Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo hii anatarajiwa kuwasili nchini Uingereza, jijini London kumuwakilisha Rais, John Pombe Magufuli katika Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 16 hadi 20 Aprili.

Mkutano huo ambao Kaulimbiu yake ni “Kuelekea Mustakabali wa Pamoja” utafanyika chini ya Uenyekiti wa Waziri Mkuu wa Uingereza, Mheshimiwa Theresa May na utafunguliwa na Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza.

Mkutano huo unatarajia kuzungumzia maeneo makuu manne ambayo ni , kukuza zaidi biashara na uwekezaji baina ya nchi za Jumuiya ya Madola kwa manufaa ya nchi wanachama na Jumuiya nzima; kukuza na kuendeleza misingi ya demokrasia; ajenda ya mabadiliko ya tabia ya nchi na maendeleo endelevu pamoja na masuala ya uhalifu wa kimataifa kama vile ugaidi, uhalifu wa kimtandao na usafirishaji wa binadamu.

Jumuiya ya Madola ilianzishwa mwaka 1949 kupitia Tamko la London ambalo lilikuwa ni matokeo ya Mkutano wa Mawaziri Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Madola. Jumuiya ya Madola ina wanachama 53 ambapo kati ya hizo, nchi 19 ni za Afrika, 7 ni kutoka Asia, 13 ni kutoka nchi za Carribean na Mabara ya Amerika, 11 ni kutoka eneo la Pacific na nchi 3 ni kutoka Ulaya.

Wajumbe wa Makamu wa Rais unajumuisha Mheshimiwa Dkt. Balozi Augustine Mahiga (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na viongozi wengine waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki.

Aidha Makamu wa Rais na wajumbe wake wanatarajia kurejea nchini Aprili 22, mwaka huu.

 

AS Monaco yawaomba radhi mashabiki, kurudisha fedha za viingilio
Karume Boys wafukuzwa Bujumbura