Wakazi wa Wilaya ya Ileje Mkoani Songwe wamehamasishwa kutunza Vyanzo vya Maji kwakuwa Maji hayana mbadala wa kitu chochote. Waziri wa Nchi mwenye dhamana ya Usimamizi wa Masuala ya Muungano na Mazingira  January Makamba amesema hayo leo katika muendelezo wa ziara yake ya kukagua mazingira nchini.

Akiwa katika Kijiji cha Ibungu Wilayani Ileje,  Makamba alishuhudia uchepushwaji wa Mto Kalembo ambao umefanywa kwa manufaa ya baadhi ya watu na haikuweza kufahamika mara moja muhusika, Aidha Makamba amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ileje  Joseph Modest Mkude kuhakikisha wanawabaini watu hao na kuwafikisha katika vyombo vya Sheria.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa wilaya ya Ileje imesema kuwa kumekuwa na uvamizi katika Vyanzo vya Maji na Serikikali imeendelea na juhudi za kuwaondoa wavamizi hao kwa kuwapatia maeneo mengine lakini baadhi ya wananchi  wamekuwa wakikaidi.

Makamba amesema ni muhimu watu kutii Sheria na Mamlaka zilizopo na ameagiza wakazi hao kupewa wiki mbili tu na baada ya hapo waondolewe kwa nguvu kwani tayari maeneo mbadala kwa makazi yao yalisha ainishwa, Pia Makamba ameahidi kutoa muongozo wa Sheria ndogo ndogo za Mazingira za Vijiji na Vitongoji ili zitumike kama nyenzo za hifadhi ya Mazingira Nchini.

Katika hatua nyingine  Makamba alitembelea Kijiji cha Lubanda Kata ya Lubanda na kufanya Mkutano wa hadhara na wananchi na kuwasisitizia kutokokata miti ovyo, kutochoma misitu na kuepuka uchepushaji wa Vyanzo vya Maji ikiwemo mito na Mabonde.

Aidha  Makamba amewashauri wakazi wa Lubanda kulima kilimo cha Matuta ama makinga maji ili kuepuka mmomonyoko wa udongo katika miinuko na ameunga mkono jitahada za wananchi wa Kata hiyo za ujenzi wa Kituo cha afya kwa kuchangia bati Ishirini na nane (28). Waziri Makamba anaendelea na ziara yake  katika Mkoa wa Rukwa.

Madiwani CUF wachapana ngumi kwenye kikao Tanga
Sauti Sol yaitoa kimasomaso Afrika Mashariki MTV MAMA, orodha Kamili