“Basi Yesu alipozaliwa katika mji wa Bethlehemu huko Yudea, wakati wa utawala wa mfalme Herode, wataalamu wa mambo ya nyota (mamajusi) kutoka Mashariki walifika Yerusalemu wakawa wakiuliza, kutoka kwao kuhusu wakati kamili ambao ile nyota ilionekana,” (Mathayo 2: 1-2).

Swali la wataalam hawa wa nyota kutoka Mashariki ambao walikuwa watu wa kwanza kugundua kuwa Yesu aliyetabiriwa alikuwa amezaliwa baada ya kuiona nyota yake walipokuwa mbali, wakijaribu tena kuuliza katika mji ule wa Bethlehemu kupata jibu kamili la wakati, bado ni kitendawili kinachotawala dunia hasa leo Desemba 25 ambayo inasherehekewa kama siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

Ukweli ni kwamba, hadi leo kitendawili cha siku aliyozaliwa Yesu bado hakijateguliwa na wasomi pamoja na wataalam wa nyakati kwakuwa siku hiyo haikuwekwa wazi kwenye vitabu vitakatifu.

Lakini leo, Desemba 25, nchi 160 duniani kote zinasherehekea sikukuu ya Krismas (Christmas) kama siku rasmi ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Mnazareti.

Kwanini leo?

Siku hii ina historia nzito na yenye misukosuko ya kiimani na kiutawala hadi kukubalika kwake kuhusishwa na kuzaliwa kwa Yesu.

Kabla ya kuzaliwa kwa Yesu, katika nchi za Scandinavia kulikuwa na sherehe kubwa katika msimu huu wa sikukuu, na zilikuwa zikianzia Desemba 21 na kudumu kwa kipindi cha siku 12. Kilikuwa kipindi cha katikati ya majira ya baridi/kipupwe (Winter solstice), wakati ambapo baridi ilipungua sana na kuanza dalili za kuonekana kwa jua. Ikumbukwe kuwa kipindi hiki hutokea mara mbili tu kwa mwaka, Juni 21 na Disemba 21.

Katika kusherehekea kurejea kwa jua, wanaume waliingia msituni na kukata magogo makubwa ambayo waliyatumia kuwasha moto na kuchomea nyama kwa ajili ya kusherehekea. Walichoma nyama hizo hadi magogo hayo yalipoteketea kabisa, na hii ilikadiliwa kuchukua siku 12. Ilikuwa ni sherehe ya kufurahia kukipita kipindi kigumu cha baridi kali na kukaribisha kipindi cha jua.

Bidii ya kuchoma nyama na kuwasha magogo makubwa ilitokana na kuamini kuwa kila cheche moja ya moto inayotoka ni ishara ya kuzaliwa kwa kondoo mpya katika kipindi kinachoanzia Januari mwakani.

Katika nchi za Ulaya, kilikuwa kipindi kizuri pia cha kukaribisha jua na kusherehekea.

Lakini tofauti na nchi nyingine, nchini Ujerumani watu walikuwa wakitoa heshima zao kwa mungu wa wapagani anayeitwa Oden. Waliamini kuwa vimondo vilivyokuwa vinapita angani alikuwa ni mungu Oden akiwatazama watu duniani na kuamua yupi afanikiwe zaidi kuanzia Januari mwakani na yupi aangamie. Hivyo, wote walikuwa wakiomba neema na huruma yake kwa mwaka ujao.

Hali ilikuwa ya aina yake katika msimu huu huko Roma. Watu waliokuwa wanaabudu miungu ya kilimo, walitumia wakati huu kufurahia wakati mpya ambao vyakula na vinywaji vilikuwa kwa wingi zaidi. Kitu tofauti zaidi kwao, ndani ya kipindi cha mwezi mmoja mfumo wa kijamii ulibadilishwa, watumwa walikuwa huru kwa muda na kuishi kama Mabwana. Masikini walienda kwenye nyumba za matajiri kudai vyakula, na wasipopewa waliruhusiwa kutumia nguvu kudai kwani matajiri walilazimika kuwapa vyakula.

Kikubwa zaidi huko Roma, Desemba 25 ilikuwa inasherehekewa kama siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa ya mungu jua aliyeitwa Mithra. Waliamini alizaliwa kutokana na miamba. Kwa warumi wakati huo, siku hii ilikuwa siku takatifu kuliko siku zote za mwaka.  Katika kipindi hiki, walitoa heshima zao kwa watoto wa Kirumi.

Sanamu ya muungu Mithra

Aidha, katika karne ya nne, Kanisa liliamua kutangaza mapumziko ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Lakini kwa bahati mbaya, Biblia haikutaja tarehe. Hivyo, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Julius wa Kwanza, aliichagua Desemba 25. Inaaminika kuwa alifanya uamuzi huo ili kuiteka siku ile ya wapagani iwe siku ya ibada na sherehe za Mungu wa kweli. Aliita ‘Feast of the Nativity’. Hii ilimeza sikukuu ya wapagani waliyoiita ‘Saturnalia festival’.

Na huo ulikuwa mwanzo wa sikukuu ya Krismas kuhusishwa na kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Katika karne ya tano ilisambaa hadi Misri, na karne ya sita ikaanza kukita mizizi nchini Uingereza. Na hadi mwishoni mwa Karne ya Nne, Siku kuu ya Krismas ilisambaa hadi katika nchi za Scandinavia, ikiwa ni Desemba 25.

Lakini, hadi leo, nchini Ugiriki na Urusi, waumini wa dini zinazofuata imani ya orthodox wanasherehekea siku ya Krismas siku 13 baada ya Desemba 25. Wao wanaamini kuwa wale mamajusi (wataalam wa nyota) walimpata mtoto Yesu siku hiyo.

Krismas kupigwa marufuku

Sherehe hizi za Krismas kukumbuka siku ya kuzaliwa kwa Yesu, zilipata misukosuko ya kupigwa marufuku katika baadhi ya nchi na tawala za kifalme.

Oliver Cromwell wa Uingereza aliposhika madaraka katikati ya Karne ya 17 (1645), alipiga marufuku sherehe za Krismas. Hata hivyo, kutokana na watu wengi kutaka kusherehekea siku hiyo, Mfalme Charles wa Pili alipoingia madarakani alirejesha sherehe hizo maarufu.

Kati ya mwaka 1659 hadi 1681, nchini Marekani, utawala wa Boston ulipitisha sheria ya kupiga marufuku sherehe za Krismas na yeyote ambaye alikutwa na hatia ya kusherehekea alitakiwa kulipa faini ya shilingi 5.

Ilibidi kusubiri hadi Mapinduzi ya Marekani (1765 and 1783) kupata kibali cha kusherehekea kwa uhuru Krismas. Juni 26 ya mwaka 1870 ilikuwa mara ya kwanza Desemba 25 kutangazwa rasmi kisheria kuwa ni mwanzo wa msimu wa sikukuu za Krismas nchini Marekani.

Kwetu, nchi za Afrika ambapo imani iliingia zaidi katika kipindi cha Karne ya 19 hadi 20 tulipata imani ya dini ya kikristo ikiwa tayari na mfumo wa sherehe za Krismas na Pasaka.

Hivi sasa, sherehe za Krismas zimesaidia kuondoa sherehe za kipagani na hivi sasa watu duniani wanamsifu Mungu wa Kweli na kukumbuka kuzaliwa kwa Mkombozi wa Dunia, Yesu Krito aliyezaliwa mjini Bethlehemu mkoani Yudea na kukulia Nazareti.

Nakutakia Heri ya Krismas. Ifanye iwe siku takatifu kwa kumuabudu Mungu na kukumbuka ukombozi wake kwako. Usiirejeshe kwenye siku chafu ya kipagani kwa kufanya yasiyompendeza Mungu.

Soma 2Wakorintho 7:1-4

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Desemba 26, 2018
Aliyemkimbiza bibi yake kwa fimbo atupwa jela

Comments

comments