Jeshi la Polisi nchini limesema askari wote wa kampuni binafsi za ulinzi nchini ambao watakuwa hawajapatiwa mafunzo na kusajiliwa kwenye Mfumo wa Uboreshaji wa Sekta ya Ulinzi Binafsi (PSGP) hawataruhusiwa kujihusisha na kazi za ulinzi baada ya Desemba 31, 2020.

Hayo yamebainishwa leo Februari 28, 2020 na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi, Narsis Msama katika kikao cha wamiliki na wakurugenzi wa makampuni binafsi ya ulinzi nchini.

Amesema endapo wahusika hawatafanikisha suala la kuwapatia mafunzo wafanyakazi wao na kuwasajili kwenye kanzi data ya PSGP Jeshi la Polisi litawazuia kufanya kazi kwani itakuwa ni kinyume na maelekezo ya jeshi hilo na maazimio ya kikao hicho.

“Kampuni ya ulinzi isiyotoa mafunzo kwa wafanyakazi wake na kuwasajili kwenye mfumo [wa PSGP] ina maana sisi tutamzuia mlinzi wake kufanya kazi; na hii ina maana kuwa kampuni itakuwa imezuiwa pia kufanya kazi mpaka pale watakapokamilisha taratibu husika,” amefafanua Kamishna Msama.

Awali, akiongea katika kikao hicho Mkurugenzi wa miradi wa Kampuni ya Data Vision International, Macmillan George amesema kwa ushirikiano wa wadau wa sekta binafsi ya Ulinzi na Jeshi la Polisi wamebuni mfumo wa kusimamia sekta ya ulinzi nchini ili kuhakikisha kuwa wadau kwenye sekta hiyo wanafaidika na wananchi wanapata huduma ya ulinzi yenye uhakika zaidi wa usalama.

Amesema mbali na hatua hiyo ambayo inakumbusha juu ya umuhimu wa utunzaji wa taarifa za makampuni pia mkutano huo umezindua rasmi utaratibu huo kwa kukutana na wakurugenzi hao wa makampuni binafsi 60 yanayotoa huduma za ulinzi Jijini Dodoma.

“Mfumo huu ni wazi kuwa utaratibu utunzaji wa kumbukumbu na taarifa mbalimbali katika sekta binafsi ya ulinzi kwa kushirikiana.na Jeshi la Polisi na ndio maana leo tumekutana hapa Dodoma na wamiliki wa kampuni binafsi za ulinzi,” amesema Goerge.

Aidha, George amebainisha kuwa mfumo huo pia utasaidia  kuhifadhi taarifa za watumishi wa sekta ya ulinzi binafsi ili kupunguza vitendo vya walinzi kuacha kazi kiholela na matukio ya uhalifu hakikiwemo masuala ya taarifa za afya na kifedha.

George ameongeza kuwa lengo kubwa la ubunifu wa mradi huo ni kuisaidia serikali katika kuratibu sekta ya ulinzi binafsi katika masuala ya kijamii kwa kuweka mikakati endelevu itakayosaidia kufikia malengo.

“Kama mnavyojua nchi haiwezi kuendelea au kupata maendeleo iwapo hakuna sekta ya ulinzi ambayo ni imara na ili uwe imara unahitaji mipango thabiti ya kimkakati ili kujiimarisha na kuleta matokeo chanya,” amefafanua Mkurugenzi George.

Naye Mkaguzi mstaafu wa Jeshi la Polisi George Nelson Andala ambaye pia ni Mkurugenzi wa kampuni binafsi ya ulinzi akizungumzia hatua hiyo amesema wameipokea kwa mtazamo chanya na wana imani itawasaidia katika mambo muhimu hasa taarifa za askari wao.

Amesema mradi huo ambao pia ni wa kuwasajili askari na watumishi katika sekta binafsi sio tu utawasajili na kutunza kumbukumbu bali pia utasaifia kuondoa dhana ya watumishi kuacha kazi kiholela na kuhama kampuni.

“Utunzaji huu wa kumbukumbu na usajili utawafanya askari kutambulika na hata kukopesheka na taasisi mbalimbali za kifedha kwakuwa taarifa zao zitakua ni halali na zenye uthibitisho wa mamlaka mbalimbali za kiserikali,” amefafanua Andala.

Urais wa JPM 'sumu' kwa Membe, Mbowe akamatwa baada ya mkutano Hai
Msekwa achambua Membe kufukuzwa CCM, ‘hata kama ni uamuzi wa kunyongwa’