Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu amepongeza mipango na mikakati mizuri ya kampuni ya SportPesa ya kutaka kukuza vipaji vya wanamichezo hasa kwa mpira wa miguu kwa Tanzania Bara na Zanzibar.

Makamu wa Rais amesema hayo leo Juni 15, 2017  Ikulu jijini Dar es salaam mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa kampuni hiyo inayojishughulisha na ubashiri wa michezo ya ‘Sports Betting’ nchini, Abbas Tarimba na Mkurugenzi Mtendaji wa hiyo, Pavel Slavkov.

Amesema kama malengo ya kampuni hiyo yatafikiwa Tanzania itakuwa bora katika mchezo wa mpira katika bara la Afrika na Dunia kwa ujumla.

Aidha, Makamu wa Rais amekubali ombi la kuwa mgeni rasmi katika mchezo wa kirafiki kati ya timu ya Everton ya nchini Uingereza na timu ya Gor Mahia ya nchini Kenya ambayo ilitwaa kombe la michuano ya Sportpesa iliyofayika hivi karibuni hapa nchini.

Pia amewahakikishia watendaji wa kampuni hiyo kuwa milango ya ofisi yake ipo wazi na pindi wakikwama katika jambo lolote wawasiliane na ofisi yake ili tatizo linalowakabili liweze kutafutiwa ufumbuzi ili lisikwamishe shughuli za kampuni hiyo.

Naye Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa ‘SportsPesa, Tarimba Abbas amesema kuwa kampuni hiyo ina malengo makubwa ya kufanya biashara hapa nchini kwa kuzingatia sheria na kanuni za nchini.

Tarimba amesema katika mipango yao wanataka katika kipindi cha miaka mitatu ijayo kampuni yao iwe ni moja ya kampuni bora nchini katika ulipaji wa kodi kwa Serikali kama wanavyofanya kwa sasa katika Serikali ya Kenya.

Pia, amemshukuru Makamu wa Rais Samia Suluhu kwa kukubali ombi lao na kuwa Mgeni rasmi katika mchezo wa kirafiki kati ya Timu ya Everton ya nchini Uingereza na timu ya Gor Mahia ya Kenya mchezo ambao unatarajiwa kufanyika Julai 13, 2017 katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Tarimba amesema moja ya lengo la kuileta Everton nchini ni pamoja na kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii nchini kupitia mchezo huo ambao unatarajiwa kuangaliwa na maelfu duniani kote, na wameshawasiliana na mamlaka inayohusika na masuala ya utalii nchini ili iweze kutumia fursa hiyo kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini.

Maafisa mifugo watakiwa kubadilika
SPUTANZA Yatahadharisha Wachezaji Wanaosajiliwa