Kiu ya fedha na uzingatiaji wa maadili ya kazi yake vilimvuta mchekeshaji maarufu Afrika Mashariki, Emmanuel Mathias aka MC Pilipili na kumvika miwani ya kuondoa aibu kisha kusherehesha harusi kati ya aliyekuwa mwandani wa moyo wake Nicole na mwanaume aliyemnasa na kuamua kumuoa kweli!

Uvumilivu ulimshinda bwana Emmanuel, maumivu ya ndani yakajaa kibaba na kumwagika nje kwenye mitandao ya kijamii. Kwa mara ya kwanza, alilia na kuweka picha za kumbukumbu ya penzi lake na bibi harusi mpya. Kila mtu alimhurumia, alimpa pole huku wengine wakimkosoa vikali kwa kulilia kwenye mitandao.

MC  Pilipili hakuwa anachekesha tena, aliwahuzunisha na kuwafikirisha wengi!! Tuliishia kumpa pole, “ni mitihani ya dunia.”

Kilichong’ata zaidi, ni majigambo ya bwana harusi Mwijaku, aliyemnasa ‘ndege Tausi’ aliyekuwa akitanda kwenye moyo wa MC Pilipili, tambo za bwana huyu zilijaa maneno ‘yanayoudhi’ kwa mtu aliyeachwa.

“Jina lake tu pilipili, mwanamke gani anataka pilipili? Hapa mtoto amefika na hatoki,” alitamba mume wa Nicole.

Mahojiano ‘serious’ yalifanyika na bwana harusi yule kwa ‘macho makavu na uso usio na tone la haya’ alizungumza kama kweli ni tukio la kweli, akimchana MC Pilipili vilivyo. Nakubali yeye ni muigizaji, lakini kwenye mahojiano pale hakuwa anaigiza.

Lakini kwa upande wangu mimi ambaye nikiri niliwahi kufanya kazi na MC Pilipili kwenye taasisi fulani kwa kipindi fulani, nilimfahamu, mbali na ucheshi wake ni mtu mwenye busara inayoendana na taaluma yake ya ualimu na zaidi hupenda sana kusoma vitabu kuhuisha busara na kujiongeza. Nilishangazwa na sikuamini kama anaweza kuanika kwenye mitandao ya kijamii kilio chake cha mambo ya faragha tena baada ya kuhudhuria harusi ya huyo mpenzi wake.

Bibi Harusi Nicole Franklyn ambaye ni muigizaji amewahi kuwa mpenzi wa MC Pilipili na penzi lao linajulikana hadi ndugu jamaa na marafiki.

Hata hivyo, siku chache baadaye, giza hilo liliondolewa na mwanga wa video ya wimbo mpya wa nguli wa kughani na uandishi, Mrisho Mpoto ulioitwa “Nimwage Radhi.” ulionogeshwa na vibwagizo vya bwana Konde Boy wa WCB, Harmonize.

Mambo yakawa hadharani, kumbe picha zote na mbwembwe zote lilikuwa tukio la kushuti video ya wimbo wa bwana Mpoto!

Hakika kwa mtazamo wangu, ni wimbo mzuri sana, wa kipekee kutoka kwenye kinywa cha Mpoto. Tangu nianze kumsikiliza akirusha mawe gizani kwa wanasiasa kupitia ‘Mjomba’, kijamii kama wimbo ‘Wanangu’, leo ameyagusa mapenzi tena kwenye kilele cha mahusiano hayo (ndoa). Ujumbe mzuri, uandishi uliotukuka na uwasilishaji wa kipekee.

Video ‘kali’, wahusika wamefanya kweli, ni wimbo unaostahili sifa zote.

Kama mtu ninayejifikirisha, niliusikiliza na kuuangalia kwa makini wimbo huo ili kujiridhisha kama kweli ulihitaji ‘kiki’ ya namna ile ili uweze kuangaliwa au kutengeneza gumzo (trend) kwenye mtandao wa YouTube.

Nilijiuliza sana maswali haya, ambayo nimeyatunza nitamuuliza pia mhusika.

Je, ‘kiki’ hii ilipangwa kwa ushirikiano wa wahusika wote kwenye video ile na kubarikiwa na Mpoto?

Je, walijiuliza mara mbili madhara makubwa ya udanganyifu walioufanya kwa macho makavu?

Je, walijiuliza kesho yao na kesho ya vyombo vya habari vilivyosambaza udanganyifu huu kwa kasi.

Je, waliiona kesho ya muziki wa Bongo Fleva kwa jinsi wanavyomomonyoa imani ya muziki huo  kwa wadau na mashabiki?

Je, mambo haya wameiga wapi?

UEFA Champions League: Ni Ronaldo au Salah?

Kwa haraka tu, nimeona kosa kubwa lililofanywa ambalo wahusika wanapaswa kuwaomba radhi Mashabiki wa muziki pamoja na vyombo vya habari kwa kutozingatia ueledi wa kazi zao.

Hii inaweza kupoteza imani kubwa ya mashabiki kwa muziki wa Bongo Fleva, pale watakapoanza kushindwa kutofautisha kati ya ‘kweli na kiki za uongo’.

Fikiria, mtu mmoja aliyekuwa na tabia ya kupiga kelele na yowe usiku wa manane akidai amevamiwa, kisha majirani wanapofika wakiwa na silaha za kujihami, wamekatisha usingizi wao halafu anawaambia alikuwa anatania. Je, mara ya pili atakapovamiwa kweli akipiga kelele za yowe na miungurumo majirani hao watakatisha usingizi wao tena?

Mfululizo wa matukio yanayotengeneza ‘Kiki’ halafu baadaye tunaambiwa walikuwa wanatudanganya yameongezeka lakini la wimbo wa Mpoto nalo limekuwa ‘jambo’.

Kiki hii ilifuata mfululizo wa kiki ya Baraka Da Prince na Romy Jones ambao walianikana mitandaoni wakionekana kukosana baada ya Romy kumtaka Naj wa Baraka awe Mchepuko wake.

Wiki moja baadaye, ulitoka wimbo walioshirikishana!! Je, huu ni utaratibu mpya? Yaani ni kweli tumeshindwa kuvuta umakini wa mashabiki kiasi hiki hadi tutengeneze uongo mzito?  Namini hili ni bomu linalotegwa kuimaliza Bongo Fleva.

Wenzetu Wasanii wa Marekani wanajua jinsi ya kuandaa ‘public stunt’ kwa sababu waliokosea ikawa udanganyifu wa wazi hadi leo inawagharimu wanapokuwa na la maana, wamepoteza imani yao tayari kwa mashabiki. Mfano ni ile ya 50 Cent na Floyd Mayweather, hadi leo wakitofautiana tena hakuna anayewachukulia ‘serious’.

*Wanasema Mkubwa hakosei, bali mkubwa hutereza, husahau au hupitiwa. Mjomba Mpoto kama uliruhusu hili lifanyike, kweli ULITEREZA/ ulisahau/ulipitiwa na nakushauri uurejee umakini wako mjomba ili usitereze tena, uza muziki wako mzuri kwa ukweli na uhakika. Nakuamini sana, una ushawishi mkubwa sio tu kwenye Bongo Fleva, hata mbele ya viongozi wa dini na Serikali.

Hadi leo, ‘Nimwage Radhi’ inashika nafasi ya pili kwenye gumzo kupitia akaunti ya Harmonize (#2 trending), ikiwa imeangaliwa zaidi ya mara 705,400. Ninaamini mafanikio haya kwenye wimbo huu yangewezekana hata bila udanganyifu wa awali. Wangewekeza zaidi kwenye ‘promotion’ ya kweli kwa sababu wimbo na video vinakidhi vigezo vya kuwa gumzo.

Mfano mzuri na bora zaidi, ni mafanikio makubwa ya uuzwaji wa albam ya ‘Money Mondays’ ya Vanessa Mdee, kushika nafasi ya kwanza kwa mauzo Afrika Mashariki kwenye mtandao, bila kuwa na kiki au ulaghai wa kusababisha taharuki.

Nikiachana kidogo na Mpoto, naomba niguse wasanii wote kwa ujumla na tukumbushane ya nyuma.

Naamini Muziki ni maisha, yaani maisha ya msanii akiamua yanaweza kuwa sehemu ya muziki wake au akipenda isiwe hivyo anaweza kutofautisha. Mfano, AY, FA, Profesa Jay kwa wanaowafahamu tangu enzi walikuwa na maisha yao lakini hawakuwahi kuyahusisha na muziki. Lakini hadi leo ni nguli wasiopotea. Huo ni uamuzi wao.

Lakini ukiyahusisha maisha yako na muziki, tupe ukweli angalau unapoamua kusema au kuanika jambo.

Juma Nature na Sinta, waliwahi kuwa kama ‘Diamond na Wema Sepetu’ wa miaka hii. Albam ya ‘Ugali’ iliyopikwa na kupakuliwa ikiwa imejaa hisia za uhusiano wa Nature na Sinta iliuza sana kwa ubora wa kazi pamoja na uhalisia wa tukio lenyewe na sio udanganyifu.  ‘Staki Demu’, ‘Inaniuma Sana’ zilikuwa nyimbo kubwa za mkasa wa kweli.

Nawashauri sana wasanii wa Bongo Fleva wasiendelee kutengeneza bomu la kukosa uaminifu kisa ‘kiki’.

Kabla sijamaliza, nitumie maneno ya G-Nako, mwanafamilia wa ‘Weusi’, alipofanya Mahojiano na The Playlist ya Times Fm, alisema ‘Kiki ni upumbavu unaoua muziki, na kwa ndio kitu kinachomkera zaidi kwenye muziki’. “Kiki zinanikata sana.” Aliwasihi wasanii kutoharibu muziki kwa kiki bali wafanye kazi nzuri zitavuta mashabiki wa kweli.

Vyombo vya habari pia visikubali kutumika kuziuza ‘kiki’ zenye uongo wa wazi, nashauri twende ndani, tuulizane na kufuatilia hiki ni nini? ‘Investigative Journalism’ ikitumika kuwaanika wanaotafuta kiki kwa udanganyifu wa wazi, italinda pia heshima ya vyombo vya habari.

Yaliyopita si ndwele, tuamshane tugange yajayo ambayo naamini yanafurahisha. Hongera Mpoto kwa wimbo mzuri na wa kipekee. Heshima yako.

Pole kwa makala ndefu, maoni na mtazamo wako ni muhimu.

Kiumbe wa ajabu awavuruga Wanasayansi, washindwa kumtambua
Atakaye poteza pasipoti kulipia mara tatu zaidi ya gharama

Comments

comments