Na Josefly: 

Naamini umewahi kusikia neno hili, ‘utani wa ngumi’! Huu ni utani anaomfanyia mtu mwenye hasira na wewe, au utani unaoakisi ukweli unaoumiza. Sasa hiki ndicho uongozi wa WCB unafanya dhidi ya Bosi wa Rockstar na Kings Music, Ali Kiba kufuatia ujumbe wake dhidi ya Diamond Platinumz uliozua gumzo.

Jana Ali Kiba aliandika ujumbe mkali akimvaa Diamond kwa kumtaja jina, saa chache baada ya mwimbaji huyo wa ‘The One’ kueleza kuwa wanafanya mawasiliano ili naye awe mmoja kati ya watakaoshiriki Wasafi Festival.

“Usiniletee mambo ya darasa la Pili unaniiibia penseli alafu unanisaidia kutafuta (UNIKOME).  Mwanaume huwa anaongeaga mara moja tu sasa ukitaka nikuweke uchi watu wajue unayonifanyia hata kwenye hilo tamasha hatokuja mtu sasa tuishie hapo nakutakia tamasha njema @diamondplatnumz. #KingKiba” ,” aliandika Ali Kiba.

Ni kama WCB wamechukua ujumbe wa Ali Kiba kwa mtazamo wa kuona kama ni sehemu ya kupandisha promosheni ya tamasha lao ambalo linafanyika kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam, Novemba mwaka huu.

Meneja wa WCB, Sallam jana aliingia kwenye kituo cha redio cha Wasafi akiwa na penseli na vifaa vingine vya kuandikia ambavyo hubebwa zaidi na watoto wa shule ya msingi na sekondari.

Mjadala wao ulijikita katika vifaa hivyo huku wakivitumia kulitangaza tamasha lao. Meneja huyo akiwagawia watangazaji kila mmoja penseli na karatasi, huku akitamba kuwa promosheni ya siku chache tu imewashtua watu na kwamba wanachohofia sasa ni kama uwanja utatosha.

“Sasa nimekuja na penseli na mkebe na karatasi, nitawapatia ili mchukue notisi ili nikiondoka tusilaumiane,”alisema Sallam.

WCB wamechukua mashambulizi ya Ali Kiba kama mtu aliyewatupia ganda la ndizi wakiwa wanakimbia, sasa wamelikanyaga ili liwaongezee mwendo kwa utelezi. Tujiulize,  Je, mwendo huo wa ganda la ndizi utakuwa na faida au utawachanganya?

Mtakumbuka Oktoba 2016, Ali Kiba alipokuwa anatumbuiza kwenye tamasha moja jijini Mombasa ambapo Chris Brown alikuwepo, alimlalamikia meneja wa WCB, Sallam kuwa ndiye chanzo cha yeye kukatishwa kuimba kwani alimuona nyuma ya jukwaa. Akajiuliza alifuata nini wakati yeye anaimba.

Lakini WCB walichukua madai hayo ya Ali Kiba na kuyafanyia utani; na hata Diamond aliingiza kwenye moja kati ya wimbo wake akionesha muziki umekatwa ghafla, kisha akamtuhumu Sallam. Ni ushindani wenye ladha ya utani.

Naamini mashabiki wa timu hizi bado hawajasahau matokeo ya ushindani wa ‘Seduce Me’ na ‘Zilipendwa’ na madhara yaliyozitokea timu zote mbili. Ilikuwa Agosti 25, 2017.

Kupitia tukio hilo, mwandishi mmoja nguli, rafiki yangu aliniambia amepata somo kuwa, ‘usichukulie poa nguvu yoyote ya mshindani wako’.

Nikukumbushe tu kwa haraka, Diamond aliingilia shughuli ya Ali Kiba akiachia ‘Zilipendwa’ saa chache tu baada ya mshindani wake huyo kuanchia ‘Seduce Me’.

Haikuwa tatizo kuachia kwa pamoja, lakini kabla ya kuachia alitanguliza kejeli ya aina yake dhidi ya wimbo wa ‘Seduce Me’. Na baadaye uongozi wa WCB uliendelea na kejeli ukitishia kuachia ngoma nyingine kubwa.

Diamond alifungulia jeshi lote la WCB, wakaishambulia Zilipendwa kwa nguvu. Nakumbuka gazeti moja kubwa liliandika kichwa cha habari, “Diamond amuundia Ali Kiba ‘Ukawa’.” Naamini unakumbuka vyama vya upinzani vilivyoungana kuunda ‘Ukawa’ dhidi ya Chama Cha Mapinduzi kwenye uchaguzi mkuu 2015. Hiyo ndiyo picha aliyoipata mhariri wa gazeti hilo.

Hata hivyo, kwa waliokuwa wanaweka alama kwa kutumia idadi ya watu walioangalia nyimbo hizo, ‘Seduce Me’ ya Ali Kiba ilikuwa mbele na ilikuwa ikiungwa mkono hadi na watu wakubwa Serikalini kama Mawaziri, walioiweka kwenye mitandao ya kijamii. Ilikuwa namba moja kwa gumzo (trending) YouTube ikifuatiwa na ‘Zilipendwa’.

Nguvu ya ushindani na madhara yake ikaonekana katika muda huo. Hata hivyo, baada ya kipindi cha joto hilo la ushindani kupita ‘Zilipendwa’ iliipiku ‘Seduce Me’ mara mbili. Hadi leo ‘Seduce Me’ imetazamwa zaidi ya mara milioni 11 huku ‘Zilipendwa’ ikiwa imetazamwa zaidi ya mara milioni 25 kwenye YouTube.

Wakati huu mambo yako kivingine, Ali Kiba na mashabiki wake wanashambulia upande wa WCB bila kuficha, na upande wa WCB wameona hili ni ganda la ndizi. Nani ataumia zaidi na nani atafaidika zaidi na mvutano huu hasa katika kuelekea Novemba kwenye tamasha?

Lakini kwa mtazamo wangu, hii ni familia ya Bongo Fleva. Rapa Jay Z kwenye wimbo wake ‘Family Feud’ alioimba na mkewe Beyonce, anasema ‘Nobody wins when the family feuds’.

Kwa tafsiri isiyo rasmi Jay Z anasema ‘hakuna anayeshinda familia inapokuwa kwenye mgogoro. ’

Watumishi watahadharishwa kugeuka Adui namba moja kwa serikali
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Oktoba 31, 2019