Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salam, Paul Makonda amebaini uwepo wa harufu ya rushwa ya kutisha katika mkataba wa ujenzi wa jengo la Machinga Complex kati ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Makonda ameviambia vyombo vya habari kuwa ofisi yake ilifanya uchunguzi kuhusu mkataba huo hadi kukamilika kwa mradi husika na kubaini ongezeko kubwa la riba ya mkopo isilolipika, pamoja na mkataba uliosaniwa na pande zote mbili kabla na baada ya mradi kutofautiana kiuhalisia na mradi husika.

Alisema kuwa uchunguzi huo umebaini ongezeko la kiholera la shilingi milioni 560 katika mkopo husika, bila kuwepo kwa makubaliano ya kimaandishi kati ya pande zote mbili.

“Nimebaini kuwa fedha za mkopo ziliongezeka toka shilingi bilioni 12.14 za kwenye mkataba na kufikia bilioni 12.7 ikiwa ni nyongeza ya shilingi milioni 560, nyongeza ambayo ilifanyika bila makubaliano yoyote kati ya mkopeshaji na mkopaji, hali ambayo haimtendei haki mkopaji,” alisema Makonda.

Aidha, Makonda alisema kuwa barua ya makabidhiano haielezei uhalisia wa jengo husika lakini imesainiwa na pande zote mbili. Alisema barua hiyo inaeleza kuwa jengo lililokabidhiwa lina sehemu yenye ghorofa 5 na ghorofa 6 ili liweze kumudu idadi ya machinga wasiopungua 10,000 wakati hali halisi baada ya kutembelea jengo hilo inaonesha jengo lina ghorofa 4 zinazobeba machinga 4,000 tu.

“Kwahiyo, barua ya makabidhiano ilisainiwa na pande zote mbili licha ya ukweli kuwa maelezo ya jengo yalikuwa tofauti na jengo lenyewe,” alisema.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa ongezeko la riba lisilo na uhalisia wa makubaliano na kinyume cha makubaliano limepelekea kuongezeka kwa kiwango cha mkopo na kulifanya deni hilo kutolipika.

Alisema kuwa ingawa mkataba ulieleza wazi kuwa Halmashauri ya jiji ingepaswa kuanza kulipa deni baada ya kukabidhiwa mradi na mkopeshaji (NSSF) ambaye pia alichukua jukumu la kujenga jengo hilo, mkopeshaji huyo alianza kudai deni lake hata kabla ya kumkabidhi mdeni jengo hilo.

Kwamujibu wa Makonda, uamuzi wa kuanza kudai deni hilo na kuweka riba ulichukuliwa kuanzia tarehe iliyokuwa imekadiliwa kuwa mradi huo ungekuwa umekamilika lakini mradi huo haukuwa tayari hadi wakati huo. Lakini licha ya kuwa mradi ulikuwa bado haujakamilika, NSSF ilianza kudai deni lake na kuweka kiwango cha riba.

Alisema kuwa kutokana na kiwango cha riba kuanza kudaiwa tangu Desemba 31, 2008 tarehe ambayo mradi ulikadiriwa kuwa ungekuwa umekamilika lakini haikuwa hivyo, hadi siku ambayo NSSF inakabidhi mradi kwa Halmashauri hiyo, deni lilikuwa limefikia shilingi bilioni 19.7.

“Ikukumbukwe tu kwamba, wakati halmashauri ya jiji ikikabidhiwa mradi siku ya kwanza ilikuwa tayari inadaiwa kiasi cha bilioni 19.7 huku mpaka Machi mwaka huu deni lilishafikia kiasi cha bilioni 38 za kitanzania, kutokea kwenye mkopo wa bilioni 12.7,” alisema.

Katika mapendekezo yake, Makonda alisema kuwa kiwango hicho cha deni la shilingi bilioni 38 kutoka deni la shilingi bilioni 12.7 hakiwezi kulipika na kwamba kutokana kuwepo makubaliano ya pande mbili yasiyo na uhalisia kuna dalili zote za rushwa iliyolainisha mambo.

Ili kumaliza tatizo hilo la kimkataba, pamoja na mambo mengine, Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam amependekeza kuvunjwa kwa mkataba huo na NSSF kupewa eneo hilo pamoja na jengo kwa makubaliano. Alisema Halmashauri ya Jiji ilipwe kodi ya ardhi na NSSF baada ya kuchukua jengo hilo, jambo ambalo alisema linaweza kufanyika kwa urahisi kwa pande zote mbili kumiliki hisa kwa pamoja.

Serikali Yatoa Mwezi Mmoja Kwa Wanao Durufu Nakala Zake
Video: Baraza la sanaa Tanzania lamfungia Nay wa Mitego