Shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF), kupitia kwa Rais wake Wallace Karia, limethibitisha kupata ushirikiano kutoka Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam katika maandalizi ya michuano ya kuwania kufuzu AFCON U17 mwaka 2019 kwa vijana kutokea katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Ameyasema hayo wakati wa mkutano wa pamoja kati ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda, TFF na wanahabari, ambapo amesema kuwa taratibu zote za mapokezi ya timu kutoka mataifa 12 zinaratibiwa kwa pamoja na ofisi ya mkoa pamoja na shirikisho na kila kitu kipo sawa.

”Kwa upande wetu maandalizi ya michuano hiyo itakayoanza Agosti 11 kwa kushirikisha timu 12, yameshakamilika ila tu tuishukuru serikali ya mkoa wa Dar es salaam kwa ushirikiano wanaotupatia kwenye mapokezi na usalama wa timu,”amesema Karia.

Aidha, kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda amesema kuwa wamejipanga kama mkoa kuhakikisha michuano hiyo inafanyika kwa mafanikio ili kurejesha imani kwa shirikisho la soka barani Afrika (CAF) na kusaidia kuendelea kupewa fursa ya kuandaa mashindano mengine.

Michuano hiyo ya vijana ambapo Tanzania tayari imefuzu fainali za mwakani kwa kigezo cha kuwa mwenyeji, inaanza Agosti 11 na kumalizika Agosti 26. Timu zitakuwa kwenye makundi mawili na zitacheza kwa mfumo wa ligi na baadae robo fainali, nusu na fainali. Bingwa atapata nafasi ya kuwakilisha Ukanda wa CECAFA kwenye AFCON U17 ya 2019

Ashikiliwa na Jeshi Polisi kwa tuhuma za kumkaba mama yake mzazi
Mateo Kovacic atikisa kibiriti Real Madrid