Waziri wa Nishati, January Makamba, Balozi wa Tanzania nchi za Nordic Grace Olotu na Bolozi wa Norway nchini Tanzania, Elisabeth Jacobsen wameshiriki katika warsha ya Viongozi iliyofanyika kwenye mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia (Liquefied Natural Gas Plant – LNG) wa Equinor.

Warsha ya mradi huo uliopo Kaskazini mwa Norway mjini Hammerfest pia ilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali na uongozi wa juu wa kampuni ya Equinor, na kuwapa nafasi ya kujadili maandalizi ya mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia Tanzania wenye thamani ya shilingi trilioni 70 Mkoani Lindi.

Aidha, Viongozi hao walitumia fursa hiyo kukutana na wafanyabiashara wa eneo hilo wanaonufaika kwa kutoa huduma kwenye eneo hilo la mradi wa Equinor, Hammerfest na kukutana na Watanzania wanaofanya kazi katika mradi huo.

Mtambo uliojengwa kwenye mradi huo wa Equinor huchakata bilioni 4.6 za mita za ujazo za gesi asilia kwa mwaka ikiwa ni pamoja na bidhaa nyingine kama gesi ya kupikia (LPG).

Sehemu ya miundombinu ya mradi wa wa kuchakata na kusindika gesi asilia nchini Norway.

Waziri Makamba aliwahakikishia Equinor na washirika wake kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha kuwa majadiliano yote ya msingi kuhusu mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia nchini yanakamilika ifikapo Desemba mwaka huu.

Tanzania kuendeleza maboresho biashara, uwekezaji
Bilioni 30 kulipa fidia wananchi Kabanga Nickel