Juzi misemo, “ukimwaga mboga namwaga ugali,” “vita vya nzige furaha kwa kunguru,” na “usilolijua ni usiku wa giza,” ilipata tafsiri ya vitendo baada ya Diamond Platinumz kuisimamisha mitandao akianika kwa mara ya kwanza vipande vya kilichoonekana kuwa ni ‘uovu’ wa mzazi mwenzake, Zari The Boss Lady.

Zari ambaye amemzalia Diamond watoto wawili hakukubali, kwa lugha ya kigeni kwenye masumbwi, she came back with a rabbit punch after being punched in the face. Yaani baada ya kupigwa konde la uso, alirejea na ngumi nzito ya kisogoni!

Lakini mashambulizi hayo ni hatari kwa watu muhimu kwenye maisha yao. Kwa bahati mbaya, tofauti na ndondi, watakaojeruhiwa zaidi kutokana na pambano hili sio wanaopigana! Ni wapendwa wao wa moyo…!

Tiffah na Nillan

Tukumbushane kidogo…

Hakuna anayefuatilia burudani ambaye hakuyafuatilia mahojiano ya Diamond akiwa anazindua vipindi vya redio yake ya ‘Wasafi’ kwenye kipindi cha Block 89. Hakika alifanikiwa kuipa umaarufu mkubwa sio ndani tu ya nchi hata nje ya nchi kupitia habari ‘mbaya’ kati yake na mzazi mwenza alizoamua.

Hakika, sio tu alimwaga mboga, Diamond alitupa hadi bakuli zilizokuwa na mboga. Kishindo cha mahojiano yale kama kilikuwa na maana ya kuipa umaarufu pia redio yake, kweli alifanikiwa. Nadhani alitumia falsafa ya ‘there is no such a thing as bad publicity’. Kipindi kiko nafasi ya pili kwenye gumzo #No2onTrending huku wimbo wake ‘The One’ ukiwa nafasi ya kwanza. Kwahiyo, amefanikiwa kuiteka mitandao, usipomuongelea utamuona au kusoma habari zake.

Nikukumbushe tu, katika mahojiano hayo, Diamond alidai Zari aliyekuwa mpenzi wake, alimsaliti kwa kuchepuka na Peter wa P- Square. Lakini pia, alidai mrembo huyo kutoka Uganda alichepuka na mkufunzi wake wa mazoezi! Hizo ndio tuhuma nzito zaidi. Mengine ni ya jinsi anavyomuwekea ugumu katika kuwaona wanaye walioko Afrika Kusini pamoja na jitihada alizofanya.

Sentensi nyingine inayong’ata zaidi ni kwamba ingawa yeye alikuwa anampenda Zari, ni Zari ndiye aliyekuwa anampenda zaidi na kwamba hata Babu Tale alipoenda Afrika Kusini kuwapatanisha ni yeye ndiye aliyekataa wasirudiane lakini mama watoto wake alikuwa anataka iwe hivyo. Kwenye hili nampa pongezi zaidi Zari kwa sababu Diamond amethibitisha kuwa alifanya kile ambacho alipaswa kukifanya kweli, sio tu Zari anajua kupenda bali anajua kupenda zaidi na ana moyo wa kujenga kuliko kubomoa.

Kadhalika, Diamond alianika kuwa alimfanyia vituko vingi Zari kama njia ya kumfanya aondoke mwenyewe. Hii inatupa kumbukumbu ya jinsi mama Tiffah alivyoamua kutundika daruga siku ya Wapendanao (Valentine’s Day) akiweka ua jeusi. Kumbe kwa Diamond ilikuwa siku ya mafanikio ya vituko vyake. Ni kama Zari aliona, ‘akufukuzae hakwambii toka,’ akanyoosha mikono juu.

Zari aliamua kujibu haraka kilichosemwa na Diamond hata kabla ya mahojiano kufika tamati, alikanusha kila tuhuma na kuwakumbusha watu kuwa anayewapa taarifa hizi ni yuleyule aliyewahi kuapa kuwa hajachepuka na hata kumkana mtoto [aliyezaa na Hamisa], na baadaye akarudi kukiri kuwa alichepuka na kupata mtoto.

“Mola akanipa Zari, kanizalia dume na mwali, nilivyomjinga nika-cheat aibu hadi kwa vyombo vya habari,” aliwahi kuimba Diamond kwenye ‘Sikomi’.

Lakini haya yote yaliyosemwa na ziada ya kuchimbua maisha ya ndani ya mahusiano na familia ya mastaa hao itakuwa kwa faida ya nani na hasara ya nani? Umaarufu huwa na kikomo na maisha mengine yataendelea, kizazi kingine kitakuja na mahojiano haya hayatafutika, kama watazidi kuwa wakubwa hata kwenye vitabu wataandikwa.

Ukiacha mbali mtikisiko unaoweza kutokea kwenye ndoa ya Peter wa P-Square, kikubwa zaidi ni kwamba watoto wao Nillan na Tiffah ndio waathirika wakuu wa majibizano ya wazazi wao tena yanayoanikwa hadharani. Watakapokuwa na uwezo wa kutambua na kuchambua, watayakuta yote mtandaoni. Ingawa watachukulia kuwa wazazi wao walikuwa mastaa, ukweli ni kwamba bado kisaikolojia inawaathiri na itazidi kuwaathiri sana.

Kabla sijakueleza madhara yaliyoainishwa kitaalam, naamini tutakubaliana kuwa utakuwa mwiba mkali kwa watoto watakapokuja kusikiliza na kusoma (sio kusimuliwa) stori ya ‘mama kumsaliti baba hadi na mkufunzi wake’, kwa mfano! au kumsikiliza baba akieleza/akijigamba kumfanyia vituko mama ili akimbie mwenyewe.

Kwa faida ya wote, kupitia mfano huu wa mgogoro maarufu wa kifamilia ulianikwa hadharani, tupitie madhara makubwa ya kiafya na makuzi yanayoweza kuwapata watoto.

Utafiti uliochapishwa na mtandao wa ‘verywellfamily’ wenye kichwa cha habari ‘How Parents Fighting Affects a Child’s Mental Health’ unaonesha kuwa familia zenye migogoro mikubwa huathiri afya ya akili ya watoto kuanzia wanapokuwa na umri wa miezi sita hadi miaka 19.

Tafiti zilizochapishwa, zimeeleza madhara ya kisaikolojia ya muda mfupi na ya muda mrefu yanayoweza kuwapata watoto.

Madhara ya muda mfupi kwa watoto:

Kwakuwa watoto huwa hawana ulinzi wowote wa kisaikolojia wa kuchuja, migogoro hiyo huwajengea uoga unaotokana na kuhofia watakachofanya wazazi/mzazi. Uhusiano kati ya wazazi na watoto huathirika sana, watoto huanza kujenga msongo wa mawazo taratibu ambao utaathiri afya yao ya kiakili na kimwili.

Madhara ya muda mrefu kwa watoto:

Hii nitakupitisha kidogo kwenye ripoti. Mwaka 2012 watalaalam wa kisaikolojia na mambo ya jamii walifanya utafiti uliochapichwa kwenye Jarida la ‘Child Development’. Watafiti walitumia taarifa walizozikusanya kwenye familia 235 za kipato cha kati na cha juu.

Kwanza, waliwahoji wazazi wa watoto ambao walikuwa wanasoma shule za awali wakati watoto wao wakiwa shuleni. Waliwauliza mmoja-mmoja kuhusu maisha yao na kama walikuwa na migogoro kati yao na kwa kiwango gani.

Miaka saba baadaye, wakati watoto wakiwa na umri mkubwa sasa, walirejea kwenye familia hizo na kuwahoji wazazi pamoja na watoto kwa nyakati tofauti. Waliulizwa kuhusu migogoro ya wazazi, tabia na mienendo yao pamoja na kuwafuatilia watoto hao kwa siku kadhaa.

Utafiti huo ulibaini kuwa watoto ambao wazazi wao walikuwa na migogoro mikubwa au walikuwa wakigombana mara kwa mara, walikuwa wakipatwa na msongo wa mawazo na kuwa na uwezekano wa kupata sonona, kuwa na uoga pamoja na tabia nyingine hatari kwa afya ya akili na mwili.

Athari nyingine kwa mujibu wa tafiti za kitaalam

  1. Utafiti uliofanywa mwaka 2013 na kuchapichwa kwenye Jarida hilo ulibaini kuwa watoto ambao wazazi wao walikuwa na migogoro walipata athari kubwa katika uwezo wao wa kutatua matatizo kwa haraka na kufikiri (cognitive performance).
  2. Migogoro ya wazazi inaweza kumsababishia mtoto matatizo ya uwezo wa kula vizuri yanayofahamika kitaalam kama anorexia na
  3. Mtoto anaweza kuathirika kitabia, wataalam wanaeleza kuwa mtoto anayetoka kwenye familia yenye migogoro mikubwa ana hatari ya kujiingiza kwenye tabia za uvutaji sigara, ulevi na hata matumizi ya mihadarati.
  4. Kama wazazi wanagombana wakati mtoto akiwepo, inaweza kuathiri uwezo wake wa kulala vizuri hata akiwa peke yake pamoja na matatizo ya kuumwa kichwa
  5. Utafiti uliofanywa mwaka 2012 na kuchapishwa kwenye jarida la Journal of Youth and Adolescence ulibaini kuwa watoto ambao wanashuhudia au wanafahamu kuhusu migogoro mikubwa ya wazazi wana hatari ya kupata matatizo ya kutojiamini na hata kuwa na mtazamo hasi kuhusu maisha yao binafsi.

Yote kwa yote, tafiti zilizochapishwa kwenye majarida mbalimbali ya kuaminika na yaliyopitishwa na Mamlaka husika duniani, zinaonesha kuwa kuna madhara hasi makubwa kwa afya ya akili na mwili ya mtoto ambaye wazazi wake wana migogoro mikubwa hasa mara kwa mara.

Hakuna familia ambayo haina migogoro au kutofautiana, lakini tofauti hizo zinapopata sifa ya kuwa ‘kubwa’, na zaidi kuanikwa hadharani ni hatari zaidi kwa watoto kuliko wazazi walio kwenye mgogoro.

Ni hayo tu! Maoni yako ni muhimu na tunayathamini bila kujali mlengo wa mtazamo wako… karibu kwa afya ya familia na Taifa kwa ujumla.

LIVE: Rais Magufuli akizundua msimu wa soko la Tumbaku Malawi
Video: Ukikutwa na mfuko mmoja wa plastiki faini sh30,000, CAG Assad aivuruga CCM

Comments

comments