Moshi mweupe wa amani ulioanza kutanda kwenye Rasi ya Korea hivi karibuni kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini, tena kwa kasi mpya na ari mpya unaanza kubadili rangi. Mkutano wa kihistoria kati ya rais wa Marekani, Donald Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un uliopangwa Juni 12 uko hatarini kuahirishwa baada ya Korea Kaskazini kudai ‘imeshtukia ujanja’ wa Marekani.

Marekani imekuwa ikiichezea Korea Kaskazini mchezo wa ‘ndege mjanja na tundu bovu’ baada ya kupoza chungu cha maneno ya moto dhidi ya Kim Jong-un ambaye anakiuka sheria za Umoja wa Mataifa na kuhatarisha amani ya dunia kwa kutengeneza makombora ya nyuklia tena yanayofika katika kona zote duniani ikiwa ni pamoja na maeneo kadhaa ya Marekani.

Kutoka kumuita “kijana mdogo anayemiliki roketi, ambaye anafanya misheni ya kujiua (Little rocket man in a suicide mission)”, hadi kumsifu kwa kumuita “mheshimiwa”. Ni hatua nzuri ya Trump iliyozua gumzo la mabadiliko ya haraka.

Mabadiliko haya, ambayo yalienda sambamba na mabadiliko ya haraka ya jinsi vyombo vya habari vilivyoanza kuripoti habari za Kim Jong-un kwa mtazamo chanya, yalitokana na hatua ambazo kiongozi huyo wa Korea Kaskazini alizichukua hivi karibuni.

Kwanza, kukutana na Rais wa Korea Kusini, mkutano wa kihistoria uliowasha matumaini ya amani ya kudumu katika eneo hilo. Pili, kuweka nia ya kukutana na Rais Trump ambayo alianza kuifanyia utekelezaji wa haraka kwa kuwaachia wafungwa watatu, raia wa Marekani waliokuwa wanafanya kazi nchini humo na baadaye kutuhumiwa kuhujumu usalama.

Wafungwa hao watatu walikabidhiwa kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Maarekani, Mike Pompeo bila kutarajia, alipokutana na Kim Jong-un. Trump alisifu sana hatua hiyo.

Hatua ya pili nzito iliyotangazwa hasa na vyombo vya bahari vya Magharibi zaidi ni ile ya Korea Kaskazini kutangaza kuwa ‘itaharibu maeneo yake yote ya vinu na majaribio ya silaha za nyuklia kati ya Mei 23 na 25 mwaka huu, tena mbele ya waangalizi wa kimataifa. Yaani wiki mbili kabla ya mkutano wa viongozi hao.

Eneo la majaribio ya silaha za kinyuklia la Korea Kaskazini

Swali kubwa linalofikirisha kwa hali ya kawaida, hivi Korea Kaskazini imeamua kuzaliwa upya kirahisi? Yaani imeamua kuharibu silaha ilizotumia gharama kubwa kuziunda kwa miaka mingi na kirahisi, tena hata kabla ya kufanya makubaliano yoyote na Marekani. Kwahiyo, wanaharibu kila kitu bila masharti yoyote!? Wenye sikio na jicho la tatu walianza kuona kuna jambo limejificha kwenye mtego wa mwenye akili ili anase kwenye ‘tundu bovu’.

Kutereza kwa ulimi wa mshauri mkuu wa Trump katika masuala ya usalama wa taifa, John Bolton alipokuwa kwenye kipindi kimoja aina ya ‘talk show’ kulizua jambo. Ulimi ulimtereza alipofananisha hatua ya Korea Kaskazini kuachana na mpango wa nyuklia na hatma ya Libya, bila kujali kuwa nchi hiyo pia inafuatilia kwa karibu kila neno la kiongozi wa Marekani.

Ni kauli za Bolton na Pompeo zilizowakasirisha Korea Kaskazini, na kuanza sio tu kutishia kuahirisha mkutano wa Trump na Kim Jong-un lakini pia kuanza kuanika ukweli wa mchakato unaoendelea.

Ukweli ni kwamba, tafsiri ya Marekani na jinsi inavyotangaza kuhusu mpango wa Korea Kaskazini kuharibu vinu na maeneo ya nyuklia bila masharti, iko tofauti kabisa. Pyongyang wana masharti yao ambayo wanataka Marekani iyaafiki pia, yaliyolenga kujilinda kiusalama huku ikijiimarisha kiuchumi kwa kuondolewa vikwazo vyote.

Go Myong-Hyun wa Chuo cha Asan, ameandika kuwa moja kati ya masharti ya Korea ambayo hayatangazwi na vyombo vya habari hasa vya Magharibi, ni kuondoa silaha za kinyuklia zote kwa pande zote katika eneo lote la Rasi ya Korea, Marekani kuondoa mwamvuli wa nyuklia iliyokuwa inautumia kulinda eneo la Rasi ya Korea.

Sharti jingine ni kuitaka Marekani kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya vikosi vyake vilivyoko Korea Kusini. Masharti haya kwa Marekani yana changamoto nzito, na ni kama mtego wa ndege mjanja pia.

“Korea Kaskazini hawajasema kuhawataachana na mpango wa silaha za nyuklia. Wanachosema ni kwamba ‘hatutafanya hivyo kama [Marekani] utaendelea kutunyooshea bunduki kichwani’. Hawataachana na mpango huu bila kupata kitu. Wanasema kwa hatua hii ‘tunatakiwa kufanya jambo, na ninyi [Marekani na Korea Kusini] mfanye jambo,” Profesa wa Chuo Kikuu cha Yonsei, John Delury anakaririwa.

Korea Kaskazini wanaamini sasa Trump anataka kuhakikisha anauchukulia mkutano huu kama ajenda inayomuinua kisiasa pia. Hivyo, imetishia kuwa itaachana kabisa na mpango wake endapo Marekani itaendelea kutoa kauli tata.

Wote, Korea Kaskazini na Marekani wanahitaji kukaa mezani, kinachowachanganya ni huo mtego wa ndege mjanja, kila mmoja anamshtukia mwenzake.

Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un alipokutana na Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in

Korea Kaskazini inataka dunia ifahamu kuwa inakaa kwenye meza ya mazungumzo ikiwa kama taifa lenye nguvu na sio kama mnyonge aliyejisalimisha. Imefanya mambo mengi mazuri ya kutengeneza njia nzuri ya makubaliano ikiwa ni pamoja na Kim Jung-un kukutana na Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in na kusaini makubalino ya awali.

Kauli tata za Marekani zinaifanya ikae chonjo. Inafahamu ingawa inahitaji sana kuwa sehemu ya dunia salama na kukuza uchumi wake, inaogopa kukosea isinase kwenye tundu bovu.

Marekani pia inahitaji mkutano huo ili kuondokana na mgogoro huo ibaki inaimulika Iran ambayo nayo imekuwa korofi mbele yake hasa baada ya Trump kutangaza kuwa anaachana na makubalino ya nyuklia, licha ya kuonywa kutofanya hivyo na mtangulizi wake, Barack Obama.

Yote kwa yote, tuombee mkutano huo ufanikiwe ili dunia iwe sehemu salama zaidi ya kuishi. Marekani imesisitiza inaendelea na maandalizi ya mkutano. Inshallah!

Burundi yapigisha kura Nkurunziza kuongoza hadi 2034
Video: Mgongolwa afafanua kuhusu misamaha ya JPM kwa wafungwa