Waziri wa Nishati, January Makamba amesema ni wakati sasa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO kuanza kujiendesha kibiashara, kwa ufanisi ili kuchangia uchumi wa Taifa.

Makamba amesema hayo wakati akizungumza na Mameneja wa TANESCO wa ngazi ya Kanda, Mikoa, Wilaya na Makao Makuu wakati akiwatambulisha Wajumbe wa Bodi ya TANESCO wakiogozwa na Mwenyekiti Omari Issa pamoja Mkurugenzi Mtendaji Maharage Chande, walioteuliwa Septemba 25, 2021 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Wajumbe wa Bodi ya TANESCO waliotambulishwa ni pamoja na Nehemia Mchechu, Zawadia Nanyaro, Lawrence Mafuru, Mhandisi Cosmas Masawe, Balozi Mwanaidi Maajar, Mhandisi Abdallah Hashim, Abubakar Bakhresa na Christopher Gachuma.

Makamba amesema Bodi iliyochaguliwa ina wajumbe kutoka nyanja mbalimbali na watasaidia Shirika kufikia malengo.

“Tunataka baada ya miaka mitatu Shirika liingie katika orodha ya mashirika bora, yenye thamani na yanayoheshimika Afrika” alisema January Makamba

Mkurugenzi Mtendaji, Maharage Chande ametaja vipaumbele ambavyo ni masilahi ya rasilimaliwatu, Wateja wa Shirika na utekelezaji wa mipango, hivyo ameomba ushirikiano kutoka kwa wafanyakazi wa TANESCO.

“Nimhakikishie Waziri tutahakikisha tunarudisha heshima ya Shirika na ufanisi kupitia ushirikiano wenu, hakuna Shirika lolote linalotoa huduma ya umeme zaidi yetu sisi, yamkini tuwape wateja wetu huduma wanayostahili”, ” alisema Bw. Maharage Chande

PICHA: Young Africans yaifuata Kagera Sugar
Kocha Nabi alia na muunganiko wa kikosi chake