nguli, P-Funk Majani, Master J, Ludigo, Enrique na Mika Mwamba wakiifanya kazi yao kama ‘Komando’ aliyeahidiwa pepo endapo atashinda vita.

Wasanii walifanya kazi kubwa ya kuandika na kuwasilisha kwa namna ya kipekee, ilikuwa kila unachokisikia redioni ni kizito. Walipigana vikumbo kwa uandishi na upekee wa mada zao zilizoelimisha na kuburudisha.

Baada ya kuibuka mafahari wengi ndani ya zizi la Bongo Fleva, mwaka 2004, mdau mkubwa wa muziki huo, Erick Shigongo mmiliki wa kampuni ya Global Publishers, iliyokuwa ikiongoza kwa kuuza magazeti pendwa, wakati huo yakiitwa ya ‘ya udaku’, alijitokeza na kudhamini pambano la mafahari hao ili kumpata fahari mmoja ambaye angevikwa taji la Ufalme/Ukali wa Rhymes.

Shigongo, alithubutu… akaweka zawadi ya gari kwa mshindi wa kwanza, Mfalme wa Rhymes. Enzi hizo wasanii wanaoendesha hata Vitz walikuwa wa kuhesabu.

Mchakato ulianzia kwenye magazeti, wakati huo hakuna mitandao ya kijamii wala simu janja. Vituo vya redio navyo vilikuwa vya kuhesabu. Basi bwana, ilibidi ununue gazeti la Kiu, Ijumaa au Uwazi ili kumpigia kura msanii umpendaye awe kati ya wasanii kumi watakaochuana jukwaani kumpata mkali wa Rhymes.

Mwitiko ulikuwa mkubwa sana, watu walipiga kura na hatimaye Global Publishers wakaanika majina ya waliopendekezwa.

Miongoni mwao ni Solo Thang, Jay Mo (Mvua na Jua), Mandojo na Domo Kaya (Nikupe Nini), Profesa Jay (Usinitenge), Inspector Haroun(Bye Bye), Afande Sele, Soggy Dogg Hunter (sasa Chief Rumanyika), Madee, Dully Sykes.

Nakumbuka ndio wakati huo Mr. Blue anatamba na ‘Blue-Blue’ mara ‘Mapozi’ na alikuwa juu. Lakini umri ulimuangusha. Bwana mdogo hata sheria ya nchi ilimtaka awe nyumbani anajisomea usiku huo na sio jukwaani kwenye ukumbi wa starehe. Aliumia sana, alitamani angepigana vikumbo na baba/kaka zake.

Mdhamini akawaweka kambini, kazi ikaanza. Wakapikwa na kupewa semina kadhaa huku wakitamba kila mmoja kuwa atakuwa mshindi. Nadhani suala la ujumbe lilikaziwa sana kwani nyimbo zao zilijieleza siku ya shindano.

Mdhamini alivyoanza kupoteza uaminifu

Washiriki wa shindano hilo walianza kupata wasiwasi hasa kwa kuzingatia kuwa siku chache zilizopita, Global Publishers kupitia gazeti lao moja pendwa (la udaku) waliandika makala ‘konki’ kuhusu wimbo wa Afande Sele uliokuwa kileleni wakati huo, ‘Darubini Kali. Wimbo alioimba kwa kupokezana na Dogo Ditto. Mashairi yake yaliandikwa kwenye ukurusa wa kati wa gazeti na kudadavuliwa kwa sifa tele. Kwa uhalisia wimbo huo sio tu ulikuwa mkali, hadi leo ni mkali. Afande Sele, Dogo Ditto na P-Funk Majani walijifungia kwelikweli.

“Afande anasema wote… wote kimya, nitakayonena hapo yatamgusa mwenye hekima. Hapo… hapo ulipo, kama waipenda pepo kwanini unaogopa kifo!?” Heeh unachekesha, haa.. unanipa raha, unafikiri Mbinguni utakwenda kwa motokaa eeh, au utapata zali kama Yesu alivyopaa…Acha kujidanganya kwa Mungu sio kwa mzungu…”

Wimbo ulishika, watu wengi waliukariri, jinsi Afande Sele na Ditto walivyopokezana ilikuwa noma kweli. Kila mstari ulikuwa na ukubwa wake. Afande anaandika kwelikweli.

Hatua hii iliibua ukosoaji wa awali, wengi wakaanza kutabiri kuwa Afande ana nafasi zaidi ya kubeba ukali wa Rhymes. Stori kutoka ndani ya kambi zikaeleza kuwa Soggy Doggy Hunter amekomaa anamtaja Afande Sele kuwa ndiye aliyepangwa.

Vituko navyo havikukosa, ushilawadu haukuanza leo… zikasambaa tetesi kuwa eti kwenye kambi watu wanarogana, eti kuna watu wanshikwa matumbo ya kuhara. Huenda ilikuwa ‘stress’ tu za kuiwaza zawadi ya gari mbele ya vichwa vyote vikali! Waswahili hatuwezi kuuacha uswahili!

Dully Sykes ambaye alikuwa miongoni mwa washiriki, alijitoa siku chache kabla ya siku ya pambano.

Siku ya Shindano

Hayawihayawi, yakawa… siku ile, Juni 27, 2004 iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu ikatimia. Kengele ikalia. Kama ingekuwa masumbwi tungesikia “ladies and getlemen, the wait is over. Let’s get ready to rumble..!”

Ukumbi ulifurika, wadau wa muziki kutoa Morogoro ndio waliotisha zaidi, walikodi magari wakaingia Dar es Salaam kwa fujo. Wakaijaza Dar wakidai, “tumefuata gari letu.”

Wengine waliotisha zaidi ni wakaazi wa Temeke. Enzi hizo kuna wafalme wawili Temeke, Juma Nature na Inspector Haroun. Mikoroshini yote wakaamka nao wakadai “wamefuata gari lao”.

Baadhi ya nyimbo zilizosikika ni Profesa Jay na ‘Msinitenge’, alipanda na Q-Chief, Mandojo na Domo Kaya ‘Nikupe Nini’, Jay Mo ‘Mvua na Jua’, Soggy Dogg na ‘Kulwa na Dotto’, Afande Sele ‘Mtazamo na Darubini Kali’. Yaani kila mmoja alitupa kombora kali na kwa mtindo wa kipekee. Asikwambie mtu, Morogoro na Temeke shangwe lao limeandikwa kwenye vitabu ‘Vitukutu vya Bongo Fleva’.

Mchujo umempata mshindi

Baada ya majaji kufanya mchakato mgumu, mwisho ilibidi tu mshindi awe mmoja. Mbele ya jukwaa walisimama wanaume wawili, Afande Sele wa Morogoro na Inspector Haroun wa Temeke. Wengine wote walikatwa.

“Na.. mshindi ni…. Afande Sele.” Ilisikika sauti ya mamlaka ya kumtangaza mshindi, ikisindikizwa mdundo wa ‘Darubini Kali’. Wacha…! Ukumbi uliripuka, Morogoro kweli wakafanikiwa kuondoka na gari lao. Selemani Msindi akavikwa taji la Ufalme, akakumbuka enzi za Mfalme Suleimani, akajiita kuwa ni Suleimani wa Pili.

Ni ngoma tatu zilizompa ushindi, ‘Mtazamo, Mayowe na Darubini Kali’. Kweli ukizisikia hata leo utamuelewa Afande kuwa ni mwandishi nguli wa vitabu aliyeamua kuviimba vitabu vyake badala ya kuviandika.

Kesho yake wanaume walianza safari kurejea Morogoro na zawadi yao ya gari, Dogo Ditto na Afande Sele wakiwa na kundi la Watu Pori walikuwa wanawapungia tu mikono mashabiki. Unaambiwa Morogoro Road (barabara ya Morogoro) ilifurika. Mapokezi ya Afande Sele Morogoro haikuwahi na haijawahi kutokea hadi leo kwa msanii. Nadhani hii kumbukumbu ndio iliyomfanya Afande mwaka 2015 ajaribu kugombea ubunge. Jamaa alipokelewa kifalme kwelikweli.

Baada ya hapo, Afande Sele alifanya ziara kubwa kuwahi kutokea akiwa na Dogo Ditto na wenzake. Kila ukumbi aliokanyaga mikoani ulifurika.

Washiriki waponda matokeo, waapa

‘Mkali wa Rhymes’, yalikuwa mashindano yalipondwa na kulaaniwa zaidi katika historia ya Bongo Fleva. Nadhani hata kuliko laana iliyowahi kutupiwa Kili Music Awards kwa kipindi chote. Washiriki walidai kuwa mshindi alipangwa tangu zamani na kwamba walimuandalia mazingira ya ushindi mapema.

Solo Thang yeye alienda mbali, aliumizwa sana na matokeo, aliamini ameonewa sana. Hakuwa na pa kusemea sana, si magazeti yote pendwa yanamilikiwa na mdhamini (Global Publishers). Solo Thang akaingia studio, akaachia wimbo mzima kueleza kilio chake. Akaubatiza jina la ‘Kilio Changu’ akimshirikisha Q-Chief.

Kwenye wimbo huo aliapa kutoshiriki tena mashindano hayo.

“…. Wengine wananirubuni eti nashindania gari, kumbe wameshapanga wampe nani toka awali. Sitarudia kosa hata zawadi waweke meli/ waongeze ghorofa mbili wanikabidhi na sheli.”  Anasikika Solo kwenye wimbo huo.

Ukosoaji kama huo ulizidi kupata umaarufu, hata Fid Q kwenye wimbo wake wa ‘Mwanza-Mwanza’ anasikika arap:

“Sio kama…. na Afande Sele wa Moro, Mkali wa Rhymes ambaye Soggy Doggy hamtaki/ anamuita Kobe hawezi mzidi mbio Farasi.”

Kutoka kaskazini, Joh Makini naye alilianika sakata hilo kwa namna yake kwenye wimbo wake ‘Hao’. Joh anasikika akirap:

“kila kitu ni dili kama u-kill wa rhymes.”

Kwa wachambuzi tunasema alimaanisha ‘ukali wa rhymes ulikuwa u-kill wa rhymes (uuaji wa ushairi).’

Mwaka uliofuata, Global Publishers walijaribu tena kuandaa shindano hilo, lakini kutokana na yaliyojili mwaka uliopita, walishindwa hata kupiga hatua. Wakati huo, wengi waliamini kama kweli yangefanyika basi huenda angeshinda Ngosha, ‘Fid Q’.

Ngosha mwenyewe aliamua kutumia tetesi hizo kukamilisha wimbo wake wa ‘Mwanza-Mwanza’ akirap, “washanitabiri mimi ndiye Mfalme nayefuata baada ya Selemani.”

Yote kwa yote, hadi leo Afande Sele anabaki kuwa juu kileleni. Ni yeye pekee ndiye mwenye taji rasmi la Ufalme wa Rhymes Tanzania. Utake usitake, iko hivyo kwenye historia!

Afande anasema hajaona wa kumpa Ufalme wa Rhymes kwani tabia za wasanii waliopo wengi haziendani na sifa za kuwa wafalme achilia mbali uwezo wao wa mashairi.

Kwenye ‘Karata Dume’ aliyomshirikisha Mez B, anarap:

“Simtazami mwingine wa kumpa mkuki na sime/ hata nikimtazama simsemi hadi nimpime/ anaweza kurithi Ufalme?/ Au anataka ujiko aonekane ndio kidume/ Kisha akamate mshiko wake za watu wamkome/ kinyume na mimi Mfalme Selemani wa Pili aliyetunga Darubini Kali..”

Shindano kama hilo likitokea katika karne hii ya simu janja itakuwaje? Nani atakuwa Simba ndani ya pori la Bongo Fleva?

Tukutane tena Alhamisi ya wiki ijayo kwa ajili ya kuangalia yaliyojiri enzi hizo kwenye muziki wa Bongo Fleva na nje ya mipaka ya +255.

Karibu pia kwa maoni na ushauri.

Je unatafuta ajira?, Hizi hapa nafasi 10 za ajira kwa ajili yako
Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria ajiuzulu

Comments

comments