Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), umefunguliwa hii leo Machi 13, 2023 jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambapo ujumbe wa Tanzania unaongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Shaaban.

Katika ufunguzi huo, Mwenyekiti wa Mkutano ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mtangamano wa Kikanda wa DRC, Balozi Songhu Kayumba amesisitiza umuhimu wa wajumbe kushiriki kikamilifu, kwa kutoa maoni yatakayolenga kufanikisha utekelezaji wa agenda zitakazojadiliwa.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango ambaye ni Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC ngazi ya Makatibu Wakuu akiwa katika meza ya Tanzania wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa SADC unaofanyika Kinshasa, Jamhui ya Kidemokrasia ya Congo.

Aidha, Makatibu Wakuu wanajadili agenda mbalimbali ambazo ni pamoja na hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa Maamuzi ya Wakuu wa Nchi na Serikali waliyotoa katika Mikutano iliyopita, huku Tanzania ikishiriki kikamilifu na imejipanga kusukuma utekelezaji wa agenda ilizoziibua au kuziunga mkono katika mikutano iliyopita.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mtangamano wa Kikanda wa DRC ambaye ni Mwenyekiti wa Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu, Balozi Songhu Kayumba akisoma hotuba ya ufunguzi ya kikao hicho.

Agenda hizo, ni pamoja naujenzi wa sanamu la Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambalo litasimikwa kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU) na Tafsiri ya nyaraka muhimu za SADC katika lugha ya Kiswahili ambayo ni hatua muhimu ya utekelezaji wa matumizi ya lugha ya Kiswahili kwenye Jumuiya.

Wajumbe wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wanaoshiriki Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC, ngazi ya Makatibu Wakuu unaofanyika Kinshasa, Jamhui ya Kidemokrasia ya Congo.

Nyingine ni mpango wa Kanda wa Ununuzi wa pamoja wa bidhaa za Afya unaoratibiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD), na Mkakati wa pamoja wa Kanda wa Kusimamia Sekta ya Mbolea.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax, anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Baraza la Mawaziri utakaofanyika kuanzia Machi 18-20, 2023 baada ya Mkutano wa Makatibu Wakuu kukamilika.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Machi 14, 2023
Dkt. Tulia anadi juhudi za Tanzania udumishaji wa amani, mahusiano