Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amemjibu msanii wa Bongo Fleva, Godfrey Tumaini maarufu kama ‘Dudu Baya‘ aliyetumia kurasa wake wa Instagram kutaja watangazaji 6 wa kiume katika tasnia ya habari akidai kuwa wanajihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Leo Makonda amezungumza na waandishi wa habari wakati akikabidhi magari kwa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Dar es salaam amemjibu msanii huyo aliyemuomba kuwashughulikia watu hao ikiwa ni pamoja na kuwapima ili kujihakikishia suala hilo.

Makonda amesema msanii huyo anatakiwa kufuata taratibu zilizowekwa kufikisha majina hayo sehemu sahihi ili yafanyiwe kazi ambapo ametaja utaratibu huo kuwa ni kutuma majina hayo kwa njia ya simu kwenye namba iliyopendekezwa na si kutaja kiholela.

“Nimesikia kuna watu wanatajwa, mtu anarekodi huku anataja, nilipoona mara ya kwanza nikasema tusingependa kuleta taharuki, hili zoezi tunatakiwa kulifanya kwa umakini sana, ikabidi nitafute namba yake ilki nimuombe kwamba ’embu tulia kwanza, taarifa kama unazo tutumie kwa meseji’.

“Nilichostuka ni kwamba jamaa (Dudu Baya) anasema wakipimwa wakabainika siyo mashoga, yupo tayari kufungwa jela, jamaa ana uhakika, ameniacha hoi, hawa wote amejuaje? Hii ni kama wachawi, wanaroga usiku lakini watu wanawajua kwamba flani ni mchawi,” amesema Makonda.

Aidha, Makonda amewaomba wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwa watulivu na kuendelea kutoa taarifa kupitia namba za simu zilizotolewa na vyombo vya ulinzi na usalama vitafanyia kazi huku akiwataka pia kukemea vitendo hivyo viovu.

Hatua hiyo ni kufuatia mkutano na waandishi wa habari ulioitishwa siku chache zilizopita na mkuu wa mkoa, Paul Makonda akisema ameunda kamati ya watu 15 watakaopambana na mashoga ambao wametapakaa hapa mjini hivyo msanii huyo aliamua kutumia ukurasa wake kuwataja watangazaji maarufu akidai kuwa wanajihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Tafiti zasaidia kupatikana kwa utatuzi wa changamoto sekta ya kilimo
RC Makonda aunga mkono mradi wa TACIP