Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekiweka mguu sawa kikosi cha kutuliza ghasia cha Field Force Unit (FFU) mkoani humo kwa ajili ya kuhakikisha oparesheni iliyotangazwa hivi karibuni na Chadema wakiipa jina la Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (UKUTA) haifanyiki.

Akizungumza wiki hii na viongozi wa kikosi hicho katika eneo la Ukonga Mkoani humo, Makonda alikitaka kikosi hicho kuhakikisha hakuna mtu hata mmoja atakayeathirika kwa namna yoyote na UKUTA kwani tayari Rais John Magufuli ameshatoa amri na wao wasisubiri kukumbushwa kuitekeleza.

‘Msisubiri maelekezo yoyote kutoka juu, asiwepo mtu yeyote akafunga duka kwa sababu ya UKUTA, nyie ni matrekta hakuna UKUTA unaweza kusimama mbele yenu, mimi kama Mkuu wa Mkoa ninaamini hatutakuwa na vurugu kwenye Mkoa wetu na hatuwezi kuruhusu vurugu kwa kuwa tunajua madhara ya vurugu’’ Alisema Makonda.

Makonda

Kamanda wa Oparesheni Kanda Maalum ya Dar es Salaam Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, (SACP) Lucas Mkondya alimhakikishia Mkuu huyo wa Mkoa kuwa hakuna atakayefanya UKUTA ndani ya mkoa wake kwani kikosi hicho kimeandaliwa vizuri tangu zamani.

Kamishna Mkondya alieleza kuwa yeyote atakayejaribu kufanya UKUTA atazimwa kabla hajatekeleza adhma yake.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza kufanya mikutano ya hadhara na maandamano nchi nzima ifikapo Septemba Mosi mwaka huu, kwa lengo la kuzindua UKUTA, wakipinga katazo la kutofanya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa hadi 2020.

Yusuf Manji Amjibu Mohamed Dewji "Mo"
Polisi wajipanga kumzuia Lissu kutumia mitandao ya kijamii